Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Wastani wa watoto 34 kati ya 1,000 {prevalence} wanakabiliwa na matatizo ya kuharibika kwa ‘valve’ za {milango ya} moyo, utafiti mpya nchini umedokeza.

Uchafuzi wa mazingira/hewa na ukosefu wa maji safi ni miongoni mwa visababishi {risk factors} vilivyotajwa/vinavyodhaniwa kuongeza uwezekano tatizo hilo kutokea.

Utafiti huo umefanywa na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete {JKCI} na matokeo yake kuchapwa ndani ya Jarida la Kisayansi la BMC la Uingereza Desemba 20, 2021.

Watafiti hao wamedokeza pia, watoto wenye umri wa miaka tisa na kuendelea na wale waliopata maambukizi katika mfumo wa hewa {kikohozi/mafua} wapo kwenye uwezekano mkubwa kupata tatizo hilo linalofahamika kitaalamu Rheumatic Heart Disease {RHD}.

Wakiongozwa na mtafiti kiongozi, Daktari Bingwa wa Watoto JKCI, Palvina Kazahura, watafiti hao wamefafanua kwamba “Wakati wa utafiti huo walibaini watoto wenye umri wa kiaka tisa na kuendelea waliohusishwa kwenye utafiti huo walikuwa na hatari zaidi ya kuwa na matatizo haya kuliko walio na umri huo.

“Aidha, watoto waliopata maambukizi mfumo wa hewa {kikohozi/mafua} zaidi ya miezi mitatu kabla ya utafiti huo, walikuwa na uwezekano mkubwa kuwa na matatizo hayo ikilinganishwa na wale ambao hawakuugua.

Utafiti huo ulifanyika kipindi cha Februari hadi May, 2019 katika shule ya msingi Muhimbili {Manispaa ya Ilala} na Shule ya Msingi Mjimpya {Manispaa ya Temeke}, zote za Dar es Salaam.

“Jumla ya wanafunzi 1,023 walihusishwa katika utafiti na 949 kati ya hao walichunguzwa kwa kipimo cha echocardiography.

"Asilimia 57 ni wasichana na wote {wanafunzi} walikuwa na umri wa kati ya miaka 7 hadi 18 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba,” wameeleza watafiti hao.

Watafiti wamesisitiza, wanafunzi hao walipatiwa maswali na fomu za ridhaa ambazo zilisainiwa na wazazi wao kukubali wahusishwe kwenye utafiti huo na wanafunzi wote hawakuwahi kuripotiwa kuwa na matatizo ya ‘valve’ za moyo hapo kabla ya utafiti kufanyika.

“Lengo la utafiti huu ilikuwa kuwabaini mapema ili wapatiwe matibabu ya mapema kwani ni tatizo linalotibika,” wamesema.

Pedro Pallangyo ni miongoni mwa watafiti waliohusika ameieleza MATUKIO NA MAISHA BLOG kwamba kwa kiwango cha asilimia 100 usafi wa mazingira una nafasi kubwa katika kulinda usalama wa afya ya moyo wa binadamu.

“Unakuta vyoo vichafu, mitaro inakatiza kwenye makazi ya watu, wengine hawapigi vema mswaki, kuoga ni kizungumkuti, madampo yapo jirani na makazi ya watu.

“Magonjwa ya ‘valve’ kama hii RHD yanatokana na bakteria kuingia kwenye mfumo wa hewa na kuzaliana kisha kwenda kenye ‘valve’ na kuziathiri.

“Ndiyo maana magonjwa haya kamwe huwezi kuyasikia kwenye nchi zilizoendelea au kwa hapa Dar es Salaam, huwezi kuyasikia maeneo kama Masaki bali Manzese, Tandika, Tandale na kwengineko kama huko.

Ameongeza “Uchafuzi wa hali ya hewa pia huchangia uwezekano mkubwa wa magonjwa haya kutokea.

Katika chapisho hilo, watafiti hao wameongeza “Maambukizi katika mfumo wa hewa, zipo tafiti chache zinazothibitisha uhusiano wake na changamoto ya ukosefu maji safi pamoja na kutokunawa mikono ipasavyo kwa maji safi tiririka na sabuni.

“Kutakasa mikono hupunguza uwezekano wa maambukizi ya vijidudu vinavyoweza kushambulia mfumo wa hewa, imeripotiwa pia nchini Pakistan vyoo duni, ukosefu wa maji safi huongeza uwezekano wa magonjwa ya RHD.

“Hata Yugoslavia ni sawa sawa na kile tulichobaini kwenye utafiti wetu {JKCI}, upatikanaji maji safi ya uhakika na huduma za uchunguzi ni muhimu katika kuzuia tatizo hili,” wamesisitiza watafiti hao.

Watafiti hao wamesisitiza "Mazingira duni ya makaazi, makaazi yasiyopangiliwa vema na ujenzi wa nyumba karibu karibu huongeza uwezekano wa magonjwa ya mfumo wa hewa na mengineyo kwani mzunguko wa hewa huwa mdogo mno.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement