Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema - Dar es Salaam

Mabaraza yote ya kitaaluma kwenye sekta ya afya yameonywa, endapo hayatawajibika ipasavyo katika kutimiza wajibu wake wa kusimamia mienendo na utendaji kazi wa wataalamu  wanaowasimamia, watawajibishwa.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeyaagiza mabaraza hayo yote kuhakikisha watendaji wake wanapita mara kwa mara kukagua watumishi wa sekta hiyo kwenye vituo vyao vya kazi.

Naibu Waziri, Dkt. Godwin Mollel amesisitiza hilo mapema leo alipofanya ziara yake ya kawaida ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala ambako amezungumza na watumishi ikiwa pia ni siku chache kukiwa na taarifa zilizosambaa mitandaoni baadhi ya wananchi wakidai kutokuhudumiwa vema hospitalini hapo.

“Leo nimekuja kwa ziara yangu ya kawaida hapa, lakini pia imekutana na hili la malalamiko ya mtandaoni, ambalo kimsingi tayari Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima alishalitolea maelekezo, tayari tuna baadhi ya taarifa lakini sitazitoa tunawaacha kwanza wataalamu wakamilishe uchunguzi na majumuisho ya kile walichokibaini.

“Lakini tunayo mabaraza ya kitaaluma, kikubwa sisi na ‘very strongly/tunasisitiza’ tunaona mabaraza haya ni wakati mwafaka wa kufanya kazi yao.

“Yanapotokea mambo yanayohusu taaluma halafu wanasubiri mpaka Waziri au Naibu Waziri aje ashughulikie kwa sababu wapo, wasifikiri tutaishia kwa yule aliyefanya makosa hayo ya kitaaluma, tutakukamata wewe ambaye ni baraza la kitaaluma ambaye hujafanya kazi yako,” amesema.

Dkt. Mollel amesema kwa muda mrefu sasa imezoeleka kwamba panatokea matatizo, analengwa peke yake yule aliyesababisha tatizo.

“Lakini kwa muelekeo na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Gwajima ni kwamba wewe uliyetakiwa kumsimamia huyo mtu hujamsimamia, unawajibika.

“Maana yake ni kwamba si tu tutaenda kusema ni daktari fulani, muuguzi fulani aliyefanya kosa, tunakuja kusema ni muuguzi huyu aliytefanya kosa, nani alitakiwa amsimamie, ni in-charge wake wa wodi, anawajibika, alitakiwa kumsimamia nesi mkuu wa hospitali, anawajibika.

“Baraza la ma-nesi, madaktari mlikuwa mnafanya nini, wasingojee mambo yatokee ndiyo waende wakafanye mambo, wanatakiwa kila siku kazi yao kuzunguka kuangalia yale makosa hayatokei,” ameagiza.

Amesema kitakachowanusuru endapo malalamiko yatajitokeza ni ukaguzi ambao timu ya Wizarani itafanya na kujihakikishia kwamba mabaraza hayo yalitimiza wajibu wake.

“Tunataka tukisoma daftari la wageni tuone uliwahi kuja, kufanya nini na kuelekeza nini, tukikuta umefanya maana yake huyu mtu ameamua kukengeuka lakini wewe umesema.

Ameongeza “Lakini tukikuta hufanyi kazi yako na kuna makosa na wewe ni mmoja wapo wa mtuhumiwa wa eneo hilo, kama tunavyosema kuna wizi wa madawa tunashindwa kuelewa inakuwaje wizi wa dawa unatokeawakati kila mkoa kuna kamati ya ulinzi na usalama, kila mkoa kuna viongozi ... RMO {Mganga Mkuu wa Mkoa},

“Wakati wizarani wanatoka viongozi wa wizara wanapita kukagua lakini hawaoni dawa zimeibwa wakati kuna viongozi wamezunguka.

“Sisi tunataka kila mtu acheze namba yake, leo nimekuja hapa, sijaja kumwambia yeyote umekosea, hii ni mara ya pili {kuja}.

“Tulikuja tukaona matatizo akabadilishwa mganga mfawidhi, tumerudi tena kutoa mwelekeo ili atakayekosea hatatulaumu, atakuwa ameleekezwa na hajatekelezwa.

Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema watumishi wa sekta ya afya wanafanya kazi kubwa na nzuri isipokuwa tu changamoto ya uwepo wa wachache ambao hawatimizi wajibu wao sawa sawa.

“Hivi sasa bado kuna UVIKO – 19 ulimwenguni lakini nchi yetu imetulia ni juhudui za hawa watu. Kuna nchi wanafunzi hawajaenda shule miaka miwili sasa, watu wanakufa, Tanzania hatujawahi kufungiwa ndani, bado tupo salama,” amesema.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mollel akiambatana na maafisa wengine wa Wizarani akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Tiba, wametembelea wodi kadhaa ikiwamo ya watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalum, wodi ya wajawazito na chumba cha radiolojia.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benele {pichani} amesema hospitali hiyo imeendelea kuimarisha huduma zake mbalimbali lengo ikiwa wananchi wazipate kwa wakati.

“Kipindi cha Julai – Novemba 2021 tumehudumia wagonjwa 209,867, wakina mama waliojifungua ni 2,743, watoto hai ni 2,712 na sasa hospitali inatoa huduma za kibingwa katika idara ya upasuaji, pua, masikio na koo, magonjwa ya ndani, watoto, magonjwa ya wanawake, magonjwa ya ngozi, kinywa na meno kwa watoto,” amebainisha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement