Na Veronica Mrema – Dodoma
Walimu wakuu wa shule zote nchini wameagizwa kushirikiana
na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukagua miundombinu ya umeme mashuleni,
ili kuepusha matukio ya moto ambayo hivi karibuni yameripotiwa maeneo
mbalimbali nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako ametoa agizo hilo leo alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu
wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) uliofanyika jijini hapa kwa siku tatu
(Desemba 20 hadi 22, mwaka huu).
“Hivi karibuni yameripotiwa matukio ya shule kuungua moto,
imarisheni ulinzi na usalama wa shule, shirikianeni na TANESCO), kukagua
miundombinu ya shule kama ipo salama au la,” ameagiza.
Waziri Ndalichako aliwaagiza walimu wakuu hao kuhakikisha
pia wanasimamia nidhamu za walimu wanaowasimamia shuleni ikiwamo katika suala
la mavazi, wavae yenye staha.
“Nyie nikiwaangalia mmependeza kweli kweli, nendeni
mkawasimamie na walimu wenu vizuri, wavae mavazi yenye staha na wale
wasiozingatia wachukuliwe hatua za kinidhamu, vivyo hivyo kwa wanafunzi,”
ameagiza.
Naye, Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, David Silinde, amesema tayari mwongozo wa usimamizi wa
nidhamu kwa walimu umeshaandaliwa, utasambazwa wakati wowote kuanzia sasa kwa
ajili ya utekezaji.
“Naamini mwongozo huu utakapotoka, utasaidia kufanikisha
usimamizi wa nidhamu kwa walimu, kwa sababu tumeshawafukuza na hata kuwashusha
vyeo lakini bado kuna changamoto, mwongozo tunaotarajia kuutoa utasaidia
kukabili changamoto hii,” amesema.
Chapisha Maoni