Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


 Na Veronica Mrema - Mwanza

Madini tembo 'heavy metals' kimsingi hayahitajiki kabisa kuingia mwilini mwa binadamu, hata hivyo yanapoingia kuna kiwango ambacho mwili huweza kuhimili.

“Yapo baadhi ya madini tembo yanapoingia huenda kuharibu viungo mbalimbali vya mwili ikiwamo figo mifupa na viungo vingine," anasema Mchunguzi wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA – Kanda ya Ziwa, Maximillian Rwezaula.

Anafafanua “Kwa mfano madini tembo aina ya ‘lead’ yanapoingia mwilini, badala ya kuifanya mifupa kuwa imara, yenyewe huifanya kuwa dhaifu.

“Madini tembo aina ya ‘mercury’ yanapoingia mwilini yenyewe huweza kuharibu mishipa ya fahamu ya binadamu na hivyo kuathiri uwezo wake wa kumbukumbu, mtu anakuwa anasahau mambo.

“Madini tembo yakiwa kwenye vipodozi kwa kiwango kikubwa binadamu anapotumia huenda kuathiri ngozi yake,” anasema.

Anaongeza “Hivyo, kwa kuwa kuna kiwango kidogo ambacho mwili huweza kuvumilia, ndiyo maana tunafanya uchunguzi, ili kujiridhisha kwamba bidhaa ile inapotumiwa na binadamu haiendi kumsababishia madhara makubwa.

“Kwa kuwa TMDA sasa hivi hatuna mamlaka ya kudhibiti bidhaa za vyakula, ndiyo maana tunaalika wadau wanaohusika na udhibiti wa bidhaa hiyo kuja kushirikiana nasi kufanya tafiti.

“Ikiwa tutafanya sisi TMDA hatuna mamlaka ya kutoa matokeo ya kile tulichokibaini kwenye sampuli, isipokuwa majibu ya sampuli yatakabidhiwa kwa mamlaka zinazohusika.

“Aidha, wanafunzi wanaotaka kufanya tafiti nao tunawaalika waje, tutafanya nao, kwa sababu mashine tunayo na ni ya kisasa,” anatoa rai.

MASHINE YENYEWE

"MP AES (Microwave Plasma – Atomic Emission Spectrometer) ni miongoni mwa mashine za kisasa tulizonazo ndani ya maabara hii.

“Mashine hii imenunuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ina uwezo mkubwa wa kuchunguza aina  tofauti tofauti  ya madini tembo kwa wakati mmoja.

 “Yaani kwa mfano naweza kuchunguza madini tembo aina ya copper, lead na mercury kwenye sampuli moja kwa wakati mmoja, tofauti na mashine nyingine ningelazimika kupima (kuchunguza) aina moja moja,” anasema Rwezaula. (Chini, akifafanua jambo mbele ya mashine hiyo. Picha na Veronica Mrema)

Anasema mashine hiyo ni ya kipekee kwani imeundwa tofauti na mashine nyingine zinazotumika kuchunguza madini tembo, yenyewe haitumii kabisa gesi aina ya petroleum.

“Inatumia gesi ya naitrojeni ambayo tunaivuna kutoka kwenye mazingira yetu yanayotuzunguka, haitumii kabisa ‘petroleum gas’ ambayo kiuhalisia yenyewe ni kama moto.

“’Petroleum gas’ ni kama zile zinazotumika kupikia majumbani, mashine inapotumia ‘petroleum gas’ mtaalamu anapoiwasha ili kufanya uchunguzi wa sampuli zake hulazimika kukaa hapo hapo hadi zitakapomalizika kisha aizime,” anasema.

Anaongeza “Lakini kwa kuwa mashine hii tuliyonayo haitumii ‘petrolium gas’ bali tunatumia ‘naitrogen gas’, wataalamu hatulazimiki tena kuweka sampuli na kusubiri hadi zimalizike ili tuzime mashine.

“Tunao uwezo wa kupanga sampuli zetu na ku-set muda ambao tunataka mashine ifanye kazi ya uchunguzi na kuiacha ikifanya kazi yenyewe, wakati huo tukiendelea na shughuli nyingine ndani ya maabara,” anasema.

Rwezaula anasema mashine hiyo itafanya kazi yake ya kuchunguza madini tembo ndani ya sampuli zilizopangwa na muda ule ambao mtaalamu ame-set unapokamilika, hujizima yenyewe.

“Ndiyo maana wakati ikiendelea na kazi ya kichunguzi, mtaalamu anaweza kuendelea na shughuli nyingine, ule muda ukiisha tu, mashine hujizima yenyewe, hii ni faida kubwa mno ya kutumia mashine hii,” anasisitiza.

SAMPULI ZIPI?

Rwezaula anabainisha baadhi ya sampuli zinazofanyiwa uchunguzi wa madini tembo kwa kutumia mashine hiyo ya MP AES ni vifaa tiba, maji, vipodozi na kwenye vyakula.

“Kwa mfano maji yanayotengenezwa viwandani hayawezi kuruhusiwa kwenda kuuzwa sokoni, mtaani pasipo kufanyiwa uchunguzi wa madini tembo, hapa TMDA tuna uwezo huo.

“Kwa upande wa vyakula, kwa mfano kwenye sukari, mchicha tunaweza kuchunguza, kwa kushirikiana na wadau (taasisi) zinazohusika na kufanya tafiti hizo kwenye vyakula pamoja na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wanaofanya tafiti,” anasisitiza.

KUHUSU DAWA

Anasema mashine hiyo yenyewe imeundwa mahususi kwa kuchunguza sampuli za vifaa tiba, maji, chakula na vipodozi pekee.

“Kwa upande wa uchunguzi wa ubora, ufanisi na usalama wa bidhaa za dawa, huwa tunatumia mashine nyingine za kisasa tulizonazo ndani ya maabara, kuzichunguza sampuli hizo,” anasema.

Anaongeza “Kwa kutumia MP AES tunachunguza sampuli za vifaa tiba kwa mfano sindano na huwa hatuweki moja kwa moja sindano kama sindano, tunachukua sindano tunaiweka kwenye maji kwa muda fulani, tunaiacha humo.

“Ikiwa sindano ile ina madini tembo, yatatoka na kuingia kwenye maji, sampuli hiyo ndiyo ambayo tutaichukua na kuifanyia uchunguzi kwa kutumia mashine hii,” anabainisha.

Rwezaula anasema ikiwa madini hayo yamo kwenye sindano yatabainika kwa kutumia sampuli hiyo iliyopatikana na ikiwa hayamo mashine hiyo itawawezesha wataalamu kubaini pia.

“Jambo la muhimu linalozingatiwa, linalofanyika humu ndani ni kujiridhisha kwamba bidhaa zilizoruhusiwa kuingia sokoni ni salama, bahati nzuri ni kwamba hatujawahi kupata bidhaa ambazo zina kiwango kikubwa cha madini tembo.

“Endapo kama bidhaa imepita bila kupitishwa na TMDA kwa ajili ya uhakiki na zikawa na madhara itakuwa athari kubwa kwa jamii.

“Lakini kwa kuwa waingizaji wanazingatia maelekezo, wanaleta sampuli kabla ya mzigo kuruhusiwa kuingizwa nchini, tunahakiki na kuwapa majibu, hii ni faida kubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” anasema Rwezaula.

VIWANGO KIMATAIFA

Mchunguzi huyo mbobezi anasema japokuwa madini hayo hayahitajiki kuingia ndani ya mwili wa binadamu lakini kipo kiwango ambacho kinaweza kuhimilika kinapoingia,

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeweka viwango vinavyoweza kuhimilika ambavyo hata hivyo ni siri katika kuimarisha shughuli za kidhibiti duniani.

“Ni ‘confidenital’ (siri) sisi (watafiti / Mamlaka za udhibiti) ndiyo ambao tunajua kiwango gani kinaweza kuhimilika kwenye mwili, tunapofanya uchunguzi lazima tukute ama kile kinachopendekezwa na WHO au chini lakini kinapozidi hatuwezi kuruhusu bidhaa hiyo kuingizwa sokoni.

“Mtengenezaji tutamueleza tu tumezuia bidhaa na sababu ni ipi, lakini kile kiwango kinachopaswa huwa hatukiweki wazi, ni siri na hii ni ‘international standards’,” anasisitiza.

Meneja wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza anasema matokeo ya uchunguzi wa sampuli hizo hutumika katika ngazi za juu za maamuzi kwa manufaa ya kulinda afya ya jamii.

“Zipo kwa lengo la kimaamuzi kwa ajili ya Taasisi za Kidhibiti duniani, ndiyo maana vile viwango ni siri,” anasema Simwanza.

Jengo la TMDA - Kanda ya Ziwa, Buzurugwa Mkoani Mwanza ambako ndiko kuna mashine hiyo.

MILANGO IPO WAZI

Simwanza anasisitiza kwamba Mamlaka hiyo ‘imefungua milango’ yake kwa wadau mbalimbali wa masuala ya tafiti za madini tembo, kushirikiana nao kwa lengo lile lile la kuendelea kulinda afya ya jamii. 

“Mamlaka ‘imepanua wigo’ wa ushirikiano na wadau wa tafiti za madini tembo ndani na nje ya nchi, tuna mashine ya kisasaka Mashariki (EAC), hivyo si tu kwa Tanzania bali pia katika nchi zilizopo katika Ukanda huu,” anasisitiza.

Simwanza anaongeza “Hatua hii ya ‘kupanua wigo’ wa ushirikiano wa kitafiti kwa upande wa madini tembo na wadau wengine, ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe, aliyoyatoa Septemba, 2020 alipotembelea maabara hiyo.

“Katibu Mkuu alielekeza TMDA tushirikiane na wadau mbalimbali katika eneo hili (la uchunguzi wa madini tembo), wadau walete sampuli zao tupime, majibu yapatine mwisho wa siku tulinde afya ya jamii,” amebainisha.

Anaongeza “Tumeanza utekelezaji, tunaalika taasisi zinazofanya tafiti walete sampuli zao, mashine tunayo imenunuliwa na Serikali kwa takribani Sh. bilioni moja na wataalamu tunao, wadau waje tushirikiane.

TAFITI KANDA YA ZIWA

Kaimu Mkuu wa Maabara wa TMDA - Kanda ya Ziwa, Bugusu Nyamweru anasisitiza “Kimsingi katika mfumo wa tiba kuna kiwango ambacho mwili wa binadamu unatakiwa kuwa na madini tembo na kila mmoja anacho.

“Lakini ni kile ambacho mwili unaweza kuhimili na kwamba kiwango hicho kinapozidi huleta athari.

“Binadamu wote tuna madini tembo kiasi fulani, kwa mfano  dhahabu wote tunayo mwilini lakini ni kwa kile kiwango ambacho unahimili, kiwango cha madini hayo kikizidi mwili unapata athari mbalimbali,” anasema.

 “Hivyo lengo letu (TMDA – Kanda ya Ziwa) ni kuongeza wigo katika masuala ya uchunguzi na tafiti, vifaa vipo, tunatoa wito kama kuna taasisi itahitaji kufanya tafiti eneo hilo tupo tayari,” anasisitiza.

Nyamweri anaongeza “Kwa sababu maabara hii kama sehemu ya Mamlaka, katika eneo ambalo tunaona linahitaji kuongeza wigo ni kwenye tafiti.

“Kwa mfano, ukweli kabisa Kanda ya Ziwa kunaonekana kuna kesi nyingi za saratani tunajua kule kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wanatumia ‘mercury’ na wakati mwingine wanashika kwa mikono, tunahitaji kushirikiana na wadau wanaofanya tafiti, walete sampuli hizo tuzichunguze,” anasema.

Nyamweru anasema wanawaalika wadau hao ili washirikiane nao katika tafiti hizo kwani wanafahamu kwamba kweli takwimu zinaonesha kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani inayotokea katika Kanda hiyo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement