Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Janga la CORONA bado linaitesa dunia, ingawaje yapo
matumaini ya kupatikana kwa chanjo, nchi mbalimbali zikiwa tayari zimeanza
kutoa kwa raia wake na kueleza ni hatua ya mafanikio.
Hata hivyo, kubainika kwa aina mpya ya virusi katika
mataifa kadhaa ikiwamo Marekani na Nigeria ni suala linaloibua hofu kwa
binadamu, likiangaziwa kwa ukaribu zaidi hivi sasa.
Mwanzoni mwa Desemba, 2020, Kituo cha
Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) kilinukuliwa kikieleza
idadi ya jumla ya maambukizi yaliyothibitishwa ya virusi vya Corona barani humu
imekaribia milioni 2.25, huku idadi ya vifo ikifikia 53,543 na wengine wapatao
milioni 1.9 wameugua na kupona Afrika.
Kwa mujibu wa Africa CDC, nchi zilizoathiriwa
vibaya zaidi na virusi hivyo barani humo ni Afrika Kusini, Morocco, Misri na
Ethiopia, huku Kenya nayo
ikishuhudia ongezeko la maambukizi miongoni mwa raia wake katika siku za hivi karibuni.
Eneo la kusini mwa Afrika linatajwa kuwa lenye kiwango cha juu
zaidi cha maambukizi ya COVID-19 na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo huku eneo
la kaskazini mwa Afrika likiwa la pili.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lenyewe limewatoa wasiwasi
wanadamu hasa juu ya aina mpya ya virusi hivyo iliyoripotiwa kwenye mataifa
kadhaa.
WHO linasisitiza pia chanjo hizo zilizotengenezwa kupambana
na COVID - 19 zina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya virusi hivyo, lakini uchunguzi
zaidi unaendelea.
NI
MWAKA MMOJA
Kufikia Desemba, 2020 dunia ilitimiza mwaka mmoja tangu Desemba,
2019, iliposhuhudia mlipuko wa ugonjwa huo huko Wuhan, China.
Awali haukujulikana ulikuwa ugonjwa gani na ulisababishwa
na aina gani ya virusi hadi pale wataalamu walipofanya uchunguzi wa kina wa
kimaabara.
Hatimaye ilibainika chanzo chake ni maambukizi ya virusi vya
Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu, ukapewa jina COVID –
19.
Mithili ya moto uteketezao nyika, ulianza kuenea kwa kasi kwengineko
duniani, wengi wakaambukizwa virusi hivyo na wengine kupoteza maisha hasa wazee
na watu wanaokabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza (sugu).
Takwimu za WHO zinaeleza tangu Desemba, 2019 hadi Januari
3, 2021 jumla ya wagonjwa milioni 83.32, vifo milioni 1.8 vimeripotiwa.
Hivi sasa nchi mbalimbali zimeendelea kuchukua hatua
ikiwamo kuweka sharti la upimaji ya maambukizi hayo kwa wasafiri wanaotoka nchi
moja kwenda nyingine, Tanzania ikiwamo.
TANZANIA
Machi 16, 2019 Tanzania iliripoti kisa cha kwanza cha
mwanamke mmoja mwenye raia wa Tanzania, alithibitika kuambukizwa virusi hivyo na
kuugua, aliwasili nchini akitokea Ubelgiji kwa ndege ya Shirika la Rwanda.
Kulingana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) idadi
ya visa iliongezeka kutoka kimoja hadi kufikia 480, April, 2020 huku vifo 18
vikiripotiwa kutokana na ugonjwa huo.
Serikali ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali kuukabili
ili kuhakikisha inalinda wananchi wake dhidi ya janga hilo na mara kadhaa
imenukuliwa ikisisitiza hivi sasa hakuna kisa chochote cha Corona.
Miongozo ya kitaalamu ilitolewa kwa umma kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikielekeza jinsi ya kuepuka
maambukizi ya ugonjwa huo usio na tiba hadi sasa duniani.
Hatua hizo ni pamoja na kukaa umbali wa mita moja hadi
mbili kati ya mtu na mtu hasa anayekohoa na mwenye historia ya kusafiri kutoka
nje ya nchi, kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na
kutumia vitakasa mikono.
Mikusanyiko ya watu nayo ilizuiliwa kwa muda, kwa mfano shule na vyuo vyote nchini vilifungwa, kwa lengo la kuepusha uwezekano wa kusambaa zaidi kwa maambukizi hayo.
TAFITI
ZA DUNIA
“Ni changamoto ya dunia nzima, mlipuko wa Corona uliibua
hofu kwamba huenda inaenezwa kwa njia ya kuongezewa damu.
“Lakini tafiti mbalimbali zilipofanyika zilionesha haiambukizwi
kwa njia ya kuongezewa damu,” anasema Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama
Tanzania (NBTS), Dk. Magdalena Liymo (pichani) katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG hivi karibuni.
Dk. Liymo anaongeza “Hivyo wagonjwa waliopatiwa huduma ya
kuongezewa damu maana yake ni kwamba hakukuwa na maambukizi ya Corona kwa njia
hiyo.
“Kwa kuwa haienezwi kwa njia ya damu, lakini pia
mikusanyiko ilizuiliwa, NBTS tulifanya maboresho ya mazingira ya uchangiaji
damu kwenye vituo vyetu kwa kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya, ili
kuwalinda wananchi na watoa huduma wetu.
“Tulihamasisha jamii kujitolea damu kwa hiyari, tukaweka
vitanda vyetu kwa kuzingatia umbali wa mita moja, vitakasa mikono, maji safi
tiririka na sabuni, tukahimiza uvaaji wa barakoa na hatua zote muhimu ili
kuepusha maambukizi ya ugonjwa huo.
“Jamii ilihamasika, watu walijitokeza kuchangia damu kwa
hiyari, tulipata upungufu kiasi cha asilimia kati ya tano hadi 20 ya makusanyo
ya damu kulinganisha na kipindi ambacho hakukuwa na ugonjwa,” anabainisha.
RIPOTI
ZA NBTS
Kwa mujibu wa NBTS zaidi ya asilimia 80 ya wachangia damu
ni wanafunzi na wana - vyuo. Kutokana na marufuku ya mikusanyiko ya watu ikiwa
ni hatua ya kukabiliana na Corona, ililazimika kuchukua hatua mbadala kukusanya
damu salama ili kuendelea kuhudumia jamii pale ilipohitajika.
Takwimu za NBTS zinaonesha katika kipindi hicho makusanyo
ya damu salama yalishuka ambapo kipindi cha kuanzia April, 2019 yalikuwa chupa za
damu 22,044 ikilinganishwa na chupa za damu 25,737 kipindi cha Machi, 2019
(ugonjwa ulipothibitishwa) na chupa za damu 31,502 kipindi cha Februari, 2019
kabla ya ugonjwa kuingia nchini.
Ripoti za NBTS zinaeleza kushuka huko kwa makusanyo
kulichangiwa na kufungwa kwa shule na vyuo, kukosa fursa ya kukusanya damu katika
ofisi mbalimbali pamoja na zuio la mikusanyiko ikiwa ni hatua ya kukabiliana na
ugonjwa huo kuzuia usienee.
Hata hivyo, hatua zilizochukuliwa kipindi cha mwezi Juni,
2020 ‘kilizaa matunda’ ambapo Tanzania, mapinduzi yalishuhudiwa kwenye kampeni
ya ukusanyaji damu kitaifa, ambayo ilifanyika kuelekea kilele cha siku ya
wachangia damu duniani.
Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa wa
wadau wa vyombo vya habari kwenye kutoa elimu kwa jamii ambayo ilisaidia kuwaondolea
hofu wananchi na kujitokeza kuchangia damu.
Kipindi hicho Tanzania ilikuwa katikati ya mapambano dhidi
ya Corona, ambapo kampeni hiyo ililenga kukusanya chupa za damu 24,800 na
makusanyo yalikuwa chupa 18,075 sawa na asilimia 79.3.
Takwimu za NBTS zinaeleza
katika kampeni hiyo ambayo wananchi walijitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa
hiyari, timu za halmashauri walikusanya jumla ya chupa za damu 14,841 sawa na
asilimia 67.5 na timu za Kanda 3234 sawa na asilimia 116.
RIPOTI
ZA WHO
Kila nchi ili itosheleze mahitaji yake inahitaji kukusanya
damu kiasi cha asilimia moja ya idadi ya watu wake, kulingana na tathmini ya WHO.
Hivyo, kwa idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 50 kulingana
na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania inahitaji kukusanya chupa za damu salama
zipatazo 550,000 kutosheleza mahitaji yake.
“Lakini hatujawahi kufikia kiwango hicho, ingawa
tumedhamiria kukifikia, kwa mwaka 2015/16 tulikusanya chupa za damu 196,000,
mwaka 2016/17 chupa za damu 233,000, mwaka 2018/19 chupa za damu 309,376,”
anabainisha Dk. Liymo.
Anasema katika chupa za damu 309,376 kundi lililochangia
kwa kiwango kikubwa lilikuwa la O+ kwa kiwango cha asilimia 51 na kwamba kwa makundi
adimu ikiwamo A-, B-, AB- na O- hayo ukusanyaji wake ulikuwa chini ya asilimia
moja.
“Hawa wenye makundi adimu walikuwa wachache mno, ndiyo
maana sasa hivi tunawaweka kwenye kanzi data zetu, ili tuwafahamu na kuendelea
kuwahimiza kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wahitaji wa makundi
haya pale inapotokea,” anabainisha.
USALAMA
NA UBORA
Dk. Liymo anasema damu zote zinazokusanywa nchini
huchunguzwa usalama na ubora wake kabla ya mgonjwa kuongezewa.
“Tunazifanyia uchunguzi wa kimaabara iwapo zina maambukizi
ya Homa ya ini B na C, Virusi Vya Ukimwi na kaswende zile zitakazokuwa salama
ndizo zinazotumika na zile ambazo si salama zinaharibiwa,” anasema.
Anafafanua “Kwa mfano, tunachukua nusu lita ya damu kutoka
kwa mchangiaji (sawa na mils 450), ikiwa kiasi hicho cha ujazo hakikufika au kimezidi,
au kukawa na matatizo kwenye uhifadhi, na kasoro nyinginezo zitakazobainika,
damu hiyo inaondoshwa, haitatumika.
“Tunahakikisha, damu tangu imechukuliwa kwa mchangiaji,
imepita kwenye hatua zote za uchunguzi wa usalama na ubora wake hadi inamfikia
mgonjwa inakuwa imekidhi vigezo vyote,” anasema.
Meneja huyo wa NBTS anaongeza “Mwaka 2019 asilimia 15 ya
damu iliyokusanywa iliharibiwa ambapo asilimia 13 ilibainika kuwa na maambukizi
ya magonjwa na asilimia mbili haikufikia vigezo vinginevyo vya ubora na
usalama.
“Kimsingi tunataka kuwahakikishia watu damu inayotumika
imekidhi vigezo vyote vya ubora na usalama,” anasisitiza.
Anasema katika utoaji wa huduma baadhi ya makundi ya watu
kwenye jamii hupewa kipaumbele kuhakikisha yanapohitaji damu salama
yanahudumiwa ikiwamo lile la wagonjwa wa siko seli, saratani, wajawazito na
watoto chini ya miaka mitano.
UTENGENEZAJI
MAZAO
Dk. Magdalena anasema NBTS huzalisha mazao ya damu ambapo
kwa kila chupa moja (unit) huweza kuzalisha mazao matatu na hivyo kuokoa uhai
wa wagonjwa watatu wenye uhitaji kwa wakati mmoja.
“Tunazalisha plasma, chembe sahani na chembe nyekundu,
lakini ikiwa tunabaini damu haikuwa salama hata yale mazao yake hatuwezi
kuyatumia kwani si salama, hivyo tunayaharibu,” anabainisha.
Anabainisha “Kwa kuzalisha mazao ya damu tunaweza kuhudumia
wagonjwa watatu kwa kila chupa moja ya damu, kwa sababu tunapata mazao ya aina
tatu, mgonjwa wa saratani atahitaji chembe sahani ataongezewa, anayejifungua
atahitaji chembe nyekundu ataongezewa.
Swali linasalia, Je! Watanzania wamejifunza na kubadili mtizamo juu ya uchangiaji damu badala ya kusubiri kuhimizwa na kufuatwa kuchangia damu wajenge utamaduni wa kuchangia wenyewe kwa hiyari?
Chapisha Maoni