Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

“Nilipofanyiwa upasuaji, siku iliyofuata niliweza kuamka na kukaa kitandani, nilipokaa, nilishangaa kujiona nimekuwa mrefu tofauti na hapo kabla ya upasuaji, nilijisemea mwenyewe… ‘kumbe mimi ni mrefu kiasi hiki’.

Ni simulizi ya Tecla Mwambulukutu, msichana aliyekuwa na tatizo la kibiongo kabla ya kutibiwa kwa upasuaji wa kisasa, mwaka 2019 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu, Mgongo na Uti wa Mgongo Muhimbili (MOI).

Ni mtoto wa pili kuzaliwa miaka 17 iliyopita ndani ya familia ya Janeth na Nathan Mwambulukutu, mamake anasema alipozaliwa hakuwa na ulemavu wa aina yoyote ile.

“Lakini alipofika darasa la saba, nilianza kumuona mgongoni kama kuna kupinda fulani hivi, sehemu ya pingili mbili, kwenye mgongo wake, nilimueleza nilichokiona, aliniambia hata yeye hajui ni kitu gani,” anasimulia Janeth.

Janeth anaongeza “Alikwenda kidato cha kwanza, aliporudi likizo kipindi cha Pasaka, nilimnunulia nguo ya sikukuu, alipokuwa akiijaribisha niliona pale mgongoni pamezidi kupinda, nilimuuliza tena, alinijibu hajui ni kitu gani.

“Mara nyingi alikuwa akilalamika kupata maumivu makali ya mgongo, ilibidi nimpeleke hospitalini kwa uchunguzi zaidi, tulizunguka hospitali mbalimbali za kawaida, hawakugundua chochote hadi pale nilipofika huku Muhimbili, ndipo iligundulika ana tatizo la scoliosis (kibiongo).

“Daktari alinieleza ni tatizo linalowapata zaidi watoto wa kike kuliko wa kiume hasa katika umri wa miaka tisa, hata hivyo bado haijajua ni sababu zipi zinachangia hali hiyo,” anasema.

Anaongeza “Tangu amefanyiwa upasuaji hajawahi kuhisi tena maumivu makali ya mgongo kiasi cha kulazimika kumtafuta daktari amsaidie, anaendelea vizuri na shughuli zake, amerefuka vizuri, sasa yupo kidato cha tano.

UNYANYAPAA NI MKUBWA

Tecla anasimulia kwamba kabla ya kufanyiwa upasuaji huo alikabiliana na unyanyapaa mkubwa kwenye jamii iliyomzunguka, shuleni, kiasi cha kumfanya apoteze hali ya kujiamini mbele ya hadhara.

“Nilikuwa najua nina shida ya mgongo lakini sikuwa najua kwamba shida ile ilionekana wazi hadi kwenye kutembea kwangu.

“Wanafunzi wenzangu waliniambia nilikuwa natembea upande mmoja, walianza kunitania kwa kuniita majina hayo mbalimbali kwa mfano kitale, kibega, kibiongo, yalikuwa maneno makali kwangu, yaliniumiza mno,” anasimulia.

“Nilijihisi kukosa kujiamini kiasi cha kushindwa hata kuthubutu kutoka mbele ya umati kuchangia ‘debate’ (midahalo) shuleni, nilishindwa kutoka mbele kwenda kuchangia, niliogopa kwamba nitachukua ‘attention’ ya shule nzima, kuniangalia ninavyotembea, wengine wangeweza kuanza kunicheka, nilinyamaza.

Tecla akimuonesha mwandishi wa makala haya, jinsi anavyoweza kutembea mithili ya Miss Tanzania. Msichana huyo mrembo anasema anatamani siku moja kufikia ndoto hiyo baada ya kutibiwa na kupona tatizo la kibiongo lililomtesa tangu akiwa na umri wa miaka tisa. 

ALIPOTEZA TUMAINI

Tecla anaongeza “Niliporudi nyumbani kipindi cha likizo, nilimuuliza mama yangu, ‘Hivi umesahau kabisa kwamba mimi naumwa?’,... ni kitu ambacho kilikuwa kinanikosesha amani katika jamii.

Anasimulia kwamba hali ile ilikuwa inamfanya awe mwenye huzuni muda mwingi, hasa alipokuwa akifikiria juu ya ndoto yake ya kuja kuwa Miss Tanzania.

“Ni ndoto yangu ya siku nyingi, lakini nilipofikiria kuhusu mgongo wangu, vile nilivyopinda… itakuwaje kufikia kuwa Miss Tanzania, niliona wazi ni jambo ambalo halitawezekana, nilikosa raha,” anasema.

Anasema mwaka 2016 ndipo walipoanza kuhangaika hospitali mbalimbali na mamake, hatimaye walifika MOI na kutibiwa kwa upasuaji wa kibingwa.

“Tulihangaika mno, awali madaktari (kwenye hospitali zile ndogo) hawakugundua tatizo, zaidi ya kuona tu mgongo umepinda, wapo waliotueleza kwamba haliwezekani kutibika, kurudi tena kwenye hali ya kawaida, nilikata tamaa, walinisisitiza nimuombe Mungu, lisiendelee kuongezeka.

KIBIONGO NI NINI?

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Juma Magogo anasema kibiongo (scoliosis) ni kupinda kwa mgongo na kupinda huko hupelekea kukandamiza kwa baadhi ya viungo ndani ya mwili wa binadamu hasa mapafu na moyo.

‘Wenye tatizo hili huwa wanapata changamoto ya upumuaji (lakini si hii iliyopo sasa duniani), hii ni kwa sababu ya kule kukandamizwa kwa mapafu, sehemu kubwa ya mgongo inayopinda ni ile iliyo nyuma ya kifua.

“Huwa wanapata pia maumivu makali na haiwaletei picha nzuri katika jamii kutokana na kule kupinda kwao, inapelekea kujiona tofauti kidogo na jamii inayowazunguka,” anafafanua Dk. Magogo.

Daktari Bingwa huyo anasema kuna makundi matatu ya wagonjwa wenye tatizo la kibiongo (aina za kibiongo), wapo wanaozaliwa nalo, wanaolipata kipindi cha ukuaji (rika balehe) na wanaolipata kutokana na kuugua magonjwa mengine yanayohusisha misuli.

“Kwa kundi la kwanza, wakati wa uumbaji tumboni mwa mama inaweza kutokea baadhi ya pingili za mgongo kushindwa kukaa sawa na zingine au kushindwa kukaa katika ule mgawanyiko unaotakiwa.

“Kundi la rika balehe, baadhi ambao mgongo huanza kupinda lakini hadi sasa haijulikani sababu inayochangia hali hiyo kutokea ni nini, anakuwa viungo vyake vingine vipo sawa sawa lakini mgongo pekee unakunjia.

“Kundi la tatu, ‘Neuromasicular scoliosis’ yaani wanakuwa wamepata tatizo kutokana na magonjwa mengine waliyowahi kupata yanayohusisha matatizo ya misuli,” anafafanua Dk. Magogo.

TAKWIMU ZIPOJE?

Anaongeza “Hadi sasa Tanzania hakuna takwimu za Kitaifa zinazoonesha hali halisi juu ya tatizo hili, kwamba kuna wagonjwa wangapi wanaokabiliwa nalo.

“Hivi sasa nimekuwa nakusanya data kwa ajili ya kufanya tafiti wa kina kuona ugonjwa huu upo kwa ukubwa kiasi gani Tanzania, ili pia kusaidia upangaji wa matibabu kwa wagonjwa hawa.

“Takwimu zetu hapa MOI zinaonesha kwa mwezi huwa tunapokea na kutibu  wagonjwa wanne ama watano, hii ni sawa na wagonjwa 45 hadi 60 kwa mwaka,” anabainisha.

Anaongeza “Lakini kwa uhalisia tulipaswa kuwa na takriban wagonjwa 200,000 kwa mwaka wanaotibiwa tatizo hili, ambao bado hatujawafikia.

“Haya ni makadirio tunayoweza kuyapata kwa kulinganisha na takwimu za nchi nyingine… chukulia mfano takwimu za Marekani, wao wana idadi ya watu milioni 300 ambayo ni mara tano zaidi ya idadi ya watu Tanzania.

“Kwao asilimia 1.3 ya idadi yao ya watu ni sawa na wagonjwa milioni nne, ambao wanatibiwa kwa mwaka na asilimia 25 kati yao hutibiwa kwa njia ya upasuaji.

“Kwa hiyo, tukilinganisha takwimu hiyo na kwetu, maana yake ni kwamba asilimia 1.3 ya idadi ya Watanzania milioni 60 kulingana na  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hii ni sawa na wagonjwa 800,000 wanaougua ugonjwa huu.

“Tukichukua ile asilimia 25, maana yake ni wagonjwa 200,000 ambao wanahitaji upasuaji kila mwaka nchini, huku tunaita ni ‘ku-extrapolate’, yaani kuchukua data ya nchi nyingine na kulinganisha na nchini mwetu,” anafafanua.

Anaongeza “Kwa hiyo, data kamili itapatikana baada ya sisi (MOI), kuendelea kutafuta wagonjwa hawa na kuelimisha jamii, wawalete hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.

“Kwa sababu, hivi sasa tunaona na kutibu wagonjwa 40 lakini kiuhalisia tulipaswa kuwa na wagonjwa 200,000,” anasema.


WANAWAKE ZAIDI

Dk. Magogo (aliyevaa nguo ya kijani sambamba na koti jeupe pichani akijadili picha ya radiologia na wataalam wenzake wa MOI) anasema tatizo hilo huwakumba wanawake mara tano zaidi ya wanaume duniani, suala hilo nalo bado linafanyiwa tafiti kujua nini kinachosababisha.

“Hata katika idadi ya wagonjwa hawa hapa MOI wanaume wanahesabika, unaweza kukuta ni watatu hadi watano kati ya wagonjwa wote tulionao kwa mwaka.

“Tafiti zinaendelea japokuwa kuna hisia kwamba pengine linahusiana na masuala ya homoni au vinasaba kwa wanawake (wasichana), ni kama ilivyo kwa magonjwa mengine unakuta wanaume ni wengi zaidi kuliko wanawake,” anafafanua.

Anaongeza “Mara nyingi wakina mama ndiyo huwa wa kwanza kuwagundua watoto wao, kipindi wanapowaogesha, kuwanunulia nguo mpya au viatu, huhisi na kuona mabadiliko katika migongo (miili) ya watoto wao.

“Kama ameota matiti, moja linakuwa limesogea mbele kuliko jingine, au anakuwa bega moja limepanda juu kuliko jingine, au anaona kupinda kwa mgongo kama ilivyokuwa kwa Tecla.

“Au anapokuwa ameketi na wenzake yeye hujipinda zaidi, mtoto huwa mchaguzi wa viatu, mara nyingi hukataa kuvaa viatu virefu, kwa sababu anapovaa huhisi maumivu makali ya mgongo, hivyo hupendelea kununuliwa na kuvaa viatu vya chini (flat shoes),” anasema.

TIBA MAZOEZI

Daktari Bingwa huyo anasema pamoja na tiba ya upasuaji, tatizo hilo linaweza pia kutibika kwa njia ya tiba mazoezi, ikiwa litagundulika katika hatua za awali.

“Linatibika na kupona vizuri zaidi mtoto akiwa katika umri huo wa miaka tisa hadi 14, tunatumia vipimo vya CT Scan na X-ray kuangalia limefikia hatua gani, vipimo hivi hutuwezesha kuangalia mgongo kuanzia ile ‘level’ ya shingo hadi kwenye mkia.

“Kwa vipimo hivi tunaweza kujua ‘angle’ ambayo kwa hiyo tutachagua aina ya matibabu kwa mgonjwa, ‘angle’ ya kupinda ikiwa chini ya 25 mgonjwa anaweza kutibiwa kwa njia ya tiba mazoezi.

“Tunaweza kumpa muda na kumfutialia kwa kipimo maalum ambacho kinaweza kutumika hata nyumbani, shuleni, anakuwa anashika magoti na kuinama, tunamuelekeza mama, mwalimu jinsi ya kumpima ‘angle’, ikiwa itaonekana linaongezeka, anamrudisha kwetu.

“Lakini ikiwa kuanzia 60 na kuendelea hapo haiwezekani tena kutibu kwa mazoezi, huhitaji upasuaji, ili kuzuia kuendelea kupinda kwa mgongo wake,” anasema.

Anaongeza “Kwa sababu asipofanya upasuaji anaendelea kuwa na maumivu, anaathirika kisaikolojia, anazidi kunyanyapaliwa, anashindwa kujiamini kuingia kwenye mahusiano, hususan wasichana wanaathiriwa mno kisaikolojia na tatizo hili.

Anasema kisayansi mgongo utaendelea kupinda, moyo na mapafu yatazidi kukandamizwa, ikiwa mapafu ndiyo yaliyokandamizwa atazidi kupata shida ya upumuaji, ataishi na maumivu makali na ikiwa moyo utakandamizwa kuna uwezekano mkubwa kwa mgonjwa kupoteza maisha.

Tecla na mama yake wakiwa na nyuso za furaha walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni.

NDOTO ZANGU ZITATIMIA

Tecla ambaye ni msichana mrembo na anayejiamini, anasimulia “‘Soon after’… nilivyofanyiwa upasuaji MOI, hata shule yangu wenyewe wanaweza kuwa shahidi, nilianza kuhudhuria ‘debate’, nilianza kujitolea kwa sababu ‘nili-gain ile confidence’ yangu tena,” anasimulia huku akitabasamu.

Anaongeza “Nimepata tena tumaini kuifikia ndoto yangu ya Umiss Tanzania, sasa nipo kidato cha tano, nitasoma kwa bidii, niweze kufanya vema katika masomo yangu.

“Ningependa kuwaambia watu kwamba tatizo hili linatibika na kupona kabisa, wasikae nyumbani, watoto nao wawahishwe hospitalini, wasifichwe, wasitengwe, wasinyanyapaliwe.

“Hata kwenye hii MOI Marathon nawaomba Watanzania, wadau wajitokeze kwa wingi kuchangia ili kuweza kuokoa maisha, kwa sababu mtoto akiwa na tatizo hili kuna changamoto nyingi, kiasi cha kujiona hana thamani kwenye jamii, inashusha kipaji chake, alichojaliwa,” anasisitiza Tecla.

1 Maoni

Chapisha Maoni

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement