Na Veronica Mrema - Dodoma
Mgonjwa mmoja mwenye tatizo sugu la figo (kidney failure) huhitaji huduma ya uchujaji damu ‘dialysis’ si chini ya mara tatu kwa wiki, katika kila awamu hulazimika ‘kukaa’ kwenye mashine kwa wastani wa saa nne.
Hii ni ratiba mpya ambayo mtu aliyegundulika kuugua tatizo
hilo hulazimika kuianza na kuishi nayo maisha yake yote ama hadi pale atakapofanikiwa
kupata mtu wa kumchangia figo nyingine ya kupandikizwa.
Kulingana na wataalamu wa afya, kuna aina mbili za magonjwa ya figo, yale ya dharura na sugu.
Wanatoa mfano kwamba, mjamzito anapopoteza damu nyingi wakati
wa kujifungua au majeruhi wa ajali akipoteza damu nyingi, hupata tatizo la dharura la figo, figo hushindwa kabisa kufanya vema kazi yake ya kutoa sumu taka mwilini.
“Mtu anapougua ugonjwa wa dharura wa figo, ikiwa
hatagundulika mapema na kupatiwa matibabu sahihi kwa wakati anaweza kuishia
kuugua ugonjwa sugu wa figo, yaani figo zake hushindwa kabisa kufanya kazi yake ya
kuchuja sumu taka mwilini,” anasema Mtaalamu wa Afya ya Jamii wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dodoma, Awadhi Mohamed.
Anaongeza “Yapo baadhi ya magonjwa ikiwamo kisukari,
shinikizo la damu mtu anapougua, asipotibiwa kwa wakati, asipozingatia maelekezo
ya wataalamu anaweza pia kuishia kuugua ugonjwa sugu wa figo.
“Figo ni kiungo chenye umuhimu mkubwa kwa binadamu ikiwamo
kuweka sawa ‘pressure’ ya mwili. Tatizo la ‘pressure’ na ugonjwa wa figo,
ukiangalia kwa kina utaona ni kama vile kuku na yai.
“Yaani ‘pressure’ inaweza kusababisha figo kuathiriwa, vile
vile figo zikipata shida zinaweza kuathiri ‘pressure’ ya mwili,” anasema.
Mohamed anaongeza “Mtu huyu anaweza kupata athari kubwa kwa
sababu kazi kubwa ya figo ni kutoa sumu taka mwilini, hivyo kama hazitoki
atabaki na kiasi kikubwa cha maji mwilini.
“Anaweza kupata shida ya kupumua, mwili kujaa maji,
kuvimba, kwa sababu sumu hazitoki mwilini mtu huyo tunategemea atabaki na kiasi
kikubwa cha maji mwilini, shida ya kupumua.
“Figo zinasaidia pia katika uzalishaji wa chembechembe hai
za damu mwilini, ambazo humsaidia binadamu damu yake kuongezeka inapokuwa
imepungua na kuzalisha damu mpya.
“Ndiyo maana binadamu anaweza kuchangia damu na baada ya
muda damu inarudi katika kiasi kile ambacho kinahitajika mwilini mwake,”
anabainisha.
Anaongeza “Lakini figo zinaposhindwa kufanya kazi, hali hiyo huweza kusababisha mtu kupata upungufu wa damu mwilini mwake.
SUMU
TAKA
Mohamed (pichani) anasema mtu akipata athari ya figo, sumu taka
hazitoki, kuna uwezekano akashindwa kupata haja ndogo.
“Kwa sababu, haja ndogo hutengenezwa kutokana na ule
uchakataji wa sumu taka mwilini ili kuzitoa nje kwa njia ya mkojo.
“Kwa kuwa sumu taka hazitoki mwilini kwa njia ya haja ndogo, zinaanza kuwa nyingi mwilini, hatimaye muhusika anakuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha, ikiwa kitakachofanyika (matibabu) kwa wakati,” anasema.
Anaongeza “Hivyo, atahitaji kutengenezewa njia mbadala
kumsaidia, ndiyo hiyo ya usafishaji wa damu (dialysis) ili kuondoa sumu taka
mwilini na pia kupunguza kiwango kikubwa cha maji mwilini mwake.
“Kwa sababu, zile sumu tyaka hazitoki mwilini, ndizo zinazomletea athari kubwa, kwa hiyo kinapunguzwa ili kumrudisha mtu kwenye hali yake,” anasema.
MASHARTI
MUHIMU
Mohamed anasema lakini kwa sababu mtu huyu anaendelea
kuishi, kula na kunywa maana yake atahitaji kuendelea kufanyiwa ‘dialysis’ kwa
maisha yake yote hadi pale atakapoweza kupata mtu wa kumchangia figo nyingine,
apandikizwe.
“Mgonjwa atapewa masharti maalum ya kuzingatia nini ale,
nini asile, nini anywe, kwa kiwango gani ili kumsaidia asipate matatizo mengine
yanayoweza kumfanya augue,” anasema.
Anaongeza “Ni kipindi kigumu, maisha yake hubadilika
ghafla, ukiacha huo muda wa kukaa kwenye mashine akipatiwa huduma hiyo, bado
kuna muda wa kwenda hospitali na kurudi nyumbani, kuna suala la gharama na
mengine mengi.
“Si kila mtu huweza kwa haraka sana kubadilika na kuikubali
haraka hali hii mpya, kwa mfano unakuta mwingine ni mwajiriwa, pengine anaishi
eneo mbali na kilipo kituo cha usafishaji damu.
“Unakuta alikuja hospitali akitarajia kutibiwa na kurudi
nyumbani lakini sasa analazimika kukaa kwa muda kwa ajili ya kufanyiwa
‘dialysis’, tayari hii ni shida kwake,” anasema.
Anaongeza “Atakaa hospitali kwa siku kadhaa na
anaporuhusiwa bado atatakiwa kurudi tena hospitalini kliniki, athari tunaanza kuiona, huenda ana familia
inayomtegemea, sasa hawezi tena kuisaidia, analazimika kuomba msaada.
“Je, jamii inayomzunguka nayo inamuelewa namna gani, ipo
tayari kumsaidia?.. mambo mengi yanajitokeza, hapo ndipo kitengo chetu umuhimu
wake ulipo, kuhakikisha familia yake inaelewa ugumu wa aina ya matibabu
anayoyapitia.
“Je! Yanachukua muda gani na yanawahitaji kiasi gani ili
yawe endelevu kwa mgonjwa husika,” anafafanua Mtaalamu huyo wa Afya ya Jamii
BMH.
Anasema hivyo, kitengo hicho humsaidia mgonjwa kumuunganisha
na huduma nyingine pale inapohitajika.
“Kwa mfano, inawezekana alikuja hospitalini akiwa ameaga
siku mbili kazini, amefika amepewa ratiba mpya ya kukaa mwezi mzima kwa
matibabu, lazima ofisini kwake wajulishwe, kitengo chetu kinahusika kufikisha
taarifa hiyo.
“Wengine wanalazimika kuhitaji msaada wa kuhamia vituo vya kazi jirani na vituo vya usafishaji hadi pale watakapomaliza matibabu (upandikizaji figo),” anasema.
Mohamed (pichani) anaongeza “Hiyo ni hatua ya mbele, hatuwezi kwenda
kwenye upandikizaji kama hali yake ya ugonjwa inahitaji usafishaji kwanza.
NAFASI
YAO
“Idara yetu
inawajibika pia kuhakikisha huduma zote zinazotolewa hapa zinakuwa rafiki kwa
watu wote, zinafurahiwa na kila mtu na lengo la matibabu linafikiwa,” anasema.
Anaongeza “Kulingana na tafsiri ya neno afya, kwa mujibu wa
Shirika la Afya Duniani (WHO), ni ile hali ya mtu kuwa vizuri kimwili, kiakili
na kijamii na si tu kuwa na ugonjwa ama udhaifu mwilini mwake.
“Tafsiri hii ilitolewa na WHO tangu mwaka 1948 hadi sasa
haijabadilishwa, ndiyo sababu katika hospitali wapo watalaamu mbalimbali
ikiwamo wanaohusika na masuala ya afya ya jamii.
“Wataalamu hao wanafanya kazi upande wa pili wa kimatibabu
ukiacha yale yanayohusisha utaalamu wa kitabibu moja kwa moja, dawa,
upandikizaji, na mengineyo,” anasisitiza.
Mohamed anasema katika maeneo yote ya hospitali kuna
kipande ambacho ni lazima mtu awe imara kama maana ya afya inavyoeleza kiafya,
kijamii na kiuwezo.
“Kwa maana ya mtu kujiweza katika kufanya maamuzi, katika
kukubali, kufahamu vitu na shida gani imempata, na anatakiwa apitie taratibu
zipi za matibabu, itachukua muda gani, ni ugumu gani atakutana nao.
“Katika yote hayo kuna kujengewa hali ya mtu kuweza kuishi
hali aliyonayo, hapo ndipo hizi timu zinakutana (daktari na ‘social worker’), kila
mmoja atatoa huduma kwa upande wa utaalamu wake, kumsaidia mgonjwa husika,”
anasema.
Anaongeza “BMH tumefanikiwa kuwapandikiza figo wagonjwa zaidi
ya 15, kwa zaidi ya asilimia 95 wanazingatia maelekezo tunayowapa, asilimia
iliyobaki bado kuna changamoto katika kuzingatia, tunazidi kuongeza juhudi
kuwahamasisha wazingatie kwa kutumia mbinu mbalimbali tulizonazo.
“Zaidi ya asilimia 98 ya wagonjwa wanaopata huduma ya ‘dialysis’ BMH awali walipofika hapa hawakuwa wanajua hali zao na kwamba wanatakiwa kuanza kupata huduma hiyo, mapema,” anabainisha.
Picha zote kwa hisani ya BMH
Chapisha Maoni