Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Mwandishi Maalum - Dar es Salaam

Wananchi wamehimizwa kuondoa hofu kutokana na changamoto za kiafya wanazopitia, waamini wako salama kwani Serikali iko kazini kuhakikisha wanapata huduma bora za afya na hivyo kuwa salama.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Jamii na Watoto, Dk. Godwin Mollel, alipozungumza na wagonjwa wanaotibiwa Taasisi ya Moyo Jakaja Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuwashukuru wafanyakazi wa afya aliyoifanya leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. 

Dk. Mollel amewasihi wagonjwa hao kufuata ushauri wa kitaalamu wanaopewa na madaktari wanaowatibu na unaotolewa na Wizara ya Afya kwa kufanya hivyo wataweza kuepukana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na hivyo kuwa na afya njema.

“Ninawaomba wananchi muondoe hofu kwani ukiwa na hofu hata kinga za mwili zinashuka na hivyo kusababisha mwili kushindwa kukabiliana na magonjwa pale ambapo utavamiwa na vijidudu.

“Pale ambapo utakutana na changamoto mbalimbali za afya usisahau kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na  kumuomba Mungu akujalie afya njema kwani yeye ndiye kila kitu katika maisha yetu”, amesisitiza Dkt. Mollel.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi amemshukuru Naibu Waziri kwa kuwatembelea na kupata muda wa kuzungumza na wagonjwa pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo. 

Amesema mbali na Dunia kukabiliana na ugonjwa unaosababisha Virus vya Corona (COVID 19) kwa mwaka jana wa 2020 Taasisi hiyo iliweza kutibu  wagonjwa 99,046 ambapo kati ya hao wagonjwa waliotibiwa na kurudi nyumbani (outpatient) walikuwa 94,079, waliolazwa (inpatients) walikuwa 3,306 waliofanyiwa upasuaji wa kutumia tundu dogo 1262 na upasuaji wa kufungua kifua wagonjwa 399.

Amesema Taasisi hiyo haina changamoto ya upatikanaji wa dawa na  vifaa tiba na kuongeza kuwa asilimia 52 ya mapato yao yanatokana na  dawa zinazotolewa kwa wagonjwa, maabara na vipimo vingine vya uchunguzi.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na JKCI na kuhakikisha dawa zinapatikana katika Hospitali yetu na hii inasaidia wagonjwa kupata huduma zote za matibabu, vipimo na dawa bila ya usumbufu wowote”, ameshukuru Prof. Janabi.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement