Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Tafiti ni eneo muhimu katika kuimarisha afya ya binadamu, upo mfano hai na halisi wakati wa janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu {UVIKO – 19}, lilipozuka mwishoni mwa Desemba, 2019.

Watafiti duniani 'walikesha’ wakipambana kutafuta ufumbuzi wa kisayansi kukabili janga hilo lililosambaa kwa kasi na kuathiri idadi kubwa ya watu.

Kadhalika kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani, shinikizo la damu, kisukari, kiharusi, moyo na mengineyo yanayosababisha vifo vingi kila mwaka na kuathiri wengi, tafiti mbalimbali zimekuwa zikifanyika.

Tafiti nyingi zimekuwa zikilenga kuongeza kasi ya kupambana na magonjwa hayo kwa kuzuia watu wasiugue pamoja na kuimarisha matibabu kwa ajili ya wale wanaougua ili waweze kuishi vema licha ya matatizo yao.

“Nchi yoyote ile ulimwenguni ikiwa inahitaji kupata maendeleo kwa ajili ya watu wake haina budi kuwekeza ipasavyo kwenye tafiti za ndani katika sekta zake mbalimbali.

“Tafiti za ndani zina mchango mkubwa katika kusaidia ustawi wa nchi husika vile vile zinaweza kutoa mchango chanya kwa dunia nzima katika kuboresha mambo mengi,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete {JKCI}, Profesa Mohamed Janabi katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG hivi karibuni.

Magonjwa ya moyo ni kati ya magonjwa yasiyoambukiza {sugu} yanayoshika kasi na kugharimu uhai wa watu wengi, yakisababisha vifo vipatavyo milioni 18 kila mwaka duniani, kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani {WHO}.

Tanzania nayo ipo kwenye mapambano dhidi ya magonjwa hayo, miaka saba iliyopita ilianzia taasisi hiyo kwa mujibu wa Sheria ili kuwekeza na kuimarisha tafiti, uchunguzi na tiba ya moyo kwa raia wake, Afrika Mashariki, Afrika na hata dunia.

KITENGO MAHUSUSI

Anaongeza “JKCI tunatambua umuhimu wa tafiti katika kuimarisha uchunguzi, tiba na kinga dhidi ya magonjwa ya moyo.

"Hivyo hili ni eneo ambalo tumelipa kipaumbele ipasavyo ndani ya taasisi na limewekewa bajeti yake inayojitegemea kabisa, huwa hatuigusi / hatuibadilishii matumizi yake.

Takwimu za JKCI zinaeleza tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa hadi kufikia sasa tayari imefanya tafiti 50 za magonjwa ya moyo kati ya hizo, upo utafiti mpya wa hivi karibuni ambao ‘umeifumbua macho’ dunia katika magonjwa ya moyo.

“Utafiti huo uliangazia viashiria vya magonjwa ya moyo kwa ndugu wa wagonjwa {wanaohudumia watu wenye magonjwa hayo} kwa kimombo tunaita ‘Care Givers’,” anabainisha Prof. Janabi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na mwandishi mkuu wa utafiti huo JKCI, Pedro Pallangyo {pichani} akiwa na tuzo hiyo.

Anasema walilenga kuangalia viashiria vya magonjwa ya moyo kwa ‘Care Givers’, kwani magonjwa hayo yamehusishwa mno na tabia mbalimbali ambazo nyingi kati yake zimo ndani ya familia.

“Kwa mfano kama mtu ana tabia ya kula vibaya, unakuta kama wazazi walikuwa wanakula vibaya, watoto nao wanarithi hivyo hivyo, kwa hiyo unakuta kama wazazi walipata huo ugonjwa unakuja kukuta watoto nao wanaishia lipata kwa sababu ya hivyo visababishi hatarishi,” anabainisha.

Anasema waliweza kuhusisha jumla ya ndugu wa wagonjwa 1,063 na wote tuliwaona hapo JKCI. Wote walikuwa ni ndugu wa wagonjwa ambao tayari wameshagundulika na magonjwa ya moyo.

Anasema watoa huduma wote walikuwa watu wazima miaka 18 na kuendelea wastani wa umri wa wote ulikuwa miaka 40, asilimia 55.7 ya washiriki wote walikuwa wanawake.

“Tulitumia njia moja ya Shirika la Afya Duniani inaitwa WHO steps survey ili kuweza kuwachunguza hawa watu, tulijikita kuchunguza tabia kubwa saba hatarishi ambazo zinagawanywa katika makundi mawili.

“Moja ni tabia ambazo zinaitwa hatarishi zinazotokana na tabia zisizofaa na kundi la pili ni tabia hatarishi za kibaiolojia.

MATOKEO

“Kwenye kundi hatarishi za tabia zisizofaa tuliangalia vitu vikubwa vinne, kwanza uvutaji wa sigara au matumizi ya tumbaku kwa ujumla ambapo asilimia 3.2 ya ndugu wote wa wagonjwa au wanaohudumia wagonjwa walikutwa na tabia hii.

“Asilimia 5.3 walikutwa na matumizi ya pombe, asilimia 65 walikutwa na ulaji usiofaa {mbovu} na asilimia 77.1 walikutwa maisha yao hayapo ‘active’ yaani hawana utaratibu wa mazoezi ya aina yoyote {maisha yao ni tabiabwete.

Anaongeza “Kundi la pili la tabia hatarishi za kibaiolojia hili lina sababu kubwa tatu tuliangalia kwanza uzito mkubwa kupindukia ambapo 66.8% ya watu wote walikuwa na uzito mkubwa kupindukia, 69.5% walikutwa na shinikizo la juu la damu na 5.8% walikutwa na kisukari.

“Kwa lugha rahisi mwenye sababu tatu au zaidi yupo hatarini zaidi, kwa bahati mbaya, katika utafiti wetu nusu ya watu wote walikuwa na sababu hatarishi tatu au zaidi ambayo si hali nzuri.

“Kwa sababu tafsiri yake ni kwamba hawa wauguzaji miezi michache au miaka michache ijayo na wenyewe wataishia kuwa wagonjwa kama hawa ambao wanawauguza sasa hivi,” anasema.

TUZO KIMATAIFA

Dkt. Pedro anasema utafiti huo ulitunukiwa tuzo ya Kimataifa hivi karibuni katika Mkutano mkubwa  wa Afrika unaoangazia masuala ya moyo uliofanyika huko Nairobi, Kenya.

Anasema katika mkutano huo tafiti 85 ziliwasilishwa na kuchujwa kwa awamu tatu, ambapo katika awamu ya kwanza zilipita tafiti 40 baada ya kupitiwa na jopo la majaji wanane.

“Awamu ya pili zilichujwa na kusalia 20 ambapo washiriki walipewa dakika kuwasilisha machapisho yao, katika mchujo huo majaji wawili ambao ni wabobezi kwenye magonjwa ya moyo walitoa alama kwa tafiti hizo 20 na sisi kuibuka washindi wa tuzo hiyo,” anasema.

Anaongeza “Ushindi huu umekuja kama suprize kubwa kwa sababu katika hii mikutano mikubwa Watanzania tumekuwa tukienda kupigia makofi wengine kwa miaka mingi, kuliko kuwa watoa mada kutoa yake yanayoendelea kwetu kufundisha wengine.

“Katika kinyang’anyiro hiki mpaka natuma ‘abstaract’ {chapisho} sikujua kama kuna mashindano lakini tulipitishwa katika mchakato huo na kuibuka washindi.

“Ulisimamiwa na Maprofesa wawili, mmoja alikuwa raia wa Sudan mkuu wa idara ya magonjwa ya moyo Kartoom amebobea kwenye tafiti za masuala ya moyo na mwingine mkenya, walitoa alama zao kwa machapisho yote yaliyofikia hatua ya juu, tukashinda.

ZITAWEKWA KISWAHILI

Prof. Janabi anaongeza “Ushindi huo umewaongezea hari na hamasa ya kuzidi kufanya tafiti ambazo zitaleta majibu yanayoweza kuimarisha huduma za uchunguzi na tiba dhidi ya magonjwa ya moyo si tu Tanzania, bali pia Afrika na dunia kwa ujumla.

“Majibu ya utafiti huu {wa care givers} yanatupa mwanga na kutu-alert kwamba tuweze kuimarisha elimu ya afya hasa ya magonjwa sugu katika jamii zetu.

“Lakini pia kutafuta namna ya kuwa na afua {intervesions} za makundi ambayo yameathirika zaidi kama hili la watoa huduma ili kuweze kupunguza kasi ya haya magonjwa sugu.

“Tunaendelea kusambaza hizi tafiti ndani na nje ya nchi kwenye majarida ya kimataifa kwa faida ya kila mtu kwa Bara letu la Afrika na Dunia kwa ujumla,” anasisitiza.

Anaongeza “Tunaendelea kuhamasisha madaktati, wauguzi bio-engineer kufanya tafiti kwa kila wanachokiona kuweza kuchangia kwenye sayansi kwa ujumla.

“Kwa sababu bila tafiti za kwenu wenyewe ndani ya hospitali hatutaweza… chukulia mfano kwa  barabara ili uweze kujua ujenge ya namna gani unatakiwa ujue yanapita magari ya namna gani, yana uzito namna gani kwa hiyo hata huku kwenye tiba na kwenyewe ni hivyo hivyo.

“Wenzetu Wamarekani, Ulaya, Asia na kwenyewe ni hivyo hivyo wamefanya tafiti wanakuambia mgonjwa huyu anatakiwa kupewa dawa hii, sasa hiyo ni kweli lakini suala la kujiuliza kilichoonekana kule unaweza ukakileta moja kwa moja huku?.

“.., au watu wetu kwa sababu ya ‘background’ tofauti mahala tunapozaliwa, chakula tunachokula, hali ya hewa labda dawa zina tofauti labda huyu inaweza kuwa tofauti.

Prof. Janabi anaongeza “Kwa hiyo, utaona  ni vizuri sana kuwa na tafiti zenu za ndani vile vile kwa zile ndiyo zina uhalisia wa sisi kama Watanzania, Waafrika.

“Kwa sababu labda dawa inayosaidia kwa mzungu, mwarabu au mu-Asia labda kwa Waafrika inaweza kuwa dozi ishushwe zaidi au ipandishwe zaidi.

“Kwa hiyo vitu kama hivyo tafiti ni kitu muhimu sana sana katika maendeleo yoyote ile, ama sayansi au kwengine. Hapa JKCI kwa mwaka tunajitahidi kufanya angalau tafiti tatu hadi nne,” anabainisha.

Anasisitiza “Si kitu rahisi, kwa mwaka inategemea, lakini tunajitahidi tusikose machapisho matatu au manne … inachukua muda kwa sababu lazima ukusanye data. Tukiweza manne kwa mwaka huwa tunafarijika sana.

Anasema kwa kuwa idadi kubwa ya watu nchini inazungumza lugha ya Kiswahili na kwamba lugha hiyo imeendelea kukua na kuenea katika mataifa mengine mengi duniani.

Anasema JKCI wamekusudia siku za usoni kuanza kutoa sehemu ya machapisho ya tafiti zake katika lugha hiyo adhimu ya Taifa.

“Kwa sasa yapo kwa lugha ya Kingereza kwa asilimia 100, tunataka kujaribu katika mwaka mpya wa fedha kuandika kwa kifupi kwa Kiswahili kuweza kuwafikia jamii kubwa zaidi.

“Kwa mfano, tafiti zetu za UVIKO – 19 tuweze kuziweka kwa Kiswahili ili watu wazidi kupata uelewa kuhusu huu ugonjwa unavyosambaa, jinsi ya kujikinga na tutajaribu kuziweka katika ukurasa mmoja au miwili,’ anabainisha.

UMETUFUNGULIA NJIA

“Ni jambo la kujivunia JKCI kutwaa tuzo hiyo ya Kimataifa, huu ni wakati wanasayansi wetu kuamka kwamba kazi tunazofanya ni bora tufanye bora zaidi ili tunapoenda kwenye jumuiya za kimataifa tunachowasilisha kionekane bora kuliko kwenda kupigia makofi watu wengine.

“Tayari ushindi huu umeongeza visibility ya Tanzania, kwamba JKCI kuna kazi ambazo zinafanyika kubwa na za kuigwa, baada ya kuwasilisha mmoja wa maprofesa alisema hajawahi kuwaza utafiti unaweza kufanyika kwa ndugu za wagonjwa.

“Umemfungua macho, alisema akirudi kwao atampa mwanafunzi wake wa phd akafanyie utafiti, umefungua nafasi ya sisi kualikwa kwenye mikutano mingine kuna ‘sponsrors’ walikuja na kusema ‘Kenya Cardiac Society wametuwaalika wanasayansi watatu kwenda.

“Vitu kama hivi vinaongeza wigo wa sisi kuweza kuonesha kazi zetu zaidi utakuwa charge ya 'ku-motivate' sisi wa nyumbani kwamba tukifanya kazi nzuri tunaweza kusaidia pia nchi zingine,” anasema.

Anaongeza “Changamoto ambayo ni kitu tunatakiwa tujifunze, sisi huku mikutano hii imekuwa zaidi inawapa nafasi madaktari lakini pamoja na mimi kuwa daktari naona si sawa.

“Nimejifunza katika timu zote za wenzetu waliokuja Wasudan, Waethiopia, Waganda walikuwa na mchanganyiko wa madaktari, wauguzi, wafamasia na wengine kitu ambacho naamini ni afya kwa taasisi yoyote ambapo kila mkutano wanaochangamkia zaidi ni madaktari.

“Aidha, muuguzi mmoja utafiti wake ulishindana na kufanikiwa kuingia katika 20 bora, tunatakiwa kuwa ‘impower’ watumishi wenzetu hao kada nyingine pia kufanya tafiti na kujaribu kutuma kwenye mikutano kama hii wanaweza kushinda.

“Kimsingi, kwenda kwenye mikutano hii kunakupa ‘exposure’ mwisho wa siku wote mnakuwa bora katika ‘level’ za kimataifa,” anasisitiza Dkt. Pedro.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement