Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Vijana zaidi ya 16,000 nchini wakiwamo wanaofanya kazi ya
kuuza vinywaji (Bar) wamenufaika na mafunzo mbalimbali ya ufundi stadi yanayotolewa
na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo
(VETA).
Yalielezwa hayo mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Mamlaka
hiyo, Dk. Pancras Bujulu alipozungumza kwenye semina ya siku moja kwa wanahabari
wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), kuhusu majukumu yanayosimamiwa na kutekelezwa na VETA.
“VETA imekuwa suluhisho la ajira kwa vijana wengi waliokosa
fursa ya kuendelea na masomo katika mfumo rasmi, kundi la wanaouza vinywaji
tuliamua kuwaanzishia kozi ya huduma kwa wateja ili waweze kuboresha kazi zao
wakati wanapotoa huduma,” alibainisha.
Aliongeza “Waajiri wengi hupenda kuajiri vijana waliosoma
hadi ngazi ya diploma, degree, masters na PhD, wale ambao hawajafikia ngazi hizo
huachwa.
“Ili kukuza sekta ya viwanda ni lazima tutambue kwamba
vinahitaji mafundi mahiri na wenye ujuzi wa kutosha, lengo la Mamlaka ni
kuhakikisha kinakuwa chuo cha VETA kila mkoa ifikapo 2025 ili kuzalisha nguvu
kazi ya kutosha,” alisema.
Dk. Bujulu alisema tayari wana mtandao mpana wa vyuo na
kwamba mikoa miwili pekee iliyosalia ambako bado hakuna vyuo vya Mamlaka hiyo
ni Simiyu na Songwe.
“Sasa hivi kuna miradi ya ujenzi wa vyuo vya VETA
unaendelea Kagera, Geita, Rukwa na Njombe, lengo letu pia kuhakikisha kila
Wilaya inakuwa na vyuo vyetu.
“Tayari kuna jumla ya vyuo 29 vinaendelea kujengwa katika Wilaya mbalimbali nchini baada ya Serikali kutenga kiasi cha Sh. bilioni 48 katika mwaka wa fedha 2019/20 kwa ajili ya ujenzi huo,” alibainisha.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (VETA), Dk. Pancras Bujulu akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa Klabu ya Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) mwishoni mwa wiki.
Chapisha Maoni