Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Janga la UVIKO – 19/COVID – 19 kwa kiwango kikubwa liliifunga mipaka ya dunia, kati ya Taifa moja na jingine, hususan kipindi cha mwishoni mwa Desemba, 2019 na 2020 ambapo maambukizi ya virusi vya CORONA yaliporipotiwa kusambaa kwa kasi ulimwenguni mwote.

Tanzania ikaripoti wimbi la kwanza, pili na tatu lakini haikufunga mipaka yake moja kwa moja kama ambavyo mataifa mengine yalifanya.i

Hvi sasa tayari baadhi ya nchi ulimwenguni na hata Barani, Afrika kumeripotiwa wimbi la nne la maambukizi ya kirusi hicho ambacho tangu Desemba, 2019 kufikia sasa tayari kimesababisha vifo vya mamilioni ya watu.

Kutokana na mataifa kufunga mipaka yake {hususan kipindi cha wimbi la kwanza hadi la tatu} kwa mfano India ambako ni kimbilio la watu wengi wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo, huenda huko kwa matibabu,

ililazimu wagonjwa hao kutafuta mbadala wanakoweza kwenda kutibiwa kwa viwango vile vile vya ubingwa kama wa India na hapo wengi walikimbilia nchini Tanzania katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete {JKCI}.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG anasema katika kipindi hiki ambacho CORONA bado inaitikisa dunia, taasisi hiyo imetoa huduma kwa idadi kubwa ya wagonjwa kuliko kipindi kingine chochote tangu mwaka 2015 ilipoanzishwa.

Anasema kabla ya janga la UVIKO – 19 vilikuwa vinakuja vikundi vipatavyo 10 vya kutibu watu wazima na watoto lakini kutokana na janga hilo idadi hiyo ya vikundi haikufikia kwa mwaka huu.

“UVIKO – 19 ulipotokea hivi vyote havikuweza kuja, lakini kila kitu kinakuja kwa uzuri na ubaya wake, kwa sababu hakuna kipindi sisi {JKCI} tumefanya oparesheni nyingi kama cha UVIKO – 19.

“.., kwa sababu hata wale waliokuwa na uwezo wa kusafiri kwenda nje, familia zenye uwezo wa kati na juu wote ilibidi waje hapa kufanyiwa.

Anaongeza “Kama nilivyokuambia hapo awali, ukitazama oparesheni zetu zote jumla za mwaka huu tulikusudia wagonjwa 1950, kwa kutumia tundu dogo tumefanya karibu 1400 ukitizama kifua kufungua takriban 402/3 na bado tuna wiki mbili hizi, tumefikia wagonjwa 4000.

“Kwa hiyo hata kwa changamoto zote hizi imetufanya sisi tuweze kufanya oparesheni nyingi zaidi kwa madaktari wetu wazawa, tumepata wagonjwa wengi wa nje kuliko kipindi chochote kile kuanzia Zambia, DRC Kongo, Zimbambwe, Kenya, Uganda na wiki ijayo tunapokea wagonjwa sita watatu kutoka Somalia na watatu kutoka Kenya,” anabainisha.

MIAKA SITA YA KAZI

Anafafanua “Ni miaka sita sasa tangu Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete {JKCI}, ilipoanza rasmi kufanya kazi kama taasisi kamili inayojitegemea, kwa mujibu wa Sheria. 

"Kabla ya hapo, taasisi hiyo ilikuwa ikifanya kazi kama kitengo cha matibabu ya moyo, chini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili {MNH}.

Prof. Janabi anasema tangu walipoanza kutoa huduma mwaka hadi mwaka wamekuwa wakiona mafanikio kwenye hali ya utoaji huduma ndani ya taasisi hiyo.

Anasema taasisi hiyo hufanya uchunguzi wa kibingwa wa magonjwa ya moyo pamoja na matibabu yake kwa watoto na watu wazima na kwamba wagonjwa wanaoonwa ni wa ndani ya nchi na hata wanaotoka nje ya nchi.

Anasema kiwango cha uwezo wa wataalamu wa ndani ya taasisi hiyo, (wazalendo) nacho kimekuwa kikizidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, kwani wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na wataalamu wenzao kutoka nchi mbalimbali.

Anatoa mfano wa kambi ya matibabu iliyofanyika ndani ya hospitali hiyo kuanzia Desemba 10 hadi 16, mwaka huu ambapo walishirikiana na wataalamu wenzao kutoka Ufalme wa Kiarabu wa Saudia, anasema imekuwa ya mafanikio makubwa.

“Ufalme wa kiarabu wa Saudia, tunafahamiana nao kwa miaka mitatu sasa, hii ni safari yao ya pili kutokana na UVIKO - 19 walishindwa kuja (huwa wanakuja nchini mara mbili kwa mwaka, awamu hii wamekuja mara moja, 35 wakiwamo watumishi madaktari, wauguzi watoa dawa za usingizi,

“Wengine si wataalamu wa afya ni wa utawala, utaalamu wao mkubwa zaidi ni kwenye upasuaji mgumu wa watoto waliozaliwa na mattzio ya moyo,” anasema.

Anabainisha “Hatua ya kwanza tulitazama karibu watoto 100 kuwapima nani ana tatizo la kweli na anahitaji upasuaji, tulipata watoto 36 ambao wapo katika hali za kuweza kufanyiwa upasuaji wa moyo.

“Walichaguliwa watoto 34 na asilimia 60 kati yao wa kiume na 40 wa kike, wana miezi sita hadi miaka 12 wana uzito kati ya kg 4 hadi 32 ni wadogo, tilivyotizama hali zao upumuaji wapo ambao kiwango kilikuwa wastani wa asilimia 70 na wengine chini zaidi.

“Hawa, wamezaliwa na matatizo ya moyo tangu siku ya kwanza, hivyo, siku nne za kwanza tuliweza kufanikiwa kuwafanyia watoto 23 na wengi wao katika saa 24 hadi 72 walikuwa tayari wametoka chumba cha wagonjwa mahututi, wameruhusiwa kuingia ma-wodini,” anasema.

Anasema katika idadi ya wote hao waliohudumiwa, mmoja alipoteza maisha, hali hiyo ni kawaida ya upasuaji mkubwa kama huo unaofanywa.

“Mafanikio ni makubwa kwa sababu ukitazama namba yote hiyo 34 kupoteza mtoto mmoja, si kama sisi watu wa tiba tunakipenda (kifo chochote kitokee), lakini kufanya sisi ni kitu kimoja na mipango ya Mungu ni kitu kingine.

Anasema kuwatibu watoto hao ni gharama kubwa na kwamba wengi wao ni wale wanaotoka kwenye familia dunia,ambazo hazijiwezi (kiuchumi).

“… wamekuja kwetu hapa, hawa wenzetu walikuja na vifaa vyote vinavyohitajika, waliokuwa na matundu yamezibwa, ambao mishipa ya damu ilikuwa imekaa sehemu ambazo si mahala pake, wamerekebishwa.

“Tungefanya wenyewe (ndani ya nchi) gharama ni kama milioni 400 za kitanzania wangeenda nje ya nchi milioni 535 za kitanzania kwa hizi siku saba walizokuwepo hapa tumeokoa zaidi ya Sh milioni  222,” anabainisha.

Anaongeza “Mbali na kuokoa hawa watoto, lakini ukitazama kwenye hili kundi la madaktari na wauguzi na wa chumba mahututi ni kwamba kuna elimu kubwa tumejifundisha kwa sababu kuna vitu wenzetu wapo mbele.

Anasema kablaya kambi hiyo tayari wao wataalamu wa ndani JKCI walikuwa wameshawafanyia upasuaji jumla ya watoto 204 tangu januari na kwamba bado kuna watoto wengine wapatao 500 ambao wanasubiri kufanyiwa upasuaji.

“Hivyo, tumepata ujuzi zaidi, wakiondoka sisi tutaendelea {wenyewe} kutoa huduma kwa watoto wetu,” anasisitiza Prof. Janabi.

Anaongeza “Hawa wageni {saudia} tulichokubaliana nao leo kama hakuna janga la uviko mwakani taratibu zao kuja mara mbili kwa mwaka, mwanzo na mwishoni mwa mwaka.

Anasema ana imani kubwa kwamba huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo nchini zitazidi kuimarika na kutanuliwa zaidi kufikia idadi kubwa ya wananchi.

UPANUZI TIBA YA MOYO

“Lengo la kufungua sehemu nyingine ya matibabu tayari limeanza Dodoma (Hospitali ya Benjamin Mkapa) wanafanya upasuaji wa tundu dogo lakini vyote ni hatua sisi tupo hapa mwaka wa sita, nina uhakika Benjamin Mkapa itakuwa mbali Bugando, KCMC na Mbeya.

“… Lakini naomba kuliweka hili sawa sawa, kufika mpaka hizo hatua si kwamba unahitaji vifaa tu na wataalamu, kipindi hiki sisi na serikali tumejikita kusomesha wengi zaidi kuna baadhi waliosoma hapa wapo Dodoma,

“Nina uhakika baada ya muda si mrefu tutaanza kuona mafanikio makubwa zaidi, wameshaanza .. nina uhakika BMH, Mbeya {MZRH} na KCMC wakija kuanzisha wataweza kufanya vizuri zaidi kwa sababu yale makosa au changamoto tulizopata sisi 2015 – 17 tume-share na wenzetu.

“Nina uhakika si kwamba hawatapata changamoto lakini zitakuwa tofauti kidogo na zile tulizopata sisi mwanzo, nina uhakika siku za usoni tanzania itakuwa tegemezi kubwa kwa matibabu ya moyo afrika. Kwa sababu hizo dalili tumeshaziona.

MATIBABU KIDIGITALI

Desemba 17, 2021 JKCI iliandika historia mpya katika matibabu ya kibingwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, kwa mara ya kwanza ilifanikisha upasuaji kwa tundu dogo kupitia mawasiliano ya kidigitali kwenye satellite.

Kwa tiba hiyo mtandao/telemedicine wataalamu waliweza kumtibu mwanaume mmoja aliyekuwa anakabiliwa na tatizo la kuziba kwa mshipa wa damu kwenye moyo.

Mabingwa hao wa JKCI walifanikisha kuzibua mshipa huo ulioziba kwa asilimia 99 kwa kushirikiana na wataalamu mabingwa wenzao kutoka Shirika la madaktari Afrika waliopo Hospitali ya Central jimbo la Virginia nchini Marekani.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Peter Kisenge anasema upasuaji huo mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI) ulichukua takriban saa moja kukamilika.

Anasema upasuaji huo ulifanywa kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) Carto 3 System 3d & Mapping Electrophysiology system.

“Tulikuwa wakipokea maelekezo moja kwa moja kupitia mtandao wa zoom kutoka kwa wenzao Marekani hatimaye kufanikiwa kuzibua mshipa huu,” anabainisha.

Anasisitiza “Upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu kwa njia ya tundu dogo umekuwa ukifanyika ndani ya taasisi hiyo tangu 2014 na wataalamu hao wa Madaktari Africa ndiyo ambao walikuwa wakiwaelekeza na kuwasimamia hadi tumeweza kufanya upasuaji huu wao wenyewe.

“Hata leo wametuelekeza kwa njia ya mtandao jinsi ya kufungua mshipa huu ambao ulikuwa umeziba kwa kiasi kikubwa kwani wenzetu hawa wana utaalamu mkubwa zaidi kuliko sisi.

Anasema kwa kupata maarifa hayo kupitia mifumo ya kidigitali endapo atatokea mgonjwa mwengine mwenye tatizo kama hilo sasa wanao uwezo wa kumfanyia upasuaji huo.

“Miaka ya nyuma upasuaji kama huo ulikuwa unafanyika nje ya nchi, lakini kutokana na kuwepo kwa vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu wa kutosha hivi sasa huduma kama hizo zinatolewa hapa JKCI,” anasisitiza.

Dkt. Kisenge anaongeza “Kama mgonjwa huyu angetibiwa nje ya nchi gharama za matibabu zingekuwa ni zaidi ya shilingi milioni 20 lakini mgonjwa huyu ametibiwa hapa nchini kwa gharama ya shilingi milioni sita.

“Kwa kuwa mgonjwa huyu amejisajili na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) gharama zote za matibabu zimelipwa na bima hii,” anabainisha huku akiwasihi wananchi kujiunga na bima ya afya.

UPASUAJI WENYEWE

“Kuna njia mbili za kufanikisha upasuaji wa aina hii, ambazo ni mshipa wa kwenye paja au mkononi ambako vifaa maalum hupitishwa ili kuweza kuufikia moyo,” anasema Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Khuzeima Khanbhai.

Anaongeza “Kwa kuwa uzibuaji huu ulikuwa mgumu tulitumia njia ya kwenye paja tukapitisha vifaa na hatimaye kuzibua mshipa huo uliokuwa umeziba.

“Tunapofanya upasuaji wa aina hii mgonjwa huwa macho, tunazungumza naye… anakuwa amechomwa sindano ya ganzi katika eneo husika pekee {ambako kifaa maalum huingizwa kwenda kwenye moyo}.

“.., hii inatusaidia kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mgonjwa,” anasisitiza Dkt. Khanbai huku akibainisha kwamba kwa wiki wagonjwa 50 hadi 60 huchunguzwa tatizo hilo ndani ya taasisi hiyo..

“Kwa mwaka huu huyu {aliyetibiwa kwa njia ya kidigitali} ni mgonjwa wa 1499, kuna wagonjwa ambao wanakuja kama wana tatizo la gesi tumboni lakini baada ya vipimo wanaonekana mishipa yao ya damu ya moyo imeziba,” anabainisha Dkt. Khuzeima.

‘MATUNDA’ YA UWEKEZAJI

Prof. Janabi anasema kufanikisha upasuaji huo ni sehemu ya ‘mavuno ya matunda’ ya uwekezaji mkubwa uliofanywa ba Serikali ndani ya taasisi hiyo.

“Madaktari Africa wamekuwa wakija kufanya basi kambi maalum za upasuaji mdogo ambao ni mgumu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo lakini kutokana na tatizo la Ugonjwa wa UVIKO- 19 madaktari hao wameshindwa kuja nchini.

“Lakini kuwepo kwa mtambo wa mpya wa Cathlab kumewasaidia kupata maelekezo kutoka kwa wataalamu hawa wa nje ya nchi wenye utaalamu wa juu zaidi ya jinsi ya kufanya upasuaji ambao wataalamu waliopo nchini hawawezi kuufanya.

“Ninaishukuru sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa tiba ya magonjwa ya moyo uliofanyika katika taasisi hii.

KUHUSU CHANJO YA CORONA

Pamoja na hayo, Prof. Janabi anahimiza Watanzania kuendelea kujitokeza kupata chanjo dhidi ya maambukizi ya virusi vya CORONA, akisisitiza kwamba zimechunguzwa na kuthibitishwa ubora, usalama na ufanisi wake katika kukabiliana na janga hilo la kidunia.

“Nkilinganisha na mwanzo tulipoanza, mwamko upo kiasi, nimeona asilimia 62 wameenda kupata chanjo yao ya pili, ni hatua nzuri lakini bado nihimize watanzania tuwendelee kwenda kuchanja.

“Mimi nimechanja, sina tatizo lolote, chanjo zote zilizoletwa nchini ni salama, wakachanje,” ametoa rai.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement