Waziri Gwajima akizungumza na wagonjwa hao hii leo.
Mkazi wa Dar es Salaam, Mbwana
Said, ametamani kuchana kipande cha shati lake na kumpatia Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, akidai kwamba
anavutiwa na utendaji kazi wake.
Said ni miongoni mwa wagonjwa
waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala hii leo ambako Waziri
Gwajima alifanya ziara kukagua namna wanavyotoa huduma kwa wananchi.
“Ingewezekana mama (Dk. Gwajima),
ningeomba leo nichane kipande cha shati langu, uende nacho kiwe ukumbusho
kwako, hongera kwa kufanya kazi nzuri,” amesema Said mbele ya hadhara iliyokuwa
imeambatana na Waziri huyo kila mmoja akijikuta anaangua kicheko.
Awali, Said na wenzake, Leila
Mussa na Salma Juma walimueleza Waziri huyo kwamba wanaishukuru Serikali kwa
kuendelea kuboresha huduma za afya, hata hivyo kilio kilichopo sasa ni kuhusu
gharama za matibabu.
Waziri Gwajima aliwauliza iwapo
wanafahamu kuhusu suala la kukata bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF),
Said alisema yeye amekwisha kukata, lakini Leila na Salma walishangazwa na
jambo hilo kwamba hawalifahamu.
“Binafsi sijui, kama kuna hiyo
bima naomba nieleweshwe ili nikate, maana ninaugua kisukari, gharama za dawa ni
kubwa kuna wakati nashindwa kumudu na sisi wagonjwa wa kisukari wakati mwingine
huwa tunapata vidonda,” amemueleza Waziri Gwajima.
Kutokana na hilo, Waziri Gwajima
ametoa maelekezo kwa waganga wakuu wa mikoa, wilaya na timu wanazoziongoza za
afya na ustawi wa jamii, kuhakikisha zinajipanga kwenda ngazi ya chini ya jamii
ili kutoa elimu kwa wananchi.
“Inanishangaza, wananchi wanataka
kujiunga, hawana taarifa, mnafanya nini?... ofisa ustawi wa jamii, anastawisha
nini?..,” amehoji.
Waziri huyo amesisitiza “Serikali
inaelekea katika bima moja, lazima wananchi waelimishwe na wakate bima ya afya.
Chapisha Maoni