Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Ipo hatari kubwa {high alart} kwa
Tanzania kupata maambukizi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, ambao upo nchi
jirani ya Uganda, ikiripotiwa kirusi kilichozuka huko hakuna chanjo ya
kukidhibiti duniani.
Ukaribu na muingiliano mkubwa
wa idadi ya watu wa mataifa haya mawili ya Afrika Mashariki kupitia njia rasmi
za usafiri zinaongeza tishio hilo, huku pia ikitajwa changamoto ya uwepo wa
njia zisizo rasmi.
Tanzania kupitia Wizara ya Afya
imewaagiza wakuu wa mikoa kujiandaa ipasavyo kumtambua mapema mhisiwa yeyote
mwenye dalili za Ebola, kumtenga na kumpa matibabu.
Wameagizwa kuandaa timu za
wafuatiliaji za wataalamu, ‘ambulance’ za kuwasafirisha, dereva hadi eneo la
maziko iwapo kifo kitatokea.
Wizara imesisitiza mtu
aliyefariki kwa ugonjwa huo atazikwa na jopo maalum na kwa heshima zote
kulingana na miongozo ya kimataifa.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
ametoa maelekezo hayo mbele ya waandishi wa habari wakati alipokuwa akitoa
tahadhari kwa wananchi juu ya ugonjwa huo uliozuka Uganda tangu Septemba 20,
2022.
“Hadi sasa hakuna kisa chochote
kwa Tanzania,” amesema.
Waziri Ummy ameongeza “Ripoti
ya Wizara ya Afya Uganda zinaeleza kufikia Septemba 26, 2022 tayari wagonjwa 43
na vifo 23 vimerekodiwa.
“Ni takriban kilometa 130
kutoka ilipo Wilaya ya Mubende hadi Kampala, Makao Makuu ya Uganda na takriban
kilometa 220 kutoka Kampala hadi Mutukula Mkoani Kagera, Tanzania.
“Umbali kutoka Mubende kwenda
Mutukula Mkoani Kagera Tanzania kupitia Masaka ni umbali wa kilomita 230,”
amesema.
Ameongeza “Taarifa zinaonesha
kuwa watu hawa wana dalili za homa kali, degedege, kutapika matapishi yenye
damu, kuharisha na kutokwa damu machoni.
“Uchunguzi wa kimaabara
umethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola anuai aina ya Sudan (Ebola-Sudan
strain).
“Hadi sasa jumla ya watu 425
waliotangamana na wagonjwa (Contacts) wameanishwa na kati yao watu 127
wamepatikana na wanafuatiliwa ikiwa wataonyesha dalili za kuwa na ugonjwa huu.
“Uwepo wa ugonjwa wa Ebola
katika nchi jirani unaiweka nchi yetu katika hatari kubwa kutokana na
mwingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia mipaka rasmi na
isiyo rasmi.
Ameongeza “Uchambuzi wetu
umeonyesha kuwa Mikoa iliyo hatarini zaidi ni Kagera, Mwanza, Kigoma, Geita na
Mara.
“Aidha Mikoa ya Dar es salaam,
Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma ipo katika hatari kwa sababu ya
uwepo wa viwanja vya ndege na vituo vikubwa vya mabasi ya kutoka nchi jirani.
“Hata hivyo, hadi sasa hakuna
mgonjwa wa Ebola nchini Tanzania. Hivyo yatupasa kila mmoja wetu kuchukua hatua
na kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini.
“Kwa mamlaka niliyopewa
nawaagiza wakuu wa mikoa kujiandaa na ni lazima waainishe gari lipi la wagonjwa
‘ambulance’ itatumika, timu ya wataalamu wa ufuatiliaji, mtu yupi wa maabara
atahusika katika kuchukua sampuli.
“Mgonjwa akipatikana atapelekwa
wapi, vifaa vitawekwa wapi, tusidharau tetesi yoyote kuhusu wahisiwa wa Ebola,
waandae maeneo ya maziko tukipata kifo cha mgonjwa wa ebola tunapaswa
kumuhifadhi wapi.
“Waliokuwa karibu na mgonjwa
pia wanapaswa kufuatiliwa na wakuu wa mikoa wajue watawekwa wapi,” ameagiza.
Ameongeza “Tusidharau hata
dalili ya homa maana wagonjwa wengi wa Uganda waliliripoti dalili hii, dalili
nyingine ambazo waliripoti ni degedege, kutapika matapishi yenye damu,
kuharisha na kutokwa damu machoni.
Uchunguzi wa kimaabara
umethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola anuai aina ya Sudan (Ebola-Sudan
strain) na hauna chanjo.
Waziri huyo mwenye dhamana ya
afya amesema Ugonjwa wa Ebola uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1976 katika
nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan.
Tangu kugundulika kwake, kumekuwa
na milipuko kadhaa katika nchi za Uganda na DRC ambapo DRC imekuwa na milipuko
mingi zaidi. Nchi za Uganda na DRC tunapakana nazo
Chapisha Maoni