Walimu wakuu shule za sekondari wakiwa kwenye mkutano mkuu wa 15 wa TAHOSSA.
Na Veronica Mrema – Dodoma
Serikali imejipanga kufanya msako wa uhakiki wa vibali vya
walimu wa kigeni nchi nzima ikisisitiza waajiri (wamiliki) wa shule hasa za
binafsi kuzingatia kanuni na sheria za nchi katika kuajiri.
Yameelezwa hayo leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa 15 wa
Wakuu wa Shule za Sekondari uliofanyika jijini hapa kwa siku tatu (Desemba 20
hadi 22, mwaka huu).
Waziri Ndalichako amesisitiza katika jambo hilo Serikali
haina mzaha na kwamba tayari ina taarifa muhimu watakazoanza nazo wakati wa
msako huo.
“Nawasihi waajiri (wamiliki) hasa wa shule binafsi
kuzingatia miongozo ya Serikali katika kuajiri, tunazo taarifa za awali kwa
sababu tumefanya tathmini baadhi yenu mnakiuka.
“Shule binafsi baadhi zinakiuka, Sheria za nchi kwa
kuchukua walimu nje ya nchi na wanajua wazi kufanya kazi nchini bila kibali ni
makosa,” amesema.
Ameongeza “Tunajua hivyo vichaka, anzeni kuchoma moto
vichaka vyenu wenyewe, tunakuja kufanya tathmini ya kina, nawasihi walimu wakuu
wa shule za binafsi za sekondari, anzeni kutoa taarifa kwa wamiliki wenu,
tunakuja.
“Msipotoa taarifa mapema, kwa sababu mnajua… tukija huko
kukagua mtaipata,” amesisitiza.
Pamoja na hilo, Prof. Ndalichako ameagiza mazingira ya
shule zote nchini kuwekwa katika hali ya usafi kwani katika baadhi ya shule
alizotembelea amekuta ni machafu huku madarasa yakiwa yamejaa buibui.
Awali, Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia masuala ya Elimu, David
Silinde, ameagiza wakuu wa shule na wakurugenzi wote nchini kuhakikisha
wanakamilisha ujenzi wa madarasa kufikia Februari 28, mwaka huu.
“Ili wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza,
waanze masomo yao,” amesisitiza.
Chapisha Maoni