moja

Responsive Advertisement

 

Na Veronica Mrema

Goti la kulia la Hamza Mussa bado lina makovu ya alama katika sehemu ambako yalikita meno manne ya mbwa, alipong’atwa akiwa na umri wa miaka 13 huko Kijijini Ihemi, Mkoani Iringa.

Hamza anasema amewahi kusikia simulizi kuhusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ni jambo linalompa wasiwasi mkubwa kila anapotafakari hata hivi sasa.

Anasema amesikia watu wakisimulia ni ugonjwa hatari unaoua haraka lakini hajawahi kumuona mtu aliyeugua.

Anasema amewahi kusikia pia watu wakisema kule kijijini, maafisa wa afya husisitiza mtu aking’atwa na mbwa anapaswa kuwahishwa hospitalini kupatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Hata hivyo, yeye alipong’atwa, hakupelekwa hospitalini kupatiwa chanjo, alitibiwa kwa tiba asili (mitishamba).

“Bibi yangu alitumia maji ya vuguvugu aliyachanganya na chumvi, vile vile mafuta ya taa pamoja na ‘uji mzito mithili ya tope’ uliotengenezwa kwa kutumia mitishamba aliyoichukua porini,,” anasimulia.

NI MBWA ASIYEJULIKANA

Hamza anasema mbwa aliyemng’ata kule porini hakuna mtu aliyekuwa akifahamu ni wa nani, mara nyingi alionekana kuranda randa huku na kule pale kijijini kisha kutokomea porini.

“Kumbe ndiko yalikuwa makazi yake, nakumbuka ilikuwa kipindi ambacho shule za msingi zilikuwa zimefungwa, nilikwenda kijijini kumsalimu bibi yangu, nilipopata mkasa wa kung’atwa na mbwa huyo.

Anasimulia “Mimi na marafiki zangu mara kwa mara tulipenda kwenda porini kutafuta matunda yaitwayo Mitusu, yana ladha nzuri, ni maatamu mno pindi yanapoliwa.

“Siku moja tulipokwenda, pembezoni kidogo mwa mti wa matunda tuliona ‘vitoto vidogo’ vya mnyama ambaye awali hatukuelewa ni yupi.

Anasema walivutiwa na ‘vitoto’ vile vya mnyama, waliamua kuvisogelea ili kudadisi zaidi kujua vilikuwa vya mnyama gani?

“Nilichukua ‘kitoto’ kimoja kati ya ‘vitoto’ sita vilivyokuwapo, nilikiangalia kwa umakini mkubwa, nilibaini vilikuwa vya mbwa.

“Lakini wenzangu walinikatalia, porini siku ile tulikwenda watoto wapatao sita, wenzangu walisema ni vya simba, lazima tuondoke eneo lile haraka kwa sababu ni hatari endapo angetukuta,” anasimulia.

NILIBAKI MWENYEWE

Anaongeza “Ghafla katika hali ambayo nilibaki nimeduwaa, nilishangaa wenzangu wakitimua mbio na kutokomea ambako sikupajua, nilibaki mwenyewe na ‘vitoto’ vile.

“Nikiwa nimeshika mkononi mwangu ‘kitoto’ kimoja, ambacho nilikusudia kuondoka nacho nyumbani nika-katunze kwa sababu nilikapenda, kalikuwa kazuri mno, nilipoangalia mbele yangu nilistaajabu.

“Nilimuona mbwa mkubwa, niliyemfahamu, yule mzururaji kule kijijini asiyejulikana ni wa nani na wana-kijiji walishawahi kupendekeza auwawe, ndipo nilibaini yale ni makazi yake, porini.

“Alikuwa anakimbia kwa kasi kuja pale nilipokuwa nimesimama, bado nikiwa nimebeba ‘kitoto’ chake, sikuelewa nifanye nini, niliduwaa, lilikuwa tukio la ghafla mno, aliponifikia alirukia na kuning’ata katika goti langu la kulia,” anasimulia Hamza.

Anasema alijikuta akianguka chini, alihisi maumivu makali na damu nyingi zilimvuja, alipiga yowe kuomba msaada.

“Bahati nzuri jirani na eneo lile kulikuwa na watu wazima waliokuwa wakipita, walikuja mbio na kufanikiwa kuniokoa,” anasimulia.

MAFUTA YA TAA

Hamza anasema watu wale waliomuokoa walimpeleka haraka nyumbani kwa bibi yake ambaye hata hivyo hakumpeleka hospitalini, alitibiwa nyumbani kwa mitishamba.

“Niliugulia maumivu makali, hamu yote ya kufuga mbwa ilinitoka, goti langu lilikuwa bado likivuja damu, yale meno yalikita kwa nguvu mwilini mwangu.

