Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Watu wenye kundi la damu O+ (Rhesus factor ‘Rh+’) waliongoza idadi ya wachangia damu kwa asilimia 51 kati ya wachangia damu 309,376 mwaka 2019 ikilinganishwa na makundi mengine.

Makundi yaliyochangia kwa kiwango kidogo cha wastani wa chini ya asilimia moja pekee ni yale yenye ‘rhesus factor negative’, yaani A-, B-, AB- na O-, imebainishwa .

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Tanzania (NBTS), Dk. Magdalena Liymo amebainisha hayo hivi karibuni katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG, saa kadhaa baada ya kuwasilisha mada kuhusu maendeleo ya NBTS katika ukusanyaji damu salama, wakati wa kongamano la kisayansi lililofanyika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

“Makundi ya damu yenye ‘Rhesus Factor Negative (Rh-), hawa ni makundi adimu si tu Tanzania bali duniani, wapo wachache mno, ndiyo maana sasa hivi tunawaweka kwenye kanzi data zetu.

“Ili tuwafahamu na kuendelea kuwahimiza kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wahitaji wa makundi haya pale inapotokea,” amebainisha.

Amesema hakuna kiwanda cha damu duniani isipokuwa damu hupatikana kutoka kwa binadamu mwenyewe, ndiyo maana jamii inahimizwa kuchangia.

Dk. Magdalena ameongeza “Kila nchi ili itosheleze mahitaji yake inahitaji kukusanya damu kiasi cha asilimia moja ya idadi ya watu wake, kulingana na tathmini ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Kwa makadirio ya Watanzania zaidi ya milioni 50 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hivyo Tanzania inahitaji kukusanya chupa za damu salama zipatazo 550,000 kutosheleza mahitaji yake.

“Hata hivyo hatujawahi kufikia kiwango hicho, ingawa tumedhamiria kukifikia, kwa mwaka 2015/16 tulikusanya chupa za damu 196,000, mwaka 2016/17 chupa za damu 233,000, mwaka 2018/19 chupa za damu 309,376,” amebainisha.

Amesema damu zote zinazokusanywa nchini huchunguzwa usalama na ubora wake kabla ya mgonjwa kuongezewa.

“Tunazifanyia uchunguzi wa kimaabara iwapo zina maambukizi ya Homa ya Ini B na C, Virusi Vya Ukimwi na kaswende, zile zitakazokuwa salama ndizo zinazotumika na zile ambazo si salama zinaharibiwa,” amesema.

Amefafanua “Kwa mfano, tunachukua nusu lita ya damu kutoka kwa mchangiaji (sawa na mils 450), ikiwa kiasi hicho cha ujazo hakikufika au kimezidi, au kukawa na matatizo kwenye uhifadhi, na kasoro nyinginezo zitakazobainika, damu hiyo inaondoshwa, haitatumika.

“Tunahakikisha, damu tangu imechukuliwa kwa mchangiaji, imepita kwenye hatua zote za uchunguzi wa usalama na ubora wake hadi inamfikia mgonjwa inakuwa imekidhi vigezo vyote,” amesema.

Meneja huyo wa NBTS ameongeza “Mwaka 2019 asilimia 15 ya damu iliyokusanywa iliharibiwa ambapo asilimia 13 ilibainika kuwa na maambukizi ya magonjwa na asilimia mbili haikufikia vigezo vinginevyo vya ubora na usalama.

“Kimsingi tunataka kuwahakikishia watu damu inayotumika imekidhi vigezo vyote vya ubora na usalama,” amesisitiza.

Amesema katika utoaji wa huduma baadhi ya makundi ya watu kwenye jamii hupewa kipaumbele kuhakikisha yanapohitaji damu salama yanahudumiwa ikiwamo lile la wagonjwa wa siko seli, saratani, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Dk. Magdalena amesema NBTS huzalisha mazao ya damu ambapo kwa kila chupa moja (unit) huweza kuzalisha mazao matatu na hivyo kuokoa uhai wa wagonjwa watatu wenye uhitaji kwa wakati mmoja.

“Tunazalisha plasma, chembe sahani na chembe nyekundu, lakini ikiwa tunabaini damu haikuwa salama hata yale mazao yake hatuwezi kuyatumia kwani si salama, hivyo tunayaharibu,” amebainisha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement