Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima akifafanua jambo (picha kwa hisani ya mtandao)

*Mrundikano wa abiria vyombo vya usafiri nao wagusiwa

*Mfamasia Mkuu aagizwa kutangaza orodha watengenezaji barakoa waliothibitishwa 

*Aagizwa kutoa elimu utengenezaji vipukusi ndani ya nchi vipatikane kwa gharama nafuu

Na Veronica Mrema 

Vaa barakoa kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hususan katika maeneo ya msongamano, imesisitizwa.

Aidha, Mfamasia Mkuu wa Serikali ameelekezwa kutangaza orodha ya watengenezaji barakoa waliothibitishwa sambamba na kuelimisha jinsi ya kutengeneza barakoa binafsi.

Vile vile imeelekezwa elimu juu ya uvaaji wa barakoa iendelee kutolewa na wataalamu wa afya nchini. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima ametoa maagizo hayo leo kupitia tamko lake kwa umma akisisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza nchini.

"Vaa barakoa safi na salama ambayo umetengeneza mwenyewe au umenunua kwa watengenezaji wa ndani waliothibitishwa na Wizara ya Afya mfano Bohari ya Dawa, taasisi zetu za afya na watengenezaji wengine ambao tumewathibitisha," amesisitiza Dk. Gwajima.

Waziri huyo mwenye dhamana ya afya, amefafanua kwamba kila mwaka kipindi cha Novemba hadi Machi wimbi la magonjwa hususan yale yanayoathiri mifumo ya upumuaji na chakula huongezeka. 

Amebainisha hali hiyo hutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mvua nyingi ambazo huendelea kunyesha kipindi hiki. 

"Magonjwa haya yanaweza kusababishwa na vimelea vya bakteria, virusi na fangasi huambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali ikiwemo hewa, kula au kunywa kitu ambacho siyo kisafi na salama. 

"Mifano ya magonjwa haya ni pamoja homa za mapafu (Nimonia), mafua, malaria, kuhara, kuhara damu, kipindipindu typhoid, dengue, na mengine mengi. Baadhi ya magonjwa ya kuambukiza yanaenda na vipindi vya majira ya mwaka au kutokea kama mlipuko. 

"Tukiacha mwenendo huu wa magonjwa kila mwaka, kipindi hiki pia tumeshuhudia dunia ikipambana na wimbi la pili la mlipuko wa ugonjwa wa COVID- 19. Kwa msingi huu tunahitaji kuongeza kasi zaidi ya kuchukua tahadhari dhidi ya mwenendo huu wa magonjwa yote haya kwenye kipindi hiki kama Wizara ya Afya tunavyoelekeza," amesema. 

Ameongeza "Wizara ya Afya inayo miongozo ya kutosha ambayo imekuwa ikisambazwa na kuelimishwa na wataalamu wetu kupitia mifumo ya afya kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya kijiji. 

Amesema miongozo hiyo imetamka bayana uhusika wa wadau wote wa sekta na wizara zote, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi za Umma na Binafsi kuwa nani anahusika wapi katika kila mkakati wa udhibiti wa magonjwa haya. Hivyo, kila mmoja kwa nafasi yake sasa achukue hatua na atimize wajibu wake. 

"Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu wameshafanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa matamko ya kukumbusha na kuelimisha taifa juu ya mwelekeo wa tahadhari za kuchukua ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. 

"Vilevile, Viongozi wa Wizara ya Afya tumetoa matamko mbalimbali ya kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari. 

"Jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote yakiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ni la kila mmoja wetu, niwakumbushe viongozi wa Serikali na sekta binafsi, viongozi wa kijamii, viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali ngazi zote tuache kusubiri matamko zaidi bali tuamke tuwajibike kila mmoja kwa nafasi yake. 

"Napenda kurudia kuelimisha na kufafanua tena juu ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kutekeleza hatua za tahadhari za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na milipuko kwa ujumla wake ikijumuisha na tahadhari dhidi ya tishio la mlipuko wa COVID-19...
 
"Kwanza tuondoe hofu zinazojengwa bila sababu wala nia njema kwa sababu hofu inaleta madhara zaidi kiafya. Tuendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni. Iwapo maji tiririka na sabuni hakuna, tumia vipukusi (sanitizer)," amesisitiza. 

Ameongeza "Namuelekeza Mfamasia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu ya jinsi gani tunaweza kutengeneza vipukusi vyetu vya ndani ya nchi ili kuwezesha wananchi kupata kwa bei nafuu. 

"Fanya mazoezi mara kwa mara. Kumbuka mazoezi yapo ya aina nyingi na unaweza kuchagua kutegemeana na hali ya afya yako na mazingira yako siku hiyo. 

"Baadhi ya mazoezi rahisi ni kama vile kutembea kwa kasi siyo chini ya dakika 30 au zaidi walau utoke jasho, kuruka kamba, kukimbia mwendo unaoona unakufaa na kufanya zoezi la kusimama-kaa nk. Naelekeza Mwongozo wa Mazoezi utolewe. 

"Fanya mabadiliko ya tabia ya lishe unayotumia kwa kuhakikisha unapata lishe bora ikiwemo matunda na mbogamboga kwa gharama nafuu kulingana na mazingira ya vyakula vya asili katika eneo lako. 

"Naelekeza Wataalamu wa lishe ngazi zote kuandaa daftari la orodha ya vyakula vya asili vinavyopatikana eneo husika na kutoa elimu ya milo ipi iandaliwe kama kielelezo cha lishe bora. Tuache kuamini kuwa lishe bora ni vyakula vya kisasa vya biashara na vya bei ghali. 

"Tambua afya yako jilinde tukulinde. Wito huu unahusu makundi maalumu ya watu wakiwemo wenye umri mkubwa (wazee), watu wenye uzito uliopitiliza (wanene) na watu wenye magonjwa sugu (muda mrefu) mfano Pumu, Shinikizo la juu la Damu, Kisukari, Magonjwa ya Moyo na Figo. 

"Kundi hili mara nyingi huathirika zaidi na magonjwa ya kuambukiza kutokana na hali ya kinga zao kuwa haiko imara zaidi hivyo, naelekeza wataalamu wa Afya muendelee kutoa elimu zaidi mkiwashirikisha Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii," amesema. 

Ameongeza "Pia, naelekeza kundi hili liwekewe mazingira mazuri ya kupata huduma za afya kwenye vituo vyetu ikiwemo kuruhusu baadhi ya dawa za kutibu magonjwa sugu kupatikana kwenye vituo vya afya na zahanati ili kuwapunguzia kwenda mara kwa mara kwenye hospitali kubwa za halmashauri au mkoa. 

"Vilevile Mfamasia Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Tiba msimamie mwongozo wa huduma kwa makundi maalum. Madirisha ya huduma za afya kwa wazee yaimarishwe sambamba na kliniki za magonjwa sugu. 

"Tumia tiba asili za kunywa na kujifukiza zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili kama inavyoelimishwa na wataalamu husika. 

"Epuka misongamano isiyo ya lazima ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri. Wizara husika isimamie kwa kurejea mwongozo wa afya eneo husika. 

"Wahi kituo cha kutolea huduma za afya mara uonapo dalili za maradhi ili watoa huduma wapate nafasi nzuri zaidi ya kutibu. Aidha, jenga tabia ya kupima afya yako mara kwa mara angalau mara 1 kwa mwaka hata kama huumwi. 

"Niwatake Maafisa Afya wanaotoa huduma mipakani kuendelea kuimarisha udhibiti wa magonjwa katika maeneo ya mipakani kwa mujibu wa miongozo husika," amesisitiza Dk. Gwajima.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement