Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Asilimia 80 ya wananchi wanaojitokeza
kuchangia damu ndani au nje {kwenye kampeni maalum za uchangiaji damu zinazofanywa
na..} Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala {RRH}, hukimbia/hutelekeza majibu
yao.
Yameelezwa hayo na Mtaalamu wa
Kitengo cha Maabara Huduma za Damu Mwananyamala RRH, Loveness Sunda katika
mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA
BLOG yaliyofanyika wakati wa maonesho ya hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya
Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru.
Amesema Mwananyamala RRH ni
miongoni mwa vituo vya uchangiaji na ukusanyaji damu salama Kanda ya Mashariki,
Wilaya ya Kinondoni, kiasi cha damu kinachokusanywa na kituo hicho husaidia pia
kuokoa maisha ya wagonjwa kwenye hospitali nyinginezo.
Ametaja baadhi ya hospitali
wanazozihudumia pamoja na Mwananyamala yenyewe ni Kairuki, Saifee, TMJ,
Kinondoni Hospitali, Kituo cha Afya Sisa na vituo vingine mbalimbali.
“Wengi {wanaojitokeza
kuchangia damu} wanaogopa kuja kupokea majibu yao, wanayakimbia, tunadhani
wengi huhofia kuja kuchukua pale wanapofikiri kwamba endapo si mazuri
itakuwaje,” amesema.
Ameongeza "Wakija kwa mara nyingi kuchangia damu kwa sababu anakuwa na ile namba yake kwenye 'data base' yetu tunafuatilia 'status' yake kama majibu yake ni mazuri tunaendelea naye kama si mazuri tunamuelekeza nini cha kufanya.
Loveness amesema pamoja na hayo, kiasi kingi cha damu huchangwa na kundi la wanafunzi ambao wengi wao hufuatwa ma-shuleni/vyuoni na kwamba kwa asilimia 90 damu zao huwa salama.
“Yaani tukienda kukusanya damu
kutoka kwa wanafunzi tuna uhakika kwamba kama tumekusanya chupa 100 basi chupa
zipatazo 90 huwa ni salama kwa matumizi/kuokoa maisha,” amedokeza.
Amesema kiasi cha damu
kinachohitajika kutosheleza mahitaji ya hospitali hiyo na nyinginezo ambazo
wanazipatia ni wastani wa chupa 500 hadi 550 kwa mwezi hata hivyo kiasi
kinachopatikana ni chupa 300 hadi 350 pekee.
“Idadi hii ni sawa na kiwango
cha asilimia 60 tu ya mahitaji yetu, hatujawahi kufikia kiwango cha asilimia
100,” amebainisha Ofisa huyo kutoka Kitengo cha Maabara, Huduma za Damu
Mwananyamala RRH.
Ametoa rai “Hivyo bado
tunaendelea kuhimiza jamii, kujitokeza kuchangia damu kwani mahitaji ni makubwa
hasa kwa kundi la wajawazito wanaokuja kujifungua, majeruhi wa ajali mbalimbali
hasa za barabarani na wagonjwa wengine wanaolazwa hospitalini.
Hospitali hiyo iliyoanzishwa
mnamo mwaka 1973 kama kliniki hususan ya masuala ya uzazi ilifanya maonesho
hayo {Desemba 6 – 8, 2021} ili kuwaonesha wananchi huduma zake wanazozitekeleza
katika idara zipatazo 15 walizonazo.
Wananchi walipata fursa ya
kuchunguza afya zao na kupewa ushauri bila malipo huku wengine wakifika kupata chanjo
za UVIKO – 19 kwenye maonesho hayo.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo
kwa mwaka huu inasema ‘Miaka 60 ya Uhuru Tanzania Imara, Kazi Iendelee.
Chapisha Maoni