Na Veronica Mrema – Mwanza
Je! U miongoni mwa watu wanaobakiza dawa pindi wanapojihisi kupata
nafuu? Je! U miongoni mwa watu wanaotumia dawa holela kwa
kujinunulia wenyewe madukani (safe medication)? Na Je! U miongoni mwa watu
wanaotupa holela dawa zilizobaki nyumbani?
Ikiwa u miongoni mwao, basi unapaswa kubadilika mara moja,
kwa sababu hayo ni baadhi ya mambo yanayotajwa kuweka ‘rehani’ afya yako na jamii
kwa ujumla.
Kulingana na wataalamu wa afya aina yoyote ya dawa inayotumika
kutibu inapaswa mgonjwa kwanza ni lazima aandikiwe na daktari au apatiwe na mfamasia
tena baada ya kufanyiwa vipimo vya uchunguzi.
Aidha, dawa husika inapaswa kutumiwa na kumalizwa ndani ya
muda aliondikiwa ili kutibu ugonjwa unaomkabili.
Kimsingi, wanasisitiza dawa haipaswi kubakizwa hata ikiwa
mgonjwa husika anapata (anahisi) nafuu dhidi ya maradhi yanayomsumbua.
Mkazi wa Busweru Mkoani Mwanza, Eliud Bwire ni miongoni mwa waliohojiwa na MATUKIO NA MAISHA BLOG anasema yeye huwa hamalizi dozi, anapojihisi nafuu kwa sababu huamini kwamba tayari amepona ugonjwa unaosumbua, jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya wataalamu.
“Sasa nitumie ya nini, si nimepona, naacha, wakati mwingine natumia ninapojihisi kuumwa tena, ikiwa sitazitumia kwa muda mrefu kama ni vidonge nitavitupa kwenye shimo la taka kwa sababu naamini zitakuwa hazifai tena kwa matumizi. Nyumbani kwangu sina mtoto mdogo ndiyo maana sioni shaka kuzitupa shimoni, zitakaa humo hadi siku nitakapochoma taka.
“Kama ni dawa za majimaji hizo nazimwaga kwenye sinki, chupa nazitupa shimoni na wakati mwingine simwagi nazitupa humo humo, nitakuja kuchoma kwa pamoja,” anasema.
UHALISIA
WA MAMBO
“Kila dawa hutengenezwa na kiambata hai chake na kila kiambata hai kina muda wa kuishi ndani ya dawa husika,” anasisitiza Bugusu Nyamweru ni Kaimu Mkuu wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA – Kanda ya Ziwa).
Nyamweru anasisitiza mgonjwa anapomeza dawa husika kila kiambata hai kina muda wake kutoka mwilini kwenda kutibu ugonjwa husika.
“Mgonjwa anapoandikiwa dozi na daktari anapaswa kuimaliza kwani kiambata hai kina muda wa kuishi ‘expire’ ndani ya dawa husika.
“Kiambata hai kina muda wa ‘kuishi’ ndani ya dawa, ndiyo maana kuna ‘expire date’ (muda wa kuisha kwa matumizi), unapoisha wastani wa asilimia 10 ya kiambata hai hupungua na kubaki asilimia 90.
“Ile asilimia 90 inakuwa na uwezo wa kutibu lakini tunakuwa hatujui mule ndani ile asilimia 10 ambayo imepungua imebadilika kuwa nini, labda imekuwa sumu tayari, hivyo kile kinachoharibika kinaweza kuleta madhara,” anabainisha.
Nyamweru anaongeza “Ndiyo maana hata ‘syrup’ ikishafunguliwa, haitakiwi kubaki kwa sababu inaweza kuleta madhara, tunahimiza watu wazingatie matumizi ya dawa kama walivyoelekezwa na wataalamu.
MAJUMBANI!
Mkaguzi wa Dawa wa TMDA – Kanda ya Ziwa, Mtani Njegere anasema
kutupa dawa kwenye mazingira, sinki la maji inaleta athari kubwa kwa binadamu
na viumbe hai wengine na hata kusababisha tatizo la usugu wa vimelea vya
magonjwa dhidi ya dawa.
“Hatujawahi kufanya tafiti kujua kwa kiwango gani kwenye
familia zetu watu wanabakiza dawa na kuzitupa, kwa sababu imani yetu, kimsingi
dawa zinapaswa kutumika kama ilivyoelekezwa na daktari na kumaliza.
“Lakini kuna dawa zinabaki majumbani kwetu, mtu anaweza
kutumia kabla haijaisha anaiacha, ukienda baadhi ya familia unazikuta.
“Ni vema wananchi wanapokuwa na dawa hizo wawasiliane na
maeneo yanayotoa huduma za tiba au famasi, wazirudishe huko ili wao (famasi,
vituo vya kutolea huduma za tiba / afya) wawasiliane na sisi (TMDA) kwa ajili
ya uteketezaji.
“Kimsingi, dawa hata kama eneo halikai watu haifai
kuteketezwa kwenye eneo hilo kwa sababu inaweza kuteketeza hapo lakini ikachukuliwa
ama kwa mvua hadi kwenye maeneo ya makazi ya watu na kuleta madhara.
“Kwa mfano hapa Kanda ya Ziwa, inaweza kunyesha mvua,
mmeteketeza eneo la wazi, dawa ikachukuliwa hadi ziwani, matokeo yake mtu
anajikuta anakula samaki ambaye tayari ana madhara ya dawa.
“Kwa mfano ikiwa ni antibiotics, ziliteketezwa zikasafiri
hadi ziwani, samaki wakaathirika, hali ile siku za usoni inaweza kuleta madhara
kwa binadamu ikiwamo usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa,” anasema.
Anaongeza “Ndiyo maana tunahimiza jamii, dawa lazima itumike iishe, lakini ikiwa ilibakizwa isiteketezwe holela, pia wadau wetu wote wazingatie mwongozo wa utektezaji wa dawa ambao upo wazi ni ‘public document’ ipo pia kwenye webste yetu.
NI
JUKUMU KISHERIA
Mtani ambaye pia ni Mratibu Msimamizi wa Dawati la Udhibiti
wa Vifaa Tiba na Vitendanishi, TMDA – Kanda ya Ziwa anasema Mamlaka hiyo ina jukumu
kisheria la kusimamia uteketezaji salama wa bidhaa za dawa na vifaa tiba nchini
kwa mujibu wa Sheria kifungu namba 49 na 85.
Anasema TMDA hutekeleza jukumu hilo kwa kufuata mwongozo wa
uteketezaji wa dawa wa mwaka 2009 ambapo hatua mbalimbali hufuatwa.
“Uteketezaji wa dawa na vifaa tiba upo wa aina mbili.
Uteketezaji wa hiari wa bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara na uteketezaji wa
dawa usio wa hiarikwa dawa na vifaa tiba vilivyokamatwa kwa sababu mbalimbali,”
anabainisha.
Anaongeza “Uteketezaji wowote kati ya aina hizo mbili
hufuata sheria ya dawa sura 219, kanuni za uhifadhi na uteketezaji wa dawa za
mwaka 2015 zilizotengenezwa chini ya kifungu 122 cha Sheria ya Dawa na Vifaa
Tiba na mwongozo wa uteketezaji wa dawa wa mwaka 2009.
UTEKETEZAJI
WA HIARI
Mtani anasema hatua mbalimbali hufuatwa ikiwamo kufanya maombi ya
kuteketeza dawa kutoka muhusika anayehitaji kuteketeza dawa au vifaa tiba (kwa
watoa huduma za afya, maduka ya dawa).
“Hatua hii ya maombi huambatana na orodha ya dawa na vifaa
tiba vinavyopaswa kuteketezwa ambayo kawaida huandaliwa kutoka katika rejesta
ya dawa au vifaa tiba vilivyokwisha muda wake wa matumizi.
“Orodha huwa na taarifa muhimu za dawa, kwa mfano jina la
biashara la dawa, jina halisi la dawa (generic name), nguvu ya dawa, aina ya
dozi (vidonge, sindano kapsuli na nyinginezo), toleo la dawa au vifaa tiba,
tarehe ya kwisha muda wa matumizi, kiasi cha dawa, thamani na sababu ya
kuteketezwa,” anasema.
Mtani anaongeza “Maombi hayo siku hizi yanaweza pia
kufanyika kwa njia ya mtandao wa taasisi hiyo kupitia mfumo wa
imis2.tmda.go.tz/portal.
Anasema baada ya maombi na orodha kuwasilishwa katika ofisi
za mamlaka hiyo, wakaguzi huandaa ukaguzi kuthibitisha taarifa zilizowasilishwa
na thamani halisi iliyowasilishwa.
FOMU
MAALUM
“Katika ukaguzi huu, wakaguzi pia hupendekeza njia bora ya
uteketezaji wa dawa kulingana na aina ya dawa husika, ukaguzi wa kujiridhisha hufanyika
na taarifa zote hujazwa katika fomu maalum ‘verfication form) ambayo husainiwa
pia na mmiliki wa dawa au vifaa tiba vinavyotakiwa kuteketezwa,” anabainisha.
Anasema iwapo bidhaa zitathibitishwa pamoja na thamani,
Mamlaka hiyo hupanga tarehe na mahala ambapo zitateketezwa na kumjulisha mteja
kwa barua.
“Tunaiandikia pia Mamlaka ya usimamizi wa eneo ambako uteketezaji utafanyika ili kuwajulisha juu ya jambo hilo, TMDA huwajibika kuzitaarifu taasisi zingine zinazohusika ili kushiriki katika uteketezaji huo likiwamo Jeshi la Polisi, Mfamasia, Afisa Mazingira, Usalama wa Taifa na mwakilishi wa mmiliki wa dawa au vifaa tiba vinavyoteketezwa,” anabainisha.
USALAMA
WA VIUMBE
Mtani (pichani) anasisitiza “Uteketezaji wa dawa hufanyika kwa
kuzingatia sheria zilizopo ambazo hulenga kulinda usalama wa mazingira na
viumbe vilivyomo.
“Pamoja na mwongozo wa uteketezaji salama wa dawa nchini,
pia tunazingatia Sheria ya Baraza la Mazingira nchini (NEMC).
“Kutokana na tabia za dawa mbalimbali, tuna wajibu wa
kuainisha njia sahihi ambayo hufaa kwa uteketezaji fulani ili kuhakikisha
usalama wa mazingira na viumbe unalindwa,” anasema.
Anasema baada ya uteketezaji kukamilika fomu maalum hujazwa
(disposal waste) ambayo huainisha eneo ambapo uteketezaji umefanyika, njia
iliyotumika kuteketeza bidhaa husika, uzito na thamani halisi bidhaa
iliyoteketezwa.
“Fomu hiyo kwa kawaida husainiwa na maafisa waliosimamia
uteketezaji pamoja na mmiliki au mwakilishi wa mmiliki wa bidhaa husika,”
anabainisha.
Anasema uteketezaji unapokamilika cheti maalum utolewa
‘disposal certificate’, cheti hicho cha uteketezaji wa dawa au vifaa tiba huwa
na taarifa muhimu ikiwamo njia iliyotumika kuteketeza, kiasi au uzito wa dawa
pamoja na thamani ya dawa au vifaa tiba.
“Kila wakati ni jambo muhimu na la msingi kuzingatia njia
sahihi za uteketezaji salama wa dawa au vifaa tiba, kwa sababu husaidia kuhakikisha
uteketezaji umekamilika na bidhaa zimeharibiwa kwa asilimia 100.
“Hivyo hazina madhara tena kwa mazingira na viumbe, kuhakikisha
tukio zima la uteketezaji halizalishi kemikali au mazao ambayo yanaweza
kuathiri mazingira na viumbe katika eneo husika,” anasisitiza Mtani.
BAADHI
YA NJIA ZINAZOTUMIKA
“Dawa ngumu, nusu –imara na poda hizi tunatumia njia ya
kufukia, joto la juu 850C hadi 1000C na kupunguza kusambaa (immobilization).
“Kwa vimiminika tunateketeza kwa kupitisha chini ya ardhi
katika mabomba maalum (sewer), kwa joto la juu, kubadili dawa ili kutokuwa na
madhara kwenye mazingira (treated waste),” anasema.
Anaongeza “Dawa za saratani tunateketeza kwa kubadili dawa
ili kutokuwa na madhara katika mazingira au kufukia, kuteketeza kwa joto la juu
au kurudisha kwa mtengenezaji.
“Dawa zinazodhibitiwa (enye dawa za kulevya) tunateketeza
kwa kubadili dawa ili kutokuwa na madhara katika mazingira au kufukia,
kuteketeza kwa joto la juu.
“‘Aerosol and Inhalers’ hizi tunazifukia bila kubadili dawa
ili kutokuwa na madhara katika mazingira.
“Vipukusi hivi tunateketeza kwa kupitisha chini ya ardhi
katika mabomba maalum (sewer) au kupitisha katika maji yaendayo kasi.
“PVC plastiki, glass (ampuli, chupa na vials) hizi
tunafukia au kubadili na kuzitumia tena (re-cycling) na kwa upande wa ‘paper na
cardboard’ hizi tunabadili kwa matumizi mengine tena, tunachoma au kufukia,”
anabainisha.
Mtani Anaongeza “Dawa nyingi ambazo tumekuwa tukiteketekeza
kwenye mazingira yetu zina sifa ya kuteketezwa kwenye vinu vyenye joto la juu,
kwa hapa mazingira yetu (Kanda ya Ziwa) tunateketeza Hospitali ya Rufaa ya
Kanda - Bugando.
Chapisha Maoni