Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kampeni ya uchunguzi wa awali saratani ya kizazi iliyoenda sambamba na uchunguzi wa saratani ya tezidume, wakisikiliza kwa makini wakati Mtaalamu Mbobezi Masuala ya Afya ya Jamii kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Johnson Katanga, alipokuwa akizungumza. 

Na Veronica Mrema – Tanga

Ipi tofauti kati ya busha na saratani ya tezidume? Ni swali lililoibuka mapema leo, limeulizwa na Mkazi wa Tanga Mjini, Kaggy Karigo, ambaye alikuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo.

Karigo aliuliza swali hilo baada ya kupewa nafasi na Mtaalamu Mbobezi Masuala ya Afya Jamii wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Johnson Katanga, wakati wa kipindi kifupi cha elimu kwa umma kuhusu magonjwa ya saratani.

Wataalamu wa ORCI wamepiga kambi hospitali hapo tangu juzi (Januari 28, 2021) ambayo inahitimika leo (Januari 30, 2021), ikiwa ni maalum kwa kampeni ya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake.

Kampeni hiyo imeenda sambamba na mafunzo kwa watoa huduma za afya zaidi ya 25 kutoka hospitali mbalimbali ndani ya Mkoa wa Tanga, pamoja na uchunguzi wa saratani ya matiti pia saratani ya tezidume.

“Nataka kujua ipi tofauti kati ya busha na saratani ya tezidume,” aliuliza Karigo alipokaribishwa kuuliza swali.

Akijibu swali hilo, Dk. Katanga alianza kwa kufafanua maana ya tezidume kwamba hiki ni kiungo muhimu katika mfumo uzazi wa mwanaume ambacho kila mwanaume ameumbwa nacho.

Amesema tezidume huwa na kawaida ya kukua na kuongezeka ukubwa wake kadri umri wa mwanaume unapoongezeka na mabadiliko hayo ni ya kawaida.

“Ni kama vile mwili wa binadamu kawaida uzeeka na ngozi kujikunja, vivyo hivyo kwa tezidume, yenyewe kawaida huwa inaongezeka ukubwa umri wa mwanaume unapoongezeka.

“Wakati inapoongezeka kwa kuwa ipo karibu na mfumo wa haja ndogo wa mwanaume, huweza kutokea ikabana ile njia na hivyo mwanaume kujikuta akipata shida anapokuwa akikojoa, hupata mkojo kidogo, huhisi maumivu.

Ameongeza “Lakini ukuaji ule unaweza kuwa si wa kawaida (saratani), sasa kwa kuwa dalili zinafanana na ukuaji wa kawaida, ili tuweze kujua lazima tufanye uchunguzi wa awali, tunatumia kipimo cha damu, ni kama kile kinachotumika kuchunguza malaria.

“Tunapopima kwa njia ya damu kuna vichocheo ambavyo huwa tunavichunguza, vinapokuwa vingine kwenye damu hapo ndiyo tunajua mtu huyo anahitaji uchunguzi zaidi, tezidume ipo ndani ya mwili wa mwanaume” amesisitiza.

Amesema kwa upande wa busha yenyewe ni maji ambayo hukusanyika kwenye pumbu (kende), kiungo cha mwanaume ambacho kipo nje ya mwili wake, karibu na uume.

Ameongeza “Kwa hiyo hivi ni viunge viwili tofauti katika mwili wa mwanaume ingawa vyote vipo katika mfumo wake wa uzazi, tiba dhidi ya busha ni upasuaji ambapo wataalamu humfanyia mgonjwa na kuondoa yale maji yaliyojaa mule kwenye kende.

Ofisa Muuguzi wa ORCI, Bahati Msofe (anayezungumza mbele ya wananchi), amewapongeza wananchi waliojitokeza katika uchunguzi huo wa awali.

“Unapofanyiwa uchunguzi mapema kama tayari zile seli zimeanza kuleta mabadiliko ni rahisi kugundulika mapema na kufanyiwa matibabu mapema, lakini inapochelewa kugundulika ni vigumu kupona,” amebainisha.

Amehimiza wananchi hao kuendelea na utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara hata kwa magonjwa mengineyo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement