Na Veronica Mrema – Kigoma
Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS – Kigoma) ambalo
ujenzi wake ulisimama kwa miaka 26 hatimaye unatarajiwa kukamilika mapema ifikapo
Desemba, mwaka huu, jengo linatarajiwa kuwa ndilo litakalokuwa likitumika katika uchakataji wa data za Sensa ya Watu na Makazi nchini.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria katika Maadhimisho ya
Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika Kitaifa Mkoani hapa katika Viwanja ambako
ndipo zikapokuwa ofisi za NBS, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa (mwenye blauzi na suruali nyeusi pichani) alibainisha hayo.
Dk. Albina alisema jengo hilo ndilo litakalotumika ipasavyo
na kazi yake kuu ni kukusanya na kutoa uchambuzi wa mwanzo (basic analysis)
katika ngazi ya mkoa na wilaya kwa kushirikiana na watakwimu wa mikoa, wilaya
na halmashauri zake pia wadau wengine.
“Tunatarajia kwamba Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022
data zote zitakazokusanywa zitaletwa hapa na kazi zote zitafanyika hapa hapa
hadi zitakapokamilika,” alibainisha.
Aliongeza “Leo (jana) tunapata fursa ya kukagua jengo hili
ambalo ndipo ilipokuwa Idara Kuu ya Takwimu nchini mwaka 1994 ilianza ujenzi
ikishirikiana na Ofisi ya Takwimu Sweden.
“Ni takriban miaka 26 sasa jengo lenye ghorofa mbili
lilishindikana kumalizika kwa wakati, sote tulijiuliza ‘Kwa nini?’. Serikali ya
Awamu ya Tano imeamua kwa dhati na kutoa fedha Sh. milioni 684 kumalizia ujenzi
na ifikapo Desemba, mwaka huu litakuwa limekamilika,” alisema.
Alisema hilo ni jambo kubwa na deni kubwa ambalo NBS inayo kwa
watakwimu kuhakikisha wanalilipa kwa kujituma zaidi kwa kutumia maarifa na
juhudi na Mungu aendelee kuwatia nguvu
“Serikali kwa sasa inahitaji takwimu rasmi kwa wingi zaidi
katika sekta zote kuliko ilivyokuwa jana, wana-Kigoma hili ni jengo la kwanza kujengwa
katika ngazi ya Mkoa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambayo imekuwako tangu 1947
nchini.
“Hatuna budi kumshukuru Rais. Dk. John Magufuli na
kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kwa kuchaguliwa na
wananchi wa Buhigwe Kigoma na imani kubwa ya Rais. Magufuli aliyonayo kwa Dk.
Mpango kwa utendaji kazi wake.
“Kama mnavyokumbuka Dk. Mpango alipokuja kuweka jiwe la
msingi Julai, 2020 aliniagiza ‘Dk. Albina Chuwaa’ hakikisha jengo hili
linakamilika na kwa ubora unaostahili, sote ni mashahidi tunaona kasi
inayoendelea katika ujenzi huu na litakamilika ndani ya mwaka huu 2020,”
alisema.
Alisisitiza ujenzi wa jengo hilo unafanyika usiku na mchana kuhakikisha lengo hilo linatimia kwa wakati alioagizwa na kwa ubora unaostahili.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga (mwenye suti ya bluu pichani) akielezwa jambo na maofisa wa NBS wakingozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk. Albina Chuwa.
Chapisha Maoni