Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Daktari mmoja wa Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa Amana, yupo matatani kwa madai ya kuchukua rushwa ya kiasi cha Sh.
700,000 kutoka kwa mgonjwa mmoja (majina yamehifadhiwa) na kumfanyia upasuaji
hospitalini hapo, pasipo uongozi kujua.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima (aliyevaa kitenge pichani) ameweka wazi hilo leo
alipotembelea hospitali hiyo kukagua hali ya utoaji wa huduma.
Amemuelekeza Mganga Mfawidhi wa
Amana, Dk. Amani Malima kuhakikisha daktari huyo anafuatilia suala hilo na
daktari huyo anachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
zilizopo ikiwamo kufikishwa mbele ya baraza la maadili.
Dk. Gwajima amesema anazo taarifa zote muhimu kuhusu daktari huyo ambazo amezipata kutoka kwa mgonjwa aliyemuhudumia.
Waziri huyo amesema tukio hilo limefanyika Novemba 30, mwaka huu hospitalini hapo na mgonjwa huyo amemueleza hayo na kumpatia ‘chart’ (mtiririko wa
mawasiliano) kati yake na daktari huyo ambazo zilifanyika kwa njia ya mtandao
wa ‘watsup’.
“Nilitoa mawasiliano yangu,
wananchi wananifikishia malalamiko mengi kuhusu Amana, huyo daktari akijua
kwamba amefanya kosa, mgonjwa alilazimika kwenda kupanga chumba nje ya
hospitali, akatafuta muuguzi mwenyewe ambaye alimuhudumia kidonda chake hadi
kilipofunga, alimkodia hadi teksi ya kumpeleka huko aendako.
“Kidonda kilipofunga, mgonjwa
alirudi kudai risiti lakini hakupatiwa hadi leo, jinsi walivyowasiliana kwa
njia ya watsup, amenitumia kila kitu, huyu lazima apatikane, andike maelezo na
achukuliwe hatua hadi baraza la maadili,” ameagiza.
Waziri Gwajima amesema wakati
umefika kwa watumishi kubadilika, kuwajibika na kufanya kazi zao kwa weledi na
kuzingatia miiko na maadili yao.
“Nimetoa muda wa siku 90 kuanzia
sasa, kila kiongozi katika kila eneo alilopo kuhakikisha anajua wajibu wake,
zitakapotimia nitajua cha kufanya, ‘tutawachekecha’,” amesisitiza.
Chapisha Maoni