Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Baadhi ya wanaume waliojitokeza wakimsikiliza kwa makini, Dk. Kandali wa Ocean Road.

Na Veronica Mrema - Dar es Salaam

Watu zaidi ya 1,000 wamejitokeza katika viwanja ziliko ofisi za Efm na TV E, Kawe Beach jijini hapa ili kuchunguzwa afya zao na Wataalamu Mabingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), wanaume waliojiandikisha na kuchunguzwa kati ya hao ni zaidi ya 100.

Akizungumza na MATUKIO NA MAISHA BLOG, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, amesema hiyo inaonesha wazi kwamba elimu juu ya magonjwa ya saratani inazidi kufika kwenye jamii.

"Mwamko wa wananchi kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti unazidi kuongezeka kwenye jamii hadi kwa kundi la wanaume," amesema.

Dk. Kahesa amesema saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaowaona na kuwatibu Ocean Road na kwamba kwa mwaka takriban wagonjwa 800 huwa ni wenye saratani ya matiti.

"Mwezi Oktoba, kila mwaka duniani ni mahususi kwa ajili ya uelimishaji na uchunguzi wa saratani ya matiti, ili kuweza kuwagundua na kuwatibu mapema wagonjwa.

"Ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha, ORCI tumeshirikiana na Efm na ETV katika kuhitimisha kampeni ambayo tumeifanya mwezi mzima. Kampeni hii imetutia moyo, tunashukuru vyombo vya habari vimetusaidia.

"Si kitu cha kawaida kina baba kujitokeza kwa wingi namna hii hasa maeneo ya mijini ikizingatiwa pia ni mwisho wa wiki, hapa tumeweka vituo sita vya kufanya uchunguzi wa awali, vifaa na wataalamu tupo," amesema.

Ameongeza "Tunapenda kuhamasisha jamii washiriki uchunguzi wa awali ni bure kwa wale ambao hawatapata fursa kushiriki hapa leo (jana), tunawakaribisha kufika ORCI kule tunaendelea kutoa huduma hii kila siku.

Dk. Kahesa ambaye pia ni Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani amesema huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti zinapatikana nchi nzima ambapo Serikali imeweka mtandao wa vituo zaidi ya 700.

"Ocean Road ina wabobezi na vifaa vingi na huwa tunafanya huduma hizi za mkoba tunaifikia jamii kwenye makazi yao, tunatoa elimu kuhusu visababishi vinavyoweza kuongeza hatari ya mtu kupata saratani, tunahamasisha Jamii kujenga tabia ya kuchunguza mara kwa mara.

"Kwa sababu inaweza kugundua mapema na inapogundulika mapema inatibika na mtu kupona kabisa, sasa hivi Tanzania tunao mashujaa waliotibiwa na kupona baada ya miaka 20," amebainisha.

Naye, Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Kandali Samwel, amesema ingawa tafiti zinaonesha wanawake ndiyo huathiriwa zaidi na saratani ya matiti, inapowaathiri wanaume huwa kali kidogo.

"Kitaalamu tunasema inakuwa addresive' yaani inasambaa kwa haraka zaidi kuliko kwa wanawake, kwa sababu 

mwenendo wa matibabu yao huwa tofauti na wanawake," amesema.

Ameongeza "Hamasa kubwa tunayosisitiza ni watu kuchunguza mapema ili kuokoa maisha, kwani ikigundulika mapema inatibika na kupona kuliko mtu anapochelewa.

"Changamoto kubwa tunayoiona kwenye Taasisi yetu ni watu kufika wakiwa wamechelewa na ugonjwa ukiwa upo katika hatua za juu," amesema Dk. Kandali.

Meneja Mkuu wa Efm na TV E, Mohamed Lukwili amesema kwa kuwa mwezi Oktoba umetengwa maalum kwa uelimishaji kuhusu saratani ya matiti, waliona watumie nafasi hiyo kwa kushirikiana na Ocean Road kuelimisha na kuifikia jamii kuwapa huduma ya uchunguzi wa awali.

"Huu ni mwanzo, ushirikiano wetu ulianza sisi wafanyakazi wa Efm na TV E tulipokwenda Ocean Road na kufanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani, tukaona isiishie pale kwa sababu vyombo vya habari vinatazamwa kama muhimili wa nne kwenye nchi yetu, tunasikilizwa na wengi, maana yake tuna nafasi kubwa kushawishi watu wafahamu hali zao.

"Hivyo, leo tumewakusanya wanaume kwa wanawake ili wapate nafasi ya kupima saratani ya matiti na tezidume kwa wanaume, tangu saa mbili asubuhi hadi kufikia saa tisa jioni, tumeandikisha watu zaidi ya 1,400, lengo letu ni kuwezesha wengi zaidi wafanya uchunguzi hata wakifika 2,000 tutawahudumia.

"Kwa sababu tunafahamu saratani ni ugonjwa unaotesa ndugu zetu wengi Tanzania, tunapopata wananchi wengi zaidi inamaanisha waligundulika mapema tutakuwa tumeokoa wengi zaidi," amesema.

Ameongeza "Mwamko ni mkubwa wamefika hata wenye umri wa miaka chini ya 18 jamii imeelimika kwamba magonjwa haya si tu yanatesa wazee bali hata watu wa rika nyinginezo wanaathirika.

Mkazi wa Kawe, Ibrahim Yasin amepongeza uongozi wa Efm & TV E na Ocean Road kwa kuungana na kuwafikishia huduma hiyo karibu.

"Nimetamani hata waongeze siku, kwa kweli nimehamasika kufanya uchunguzi baada ya kusikia jinsi wataalamu walivyokuwa wakieleza redioni magonjwa haya yanavyotesa wengi, lakini kumbe tunaweza kuyaepuka kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha, nimechunguza saratani ya matiti na tezidume, Niko vizuri, namshukuru Mungu," amesema.

Naye, Frida Jumanne ameomba huduma hiyo kufanyika mara kwa mara ili kuwezesha wengi zaidi kufikiwa moja kwa moja kwenye jamii, kule waliko.

"Kwa sababu, unajua tena sisi Watanzania tulio wengi maisha yetu ni kutafuta riziki kila siku, baadhi tunajikuta muda unakuwa mchache, kuweza kwenda hospitalini kufanya uchunguzi wa afya, lakini wanapokuja kwenye maeneo yetu, tunaacha shughuli mara moja tunasogea, tunachunguzwa na kurudi kwenda kufanya kazi," ameshauri.

Baadhi ya wanaume waliojitokeza wakiwa kwenye foleni ya kuingia katika Kituo cha uchunguzi wa awali ya saratani ya matiti.
Dk. Kandali akizungumza na wanawake waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani, Dk. Crispin Kahesa akifanyiwa mahojiano na watangazaji wa Efm/TV E.
Wananchi wakisubiri kuhudumiwa.
Wananchi wakisubiri kuhudumiwa.

Picha zote na Veronica Mrema, Matukio na Maisha Blog.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement