Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema – Mwanza

Kila aina ya dawa inayotengenezwa duniani, ndani yake huwekwa kiambata hai ambacho ni mahususi kwa ajili ya kwenda kupambana na ugonjwa husika katika mwili wa binadamu au mnyama.

Kiambata hai hutarajiwa kuleta matokeo chanya katika tiba dhidi ya ugonjwa husika, lakini wakati mwingine dawa huweza kuleta matokeo hasi ambayo hayakutarajiwa kabla.

Ni katika hatua hiyo, wataalamu hulazimika kufanya uchunguzi wa kimaabara kuweza kujua sababu zilizochangia dawa husika kuleta matokeo hasi badala chanya.

Kimsingi, si rahisi kung’amua hilo kwa kutazama kwa macho ya kawaida, mashine za kisasa huhitajika, ili kupata majibu ya kimaabara kusaidia wataalamu kutatua changamoto iliyojitokeza.

Vivyo hivyo hata kwa upande wa maeneo mengine ikiwamo kilimo, mifugo na mazingira kwa ujumla, wataalamu huhitaji kufanya uchunguzi wa kina kuweza kujua iwapo kuna kemikali za dawa zinazoweza kuleta athari, zitatuliwe mapema kulinda afya ya jamii.

“Maabara ya TMDA (Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania), Kanda ya Ziwa tuna mashine ya kisasa LSMS / MS (Liquid Chromatograph Mass Spectroscopy).

"Mashine hii ina uwezo mkubwa wa kuchunguza  na kugundua hata kitu kidogo sana kilicho katika mwili wa binadamu,” anabainisha Kaimu Mkuu wa Maabara hiyo, Bugusu Nyamweru 

“Tunaweza kujua athari imetokea sehemu gani ya mwili, hata kama ni kitu kidogo sana kilichomo mwilini mwake,” anasema.

Kaimu Mkuu wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Kanda ya Ziwa, Bugusu Nyamweru (mwenye gloves pichani) akifafanua jambo kuhusu maabara hiyo. (Picha na Veronica Mrema)

HATUA MUHIMU

Nyamweru anafafanua “Mashine hii ina uwezo wa kupima vipande vidogo vya kemikali vilivyopo hadi kwenye mazingira, chakula na maji. Ni mahususi kwa ajili ya uchunguzi wa vitu mbalimbali na katika masuala ya tafiti.

“Ni mashine ambayo ina maeneo makuu mawili, eneo la kwanza ni upande wa HPLC (High Perfomance Liquid Chryomatography), inatumia pampu maalum.

“Pampu hiyo ni kwa ajili ya kuvuta kemikali pamoja na sampuli inayokuwa imewekwa humo ili hatimaye tuweze kuchanganua na kupata majibu,” anasema.

Anafafanua “Hivyo, eneo la kwanza ni kwa ajili ya kemikali zinazotembea, eneo la pili ni kwa ajili ya ‘column’ ambavyo vyenyewe ni vifaa vidogo lakini vina kazi kubwa kuhakikisha ile sampuli yetu tunayoichunguza inaweza kuchambuliwa na kupata kiwango cha kemikali tunayohitaji.

“Kuna eneo jingine ni maalum kwa ajili ya kuwekea sampuli zetu (autosampuler), pia kuna eneo la kuchuja ile kemikali yetu (umbo la kemikali) ili hatimaye tuweze kupata majibu, mara baada ya kuwa tumepitia hatua zote za msingi za uchunguzi,” anasema.

Anaongeza “Tunapoweka sampuli hupita kwenye ‘tube’ maalum na kuingia eneo la kutambuliwa, hutambuliwa kwa kuangalia uzito wa umbo la kemikali, kwa sababu kazi ya HPLC ni kuchambua ule mchanganyiko kwenye sampuli ili kuweza kutoa kitu tunachohitaji kwa sababu uchafu ni lazima ubaki.

“Hivyo, katika eneo la kwanza umbo la kemikali ndani ya sampuli, litaingia sehemu maalum (ndani ya mashine) ambayo ina moto mkubwa, lile umbo la kemikali litakuwa ‘ionized’, hapo tunatengeneza ‘charge’ za chanya na hasi, zile za chanya za umbo kemikali letu tutaziweka mbele.

“Zitakwenda hadi kufika sehemu ya kuchujwa na kwenda mbele zaidi, litaweza tena kuchanganuliwa, tunaligawanya tena lile umbo la kemikali kisha linaingia eneo jingine ambako litachambuliwa na hatimaye kufikia hatua ya mwisho ya kuweza kutambuliwa.

UCHANGANUZI

Nyamweru anasema uchanganuzi hufanyika mara mbili, ambapo katika sehemu ya kwanza wataalamu huichanganua kisha mchanganuo huo wa kwanza huchanganuliwa tena katika sehemu ya pili.

“Ikiwa tunaangalia umbile la kemikali tunahakikisha kwamba sampuli husika imechanganuliwa katika vipande vipande ili hatimaye tuweze kuvitambua (kuving’amua) kwamba vipande hivyo vinatokana na umbo fulani la kemikali,” anasema.

Anaongeza “Kwa mfano, vimelea kama bakteria havionekani kwa macho lakini kwa kupitia mashine hii tunaweza kuchanganua, hatimaye kujua kwa umbo la kemikali tuliloliona baada ya kupitia hatua zote za uchanganuzi linatokana na bakteria fulani.

“Mashine hii inaweza pia kutumika katika maeneo mengi, yahusuyo masuala ya dawa, tunaweza kutambua ikiwa kuna uchafuzi umetokea kwenye dawa fulani.

“Tunao uwezo kuangalia iwapo kuna kiambata kisicho hai kwenye dawa… na ni aina gani ya kiambata kilichoingia humo na hivyo kuifanya dawa husika kushindwa kutoa matokeo chanya, tarajiwa.

“Vile vile, tunaweza kuchunguza kujua iwapo kiambata hai kinachostahili kuwamo ndani ya dawa kimeanza kuharibika na hivyo kuifanya dawa husika kushindwa kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa katika mwili wa binadamu, anapoitumia,” anabainisha.

Anasisitiza “Kimsingi, kwa kutumia mashine hii, watafiti tunao uwezo wa kutambua umbo kemikali la dawa. 

Jengo la TMDA lililojengwa Buzurugwa, Mkoani Mwanza lina mashine za kisasa na wataalamu wabobezi wenye uwezo wa kufanikisha uchunguzi huo.

MABAKI MWILINI

“Aidha, katika masuala ya tafiti za kuangalia jinsi dawa inavyofanya kazi mwilini, mashine hii inaweza kutumika kujua kama mabaki ya dawa katika mwili wa binadamu.

“Baada ya kupitia katika vimeng’enya vyote mwilini, tunaweza kujua mabaki ya dawa mwilini mwake yana umbo gani na yanatengenezwa kwa kemikali zipi.

“Kwa hiyo, ikiwa tunataka kujua, je dawa ambayo mgonjwa husika ameitumia ipo katika sehemu fulani ya mwili wake kwa kiasi gani, tunaweza kujua kwa kutumia mashine hii,” anasema.

Anabainisha “Kwa mfano, kwenye mate, tishu za mwili wake au kuangalia iwapo iliingia ghafla kwenye moyo, ini au sehemu nyingine yoyote ya mwili… na je iliingia kwa kiasi gani, ili kuweza  kuchukua hatua zaidi.

MAZINGIRA

Nyamweru anasema pia wanao uwezo wa kuchunguza kwenye mazingira kujua kama kuna kemikali za dawa zilizoathiri, kwa kuzichambua na kuzing’amua kujua ni kemikali gani zilizoleta uchafuzi huo.

“Kwa mfano kwenye masuala ya kilimo, mashine hii ni muhimu katika kusaidia wataalamu kujua kama kuna uchafuzi wowote uliotokea kwenye maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuleta athari kwenye vyakula vinavyolimwa eneo husika,” anasema.

MIFUGO

Anasema wanatumia mashine hiyo kuweza kung’amua iwapo kemikali za madawa zinazotumika kuwapa mifugo, zinaweza kuleta athari kwa binadamu au la!.

“Kwa sababu mifugo tunaitumia pia kama chakula, lakini kwa sababu inakula madawa, ni muhimu kuchunguza kujua usalama wake ili mwisho wa siku tusijikute tunatumia madawa ambayo pengine hatukustahili kuliwa na binadamu.

“Hivyo mashine hii inatusaidia kufanya uchunguzi huo ili kutambua hayo, mashine hii ina manufaa mengi katika kulinda afya ya jamii,” anasisitiza.

MITISHAMBA

Nyamweru anaongeza “Hata wadau wanaotaka kufanya tafiti kwa upande wa dawa za mitishamba kujua kemikali zilizomo ndani, tunawaalika washirikiane nasi.

“Walete sampuli zao tuzichunguze kung’amua kemikali zilizomo na hadi kiwango ambacho kimo ndani ya dawa zao, tutaziainisha,” anatoa rai.

Anasisitiza kwamba mashine hiyo ina uwezo mkubwa katika kufanya kazi mbalimbali katika maeneo mengi hata kwa upande wa ‘protin’.

“Ina uwezo wa kuzichanganua, tukitaka kujua ‘protin’ gani zipo katika mwili wa binadamu, tunaweza kuitumia mashine hii kuchanganua na hatimaye kuzing’amua,” anasema Nyamweru.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement