Na Veronica Mrema
Upo uwezekano mkubwa wa beseni la kumuogeshea mtoto kugeuka ‘kiota’ {chanzo} cha kupata maambukizi ya U.T.I {Urinary Track
Infection} mara kwa mara na hali hiyo ya kujirudia rudia kwa U.T.I kunaweza
kusababisha magonjwa ya figo, hata hivyo jamii haina uelewa juu ya hili.
Hata kitendo cha
kumuacha mtoto na nepi/‘pampasi’ kwa muda mrefu
kinamuweka kwenye hatari ya kupata U.T.I mara kwa mara, endapo hujisaidia na
kukaa kwa muda mwingi pasipo kubadilishwa na kusafishwa vema.
U.T.I ni ugonjwa
unaosababishwa na maambukizi ya bakteria ambaye vimelea vyake hushambulia mfumo
wa mkojo hususan kibofu, mrija wa urethra na figo zenyewe.
Magonjwa ya figo nayo
yamegawanyika katika makundi makuu mawili, yale ambayo hutokea kwa dharura
{acute kidney failure} na yale ya kudumu {chronic kidney failure}, vipo
vyanzo/sababu nyinginezo pia zinazoweza kusababisha magonjwa haya.
Yameelezwa hayo na Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Profesa Francis Furia
alipozungumza katika mahojiano maalum na MATUKIO
NA MAISHA BLOG hivi karibuni, yaliyoangazia magonjwa ya figo kwa watoto.
“Jambo la msingi linalopaswa
kuepukwa hapa ni kuto-kumuogesha mtoto akiwa amekalishwa ndani ya maji badala
yake aogeshwe akiwa amesimama wima,” amesisitiza Prof. Furia.
Amefafanua zaidi kwamba “Wadudu
wanaosababisha maambukizi ya bakteria kwenye njia ya mkojo wengi wanapatikana
kwenye kinyesi, kwa hiyo kinyesi kikiingia kwenye njia ya mkojo, wale wadudu
watasababisha U.T.I.
“Kwa hiyo, mtoto akikaa na
nguo/nepi/‘pampasi’ ambayo imeshika kinyesi kwa muda mrefu kuna uwezekano kile
kinyesi kikaingia njia ya mkojo kikasababisha maambukizi ya U.T.I, usafi wa
mtoto ni muhimu,” amesema.
Pamoja na hayo, Prof. Furia amesisitiza kwamba “Watoto kupata U.T.I mara kwa mara cha kwanza, kuna uwezekano wana matatizo ya kimaumbile {congenital abnormalities} katika mfumo wa mkojo.
“Njia ya mkojo imeumbwa kwa
ajili ya kuhakikisha kwamba mkojo ukitoka kwenye figo unaenda moja kwa moja
kwenye kibofu kisha unatoka nje. Kama kuna kitu chochote kinazuia mkojo usitoke
nje, mkojo ukikaa kwenye kibofu kwa muda mrefu unasababisha maambukizi ya
bakteria wanaoishi pale wasababishe U.T.I.
Amefafanua “Kwa hiyo kila
mtoto anapopata U.T.I yale maambukizi ya bakteria huwa yanaathiri figo,
zinakuwa na makovu, yale makovu yanaharibu utendaji kazi wa figo kwa muda
mrefu, hivyo kupata maambukizi ya bakteria kwenye njia ya mkojo mara kwa mara
husababisha figo ziharibike.
Prof. Furia ambaye pia ni Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Figo kwa Watoto, Hospitali ya Taifa Muhimbili {MNH}, amesema
kwenye kliniki zao huona watoto waliozaliwa na matatizo ya figo na wengine
waliyapata katika kipindi cha ukuaji, kutokana na kuugua magonjwa mengine kama
vile malaria.
“Kwa wastani kliniki kwa siku
wanakuja wagonjwa wapatao 15 hadi 20, kuanzia wachanga hadi miaka 16, si wapya
hawa wanakuja kliniki mara kwa mara, wapo wa miaka 10 iliyopita tunaendelea
kuwaona, wengine walianza kliniki wakiwa shule ya msingi na sasa wamefika vyuo
vikuu,” amebainisha.
Chapisha Maoni