“Bibi alichukua maji masafi na kuyabandika jikoni, aliyachemsha kwa dakika kadhaa na kuepua, aliyatumia kunifuta kwa kitambaa safi zile damu zilizokuwa kwenye jeraha.

“Baada ya hapo, alichukua maji ya baridi na kuweka chumvi kiasi, akayatumia pia kunifuta, alipomaliza alichukua mafuta ya taa na kuyaweka pale kwenye jeraha,” anasimulia.

Anasema wakati maji yalipokuwa jikoni tayari bibi yake alikuwa amechana kipande cha kanga ambacho alikianika juani kikauke.

KIJITI CHENYE ‘UJI’

“Alipomaliza kuniosha, alikwenda kutafuta kijiti porini ambacho sikumbuki kilikuwa cha kutoka kwenye mti gani, alikuja nacho alikisugua sugua kwenye jiwe kikatoa unga unga mwingi.

“Alilowanisha ule unga unga kwa maji ya vuguvugu, alitengeneza mfano wa uji mzito kama tope, alinibandika pale kwenye jeraha, aliniacha ukakauka kabisa.

“Alichukua kile kipande safi cha kanga alichokianika, lile ‘tope la uji’ lilikauka, hivyo alinifunga jeraha lile, nilikaa navyo kwa muda wa wiki mbili, jeraha likawa limefunga kabisa, kidonda kilikauka, kilipona,” anasimulia.

IMANI MITISHAMBA

Hamza anasema kule kijijini si bibi yake pekee ambaye huamini  mitishamba inazuia ugonjwa wa kichaa mbwa.

“Wengi wana imani hiyo, wale ambao hawana imani ndiyo ambao hukimbilia hospitalini, kwa mfano yupo rafiki mmoja ambaye aling’atwa na mbwa lakini familia yao haikuamini mitishamba yeye alipelekwa hospitalini.

“Kidonda chake kilichelewa kupona tofauti na mimi nilipotibiwa kwa mitishamba changu kilipona haraka,” anasimulia.

Anaongeza “Kidonda changu kilifunga haraka, ingawa naamini nimepona lakini kwa jinsi watu wanavyosema kuhusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwamba ni hatari, sikupata chanjo, kuna wakati nafikiria kuhusu hilo, huwa napata wasiwasi, ni ugonjwa ninao-uogopa mno.

NJIA PANDA?

Je! ni kweli chumvi, mafuta ya taa, maji ya vuguvugu na mitishamba vilivyotumika kumtibu Hamza, alipong’atwa na mbwa ni tiba sahihi katika kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa kama  inavyoaminiwa?

Jubileta Bernard ni Mtaalamu wa Elimu ya Afya kwa Jamii wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anasema hadi sasa hakuna dawa inayozuia (inayotibu) ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani.

Anasema jeraha lililotokana na kung’atwa na mbwa halipaswi kufungwa na hutakiwa kusafishwa kwa sabuni na maji tiririka kwa takriban dakika 10 hadi 15 au kwa kutumia ‘spirit’.

“Hakipaswi kufungwa, kinapofungwa hali hiyo huruhusu virusi kuzaliana na kuongezeka, kisipofungwa virusi huishiwa nguvu kwenye mwanga hasa wa jua.

“Baada ya kuosha, mtu anapaswa kuwahishwa kituo cha afya kilichopo karibu apatiwe chanjo, taarifa inapaswa kutolewa pia kwa mtaalamu wa mifugo wa eneo husika,” anasema.

Anafafanua “Kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya ‘Lyssa’ ambavyo hushambulia mfumo wa fahamu, huambukizwa kwa kung’atwa au kulambwa sehemu yenye jeraha  lililo wazi na mnyama mwenye virusi hivyo.

“Virusi hivyo husafiri kutoka kwa mnyama mwenye ugonjwa kwenda kwa asiye na ugonjwa kupitia mate pindi anapong’ata au kulamba jeraha lililo wazi kwa mnyama asiye na ugonjwa,” anabainisha.

Anasema vimelea vya ugonjwa huo vinapoingia mwilini mwa mnyama aliyeng’atwa au kulambwa hushambulia neva za fahamu kuanzia eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgonjwa hatimaye kuathiri ubongo na kusababisha kifo.

Jubileta anasema binadamu na hata wanyama wengine wafugwao kama mbwa, paka, mbuzi, kondoo, ng’ombe na wengineo huweza kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

“Wanyama waishio porini akiwamo fisi, nguchiro na wengineo nao huweza kuambukizwa ugonjwa huo waking’atwa na mnyama aliyeathirika, lakini wao huchelewa kuonesha dalili kama ilivyo kwa mbwa,” anasema.

Anaongeza “Kwa kuwa ni vigumu kumbaini, kumjua mbwa aliye na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo, tunahimiza jamii kuhakikisha mbwa wanapatiwa chanjo angalau mara moja kwa mwaka, kuwakinga.

“Pia, tunasisitiza ni muhimu tukio lolote la kung’atwa na mbwa  litolewe taarifa kwa wataalamu wa afya au mifugo, ugonjwa huu hauna tiba kwa binadamu au mnyama yoyote mara tu anapoanza kuonesha dalili.

HUJITOKEZA KWA MUDA GANI?

Jubilate anasema kwa upande wa wanyama dalili za ugonjwa hujitokeza kati ya siku mbili hadi 45 au zaidi tangu alipong’atwa na mbwa mwenye virusi hivyo.

Anatoa mfano, mbwa mwenye dalili za ugonjwa hubadilika tabia, huwa mpole au mkali zaidi, hupenda kushambulia na kuuma vitu mbalimbali kama vyuma, vijiti, huangaika huku na kule na hata kukimbia ovyo.

“Hushindwa kula na kunywa maji, hutokwa mate mengi, hudhoofu, hupooza mwili hatimaye kifo, dalili kama hizi zinaweza kuonekana pia kwa wanyama wengine ambao huambukizwa ugonjwa huu kama nilivyowataja awali,” anasisitiza.

Mtaalamu huyo anasema kwa upande wa binadamu dalili huanza kujitokeza kati ya wiki moja hadi mwaka tangu alipong’atwa na mnyama mwenye ugonjwa huo.

“Lakini hutegemea pia ukubwa wa jeraha na eneo ambako aling’atwa au kulambwa, kwa mfano ikiwa aling’atwa sehemu ya kisigino na jeraha lenyewe ni dogo, dalili huchelewa kujitokeza.

“Ni tofauti na yule atakayeng’ata sehemu za shingoni au kichwani, kwa sababu ni karibu zaidi na ubongo, inatarajiwa kwamba dalili zitawahi kuonekana,” anafafanua.

Anaongeza “Huwa inategemea pia kinga ya mwili ya aliyeng’atwa na mbwa mwenye virusi, ikiwa kinga zake zipo juu mwili huweza kupambana navyo hali hiyo hufanya dalili kutojionesha haraka.

“Kinga za mwili zikishuka ndipo dalili huanza kujitokeza, hutegemea pia na kiwango au idadi ya virusi vilivyoingia mwilini, kwa mfano kama mtu aling’atwa sehemu ndogo na mbwa yule alikuwa na virusi, vikiingia vichache mwilini, maana yake vitachukua muda mrefu kuzaliana, kusafiri hadi kufika kwenye ubongo pia vitachukua muda mrefu.

“Tofauti na aliyenyofolewa nyama kubwa, atachukua muda mfupi kuonesha dalili, wapo ambao huonesha dalili siku mbili hadi miezi mitatu na wapo ambao huonesha dalili baada ya kipindi kirefu kupita,” anasisitiza.

Anataja dalili zinazojitokeza kwa binadamu ni “Maumivu ya mwili, kuwashwa sehemu ya jeraha, kuona vitu ambavyo havipo, maruweruwe hivyo kufanya mgonjwa ajifiche au kukimbia.

Anataja dalili zingine ni kuogopa maji (hydrophobia), kupata nguvu za nyingi hadi kufungwa kamba, mwili kupooza, kushtushwa na mwanga na kelele mwishowe kupoteza fahamu na kufa.

IMANI POTOFU

Anasema zipo jamii zinazoamini ni ugonjwa wa kurogwa jambo ambalo si kweli na wengi hubaki majumbani pasipo kwenda kupata chanjo.

“Ni muhimu mtu kupata chanjo mapema kwa sababu anapochelewa na zile dalili kuanza kujitokeza huwa hakuna tiba dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa na matokeo yake huwa ni kifo, dozi za chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa kwa binadamu ziko za aina mbili.

“Ipo ambayo hutolewa kwa dozi nne na nyingine dozi tano,  kwa chanjo ya dozi tano (IM) huanza kutolewa kuanzia siku ya kwanza (sifuri), dozi ya pili siku saba, dozi ya tatu siku ya 14, dozi ya nne siku ya 21 na dozi ya tano siku ya 28.

“Kwa upande wa dozi nne (ID) huanza kutolewa siku ya kwanza, siku ya saba, siku ya 14 na siku ya 28 hukamilika,” anabainisha.

Anaongeza “Mtu asipomaliza dozi za chanjo hizo ipasavyo mwili wake hukosa kinga kamili  kama inavyotakiwa ugonjwa huwa kwenye uwezekano wa  ugonjwa kukua na kuleta athari.

“Tunashauri mtu kumaliza chanjo ili mwili wake upate kinga ya kutosha ugonjwa usiindelee,” anasisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement