Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Waziri Gwajima akikagua madokezo yaliyoandikwa na kitengo cha macho kwa ajili ya kuomba fedha kwaajili ya matengenezo ya kifaa cha kutengeneza miwani katika Hospitali ya Mwananyamala.

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Mashine ya kuchonga miwani iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini hapa haijatumika kwa takriban miaka mitatu, baada ya kuharibika ‘switch’ ambayo thamani yake ya matengenezo imebainishwa ni kiasi cha Sh. 18,000.

Endapo ‘switch’ hiyo ingenunuliwa na kufungwa katika mashine hiyo, wataalamu wa idara ya macho wa Mwananyamala wangeweza kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wenye uhitaji.

Lakini kwa kuwa kifaa hicho hakijatengenezwa wale wanaokutwa na matatizo yanayohitaji tiba ya miwani huagizwa kwenda hospitali nyinginezo, ingawa yenyewe ina wataalamu wajuzi na wabobezi katika utengenezaji wa miwani.

Yamebainika hayo leo hospitalini hapo wakati wa ziara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima alipotembelea kuangalia namna wanavyotoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza mbele ya Dk. Gwajima, Mtaalamu wa magonjwa ya macho wa Mwananyamala (Optometrist), Dk. Willium Desdery amesema kwa siku huwa wanaona wagonjwa 20 katika kitengo hicho na kwamba wengi huhitaji huduma ya miwani.

Dk. Desdery amemueleza Waziri Gwajima kwamba sambamba na fedha hiyo tangu mwaka 2017, 2018 na 2019 waliandika dokezi kwa uongozi (akionesha vielelezo), waliomba pia kiasi cha Sh. milioni moja kwa ajili ya kuanza uendeshaji wa huduma fedha ambazo hawakuwahi kupatiwa.

“Imeharibika muda mrefu, binafsi nimehamishiwa hapa Mwananyamala tangu 2013, nina uwezo wa kuchonga miwani, tulipewa mashine hii kipindi hicho nilipohamia hapa, iliharibika na haijatengenezwa mpaka sasa.

“Tukipata wagonjwa wanaohitaji kuchongewa miwani inabidi tuwaelekeze kwenda kwengineko kupata huduma, hatujawahi kupatiwa hizo fedha za matengenezo na ununuzi wa vifaa ili tuanze uzalishaji wa miwani hapa hapa hospitalini,” amebainisha.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Gwajima alimuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa Wizara hiyo, Dk. Grace Maghembe kuhakikisha anampa ‘promotion’ mtumishi huyo na kusitisha ‘promotion’ zote alizotakiwa kupatiwa kiongozi wa hospitali hiyo (Medical Officer).

“Nataka pia ndani ya siku 10 aandike barua kujieleza, amepokea madokezo hayo mara ngapi na kwanini hakutoa fedha hizo ili kuwezesha kitengo hiki kifanye kazi wakati watumishi hawa tunawalipa mishahara,” amesisitiza.

Vile vile, Waziri huyo ametembelea kitengo cha afya ya kinywa na meno na kukuta kiti kimoja cha kuhudumia wagonjwa wakati wa kutoa tiba kikiwa kimeharibika.

Daktari wa kitengo hicho, Balbina Beda amemueleza Waziri Gwajima kwamba katika idara hiyo wana viti viwili na hicho kimoja kimeharibika kwa zaidi ya miaka 10, hali iliyomshangaza.

Hivyo, ameagiza pia kufanyika ukaguzi wa kina wa mapato na matumizi ya hospitali hiyo ya mwaka mzima wa 2020 na ripoti hiyo afikishiwe ofisini kwake ifikapo Januari 30, 2021.

“Haiwezekani fedha za serikali zinatumika kuimarisha vitengo gani sasa ikiwa hapa tu mashine mmeshindwa kununua kifaa hicho cha Sh. 18,000 kwa miaka mitatu, mashine haifanyi kazi, huu ni uhujumu uchumi.

“Hali hii hapana, maofisa utumishi na wakaguzi wa ndani mnafanya kazi gani?... nchi hii haiwezi kwenda namna hii,” amesisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement