Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Ni nafuu kubwa kuepuka visababishi vinavyoweza kuchangia mtu kupata magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kwa sababu vingi vipo ndani ya uwezo wake. 

Baadhi ya visababishi vinavyotajwa na wataalamu wa afya kuchangia uwezekano mkubwa kwa watu wengi kuugua ni mtindo mbovu wa maisha hasa ulaji usiofaa, ikiwamo vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi na sukari nyingi.

Visababishi vingine ni unywaji wa pombe, matumizi ya bidhaa zitokanazo na zao la tumbaku hususan sigara na kutokufanya mazoezi, ingawa wapo wengine ambao huweza kuugua kwa kurithi vinasaba kutoka kwenye koo zao.

Gharama za kutibu magonjwa hayo mtu anapougua ni kubwa na mzigo kwa muhusika, familia yake, jamii na Taifa kwa ujumla, vile vile yanatajwa kuchangia idadi kubwa ya vifo vinavyotokea duniani kila mwaka.

‘Chukua’ mfano wa mgonjwa mmoja mwenye ugonjwa sugu wa figo nchini Tanzania, anayehitaji kufanyiwa huduma ya uchujaji damu (kitaalamu dialysis), anapaswa kuhudhuria kliniki mara tatu kwa wiki.

Kwa mujibu wa wataalamu wa magonjwa ya figo, utaratibu huo, mgonjwa husika atapaswa kuufuata maisha yake yote hadi pale atakapopata mtu wa kumchangia figo ili apandikizwe.

Dk. Tatizo Waane ni Mwenyekiti Mstaafu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG, anasema kila siku atakayohudhuria kliniki mgonjwa huyo atahitaji kuwa na kiasi cha kati ya Sh. 200,000 hadi Sh. 300,000 kwa kila ‘section’ moja ya ‘dialysis’.

“Hii inamaanisha kwamba kwa wiki atahitaji kuwa na kati ya Sh. 600,000 hadi Sh. 900,000, kwa mwezi atahitaji kuwa na kati ya Sh. Milioni 2.4 hadi Sh. Milioni 3.6 na mwaka atahitaji kuwa na kati ya Sh. Milioni 28.8 hadi Sh. Milioni 43.2.

“Gharama hizi bado hazijajumuisha gharama za usafiri, malazi, chakula na nyinginezo,” anasema Dk. Waane ambaye pia ni Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

HOJA NZITO 

Gharama za matibabu kwa magonjwa sugu ni miongoni mwa mada zinazoibua mijadala mikubwa zinapojadiliwa Tanzania, hii ni kwa sababu ni jambo linalogusa maisha ya Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Magonjwa hayo ni pamoja na moyo, kisukari, figo, saratani, shinikizo la damu, kiharusi, ajali, magonjwa yanayoshambulia mfumo wa njia ya hewa na mengine mengi yaliyo katika kundi hilo.

Ni magonjwa ambayo miaka mingi iliyopita (enzi za mababu na mabibi), Tanzania yalionekana kuwakumba zaidi watu waliokuwa na umri mkubwa, enzi hizo yaliitwa magonjwa ya wazee ama ya watu wazima.

Lakini tofauti kubwa ni kwamba, miaka ya hivi karibuni, yanaonekana kuwakumba zaidi kundi la watoto na vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa inayotegemewa kujenga uchumi.

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha magonjwa hayo yanachangia takriban asilimia 33 hadi 35 ya vifo vyote vinavyotokea Tanzania.

“Magonjwa haya yanaongezeka kwa kasi kubwa nchini, kwa takriban miaka minane sasa hali inaonesha yanatesa zaidi kundi la vijana na watoto ikilinganishwa hapo kabla ambapo kundi la watu wazima (wazee) ndilo lililokuwa likiugua,” anabainisha Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa Wizara hiyo, Dk. Grace Maghembe.

JANGA LA DUNIA

Magonjwa yasiyoambukiza ni janga linaloitesa dunia hivi sasa si tu Tanzania pekee, kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2018, yalichangia vifo vipatavyo milioni 41.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linaeleza idadi hiyo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2018.

Taarifa za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP), zinaonesha pamoja na changamoto za kiafya, magonjwa hayo yaathiri nyanja nyingine za maisha na jamii kwa ujumla.

Inakadiriwa kufikia mwaka 2033 gharama zitokanazo na huduma za magonjwa hayo zitafikia Dola za Marekani Trilioni 47 fedha ambazo zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu Bilioni 2.5 kwa miaka 50 duniani.

Kwa nchi za uchumi wa kati (Tanzania ikiwamo) na zile nchi za uchumi wa chini magonjwa hayo yatagharimu mataifa hayo jumla ya Dola za Marekani Trilioni saba kwenye kipindi cha mwaka 2011 hadi 2025.

Gharama hizo zinatokana na huduma za matibabu na nguvu kazi inayopotea (loss productivity) kutokana na magonjwa hayo.

Makadirio yanaonesha gharama za huduma za magonjwa yasiyoambukiza itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya afya duniani.

Ugonjwa wa kisukari pekee ukipelekea gharama zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya afya duniani.

Dunia ikikadiria hayo, Dk. Grace anabainisha kwamba takwimu za Wizara ya Afya, Tanzania zinaonesha magonjwa sugu yanagharimu takriban asilimia 40 ya bajeti ya afya kila mwaka, huku kukiwa pia na kundi kubwa la wagonjwa wanaotibiwa kwa msamaha.

‘CHOZI’ LA MIFUKO

Ni wazi kwamba gharama za kutibu magonjwa hayo zinaonekana kuielemea bajeti ya Wizara hiyo, takwimu zake zinaonesha bado kuna idadi ndogo ya Watanzania waliojiunga na mifuko ya bima za afya.

Kwa mfano, katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ni mkubwa nchini Tanzania, takwimu zinaonesha ni asilimia 4.4 tu waliojiunga kati ya zaidi ya Watanzania milioni 60 waliopo.

Hali hiyo inatajwa kuwa kikwazo katika kuboresha na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wake, hivi sasa ikijikita kuhamasisha wengi kujiunga na mifuko ya bima ya afya.

Rais Mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati anasema pamoja na bima ya afya, ni wazi kwamba Serikali sasa inahitaji pia kutafuta mbinu mbadala kusaidia wananchi wake na uchumi wake katika kukabiliana na magonjwa sugu.

“Inaweza kuanzisha Mfuko wa Afya na huu uelekezwe katika kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza, inawezekana kuiga mfano ilivyo kwa upande wa huduma za umeme nchini, kabla ya kuanzishwa EWURA (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji), kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu tarrifs.

“Lakini sasa hayapo, si kwamba zile gharama zilizokuwa zinalalamikiwa zimeondolewa bali wananchi wanalipia moja kwa moja pindi wanaponunua umeme na sasa malalamiko hakuna tena.

“Uanzishwe mfuko kwa upande wa afya, ili kwa mfano, kwa bidhaa zile zinazotajwa kuchangia magonjwa haya ziwe zinatozwa kiasi fulani cha fedha kirudi kwenye kugharamia matibabu ya wananchi,” anashauri Dk. Osati.

SERA MPYA YA AFYA

“Kimsingi gharama za kutibu magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa na wanaobeba mzigo mkubwa ni wagonjwa wenyewe, familia zao na Serikali,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Tumaini Eli.

Anaongeza “Magonjwa haya mengi ni ‘life time’, yaani mtu akikutwa nayo kwa mfano kisukari, shinikizo la damu ataendelea kuishi nao maisha yake yote.

“Kwa kweli, bei za dawa gharama zake zipo juu, ndiyo maana Serikali hivi sasa inatafuta mbadala ambao utaweza kuwagharamia huduma wale ambao hawana uwezo,” anasema.

Anasema bima ya afya itasaidia kwa kiasi kikubwa wale wasio na uwezo na kwamba kwa wale wenye uwezo kidogo nao watamudu kuchangia huduma.

“Wengi tukiwa na bima tukichangia huduma, kapu letu litakuwa na fedha, naweza nisiugue mimi au wewe (mwandishi) lakini shangazi akiugua, kile kidogo tulichochanga sisi kwenye mfuko kitasaidia matibabu yake,” anasisitiza.

Anaongeza “Ni kama vile magari yetu tunayakatia bima lakini si yote yanayopata ajali, ajali inapotokea zile fedha zetu tulizotoa, zilizokusanywa, zinamsaidia yule ambaye alipata ajali.

“Ndiyo mfumo ambao tumeufukiria kwa kina katika kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa upande wa NCDs, kwa mfano upande wa ajali Serikali huwa inagharamia zile ‘implants’ (vifaa tiba, vipandiziki ambavyo huwekea waliovunjika kwenye ajali).

“Lakini majeruhi wengi hushindwa kugharamia zile gharama hivyo pale MOI (Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), tumeanzisha ‘Implant Fund’ ambapo Serikali inawapa fedha wananunua vile vifaa, halafu tunaanza kutafuta wale wagonjwa wanaopata ajali, tunazungumza na zile kampuni za bima ili … kwa mfano mimi nikipata ajali, kile chombo kilichokatiwa bima kile kiasi ambacho kimetengwa kwa ajili ya kulipia bima matibabu lazima kirudi kwenye lile kapu la ‘Implant’.

“Hivi sasa bado tupo kwenye mazungumzo ya ndani kiasi gani kitakwenda huko. Kwa upande wa dawa nako Serikali inatoa fedha kupitia NHIF, inalipa vituo vya afya, tunataka tutengeneze mfuko wa dawa, malipo yote yanayofanyika kwa dawa, zile fedha zinazotolewa na serikali, zirudi katika ule mfuko.

“Serikali imejitahidi kutoa fedha za dawa, kwanza ilitoa Sh. Bilioni 270, awamu ya pili ilitoa Sh. Bilioni 269 na ilitoa tena Sh. Bilioni 270 fedha za dawa ukiziweka kwenye kapu moja maana yake ni kwamba kile kituo ambacho mtu atahudumiwa, kikitoa zile dawa NHIF inalipa fedha zikitolewa zinatengeneza mfuko ndani ya kile kituo,” anabainisha.

Tumaini anaongeza “Hili si kapu la nchi nzima, ni kama kibubu cha dawa kwa kila kituo, kwamba wameuza na kuweka humo, ili zile fedha zisije zikatumika kwenye matumizi mengine, kuwe na ‘sustainability’ ya fedha za dawa.

KUHUSU MISAMAHA

“Tumeanza hivyo wakati serikali inakamilisha mchakato wa bima moja, kuhusu msamaha wa matibabu Sera ya Afya ya mwaka 2007 imetamkwa vizuri kabisa, kwamba akina mama wajawazito ambao hawana uwezo, watoto chini ya miaka mitano, wazee juu ya miaka 60 ambao hawana uwezo, ndiyo wanaostahili kupewa msamaha.

“Lakini tatizo ni kwamba haijafahamika vizuri kwenye jamii, chukua mfano kwangu, mimi ni mtumishi wa umma lakini je, mke wangu akiwa mjamzito au mwanangu akiugua atakwenda kupanga foleni kwa sababu Sera inaeleza wanapaswa kuhudumiwa kwa msamaha ingawa nimewkaatia bima ya afya?.

“Ni wazi haijaeleweka vizuri, lakini katika Sera mpya ya Afya ya 2020/21, eneo la msamaha halitatolewa ila litafafanuliwa vizuri zaidi, ni nani na nani wanaostahili kupewa huduma kwa msamaha,” anafafanua.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement