Na Veronica Mrema – Dar es Salaam
Msemo uliozuka ghafla na kujizolea umaarufu miongoni mwa jamii
hususan kwa kundi la vijana ‘mwagilia moyo’, wakiutumia kuhimizana ‘kula’
starehe haswa unywaji wa pombe kupita kiasi, utawagharimu wengi siku zijazo.
Wataalamu wa afya wamezidi kutoa tahadhari, pombe ni kati ya
vichochezi / visababishi ambavyo kwa kiasi kikubwa huchangia mtu kuishia
kwenye janga la magonjwa yasiyoambukiza {sugu}.
Magonjwa hayo ni pamoja na yale ya moyo, saratani, shinikizo la damu,
kisukari, kiharusi na mengineyo.
Pombe inatajwa kuwa na athari nyingi ikiwamo kusababisha upungufu wa nguvu za kiume, kuzaa watoto wenye ulemavu, saratani za kinywa, koo, ini, utumbo, matiti na tezidume.
Ni kichocheo cha ngono zisizo salama ambazo huchangia kasi ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa, Ukimwi na mimba zisizo tarajiwa, ajali za barabarani, nyumbani, ugomvi na athari nyinginezo nyingi.
Akizungumza katika semina maalum ya siku moja kwa waandishi wa habari
iliyofanyika kupitia mtandao wa zoom mapema hii leo Mkurugenzi Msaidizi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Yasiyoambukiza, Dkt. James Kiologwe
amesema,
“Magonjwa haya yanazidi kushika kasi, hivi sasa nchini yanachangia
takriban 41% ya vifo vyote vinavyotokea kila mwaka na ni gharama kubwa kuyatibu.
Ameongeza “Vijana mna tabia nyingi ngumu… haya mambo ya kumwagilia
moyo ni changamoto, wanahabari tusaidieni kuelimisha jamii.
Amesema pamoja na unywaji pombe kupita kiasi, tabiabwete nayo ni
changamoto nyingine ambayo inawaweka watu wengi kwenye hatari ya kuishia kupata
magonjwa hayo.
“Bado wengi hawafanyi mazoezi, wengine ni
wavutaji wa sigara, hawazingatii ulaji unaofaa... wanakula vyakula vyenye chumvi
nyingi, sukari nyingi, mafuta mengi na vinywaji vyenye sukari nyingi, hivyo wanazidi kujiweka kwenye uwezekano wa kuishia kwenye
magonjwa hayo.
Amesisitiza ni muhimu jamii kuelekeza nguvu
zaidi katika kupambana, kudhibiti na kuzuia magonjwa hayo ambayo hivi sasa ni janga kubwa
nchini na duniani.
“Tafiti zinaonesha duniani watu milioni 15 wanakabiliwa na
kiharusi, 8% wanaishi Afrika na kiharusi pekee huchangia 85% ya vifo
vinavyotokea kila mwezi kutokana na kiharusi Barani Afrika.
“Tanzania tafiti zinaonesha 26% ya watu wana Shinikizo la Damu
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili 33% ya wagonjwa wanaopokea wana kiharusi na
hufa ndani ya mwezi mmoja tangu wamepokewa.
“Tafiti zinaonesha pia robo tatu ya wagonjwa hawakuwa wanajua hali
zao kabla, walifikishwa Muhimbili wakiwa tayari wamepata madhara yatokanayo na
ugonjwa kwa mfano figo kushindwa kufanya kazi.
Ameongeza “Tuna kazi kubwa ya kuelimisha watu, wapime/wachunguze
afya zao mara kwa mara, ikiwa mtu ana umri wa miaka 40 na kuendelea inashauriwa
angalau mara moja kwa mwaka.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanasababisha vifo vya mapema, tafiti
zetu zinaonesha kuna zaidi 75% ya watu wana shinikizo la damu nab ado hawajui
hali zao.
“Kwa upande wa saratani zaidi ya robo tatu ya wagonjwa wameenda
hospitali ikiwa tayari imesambaa sana hatua za juu {tatu na nne ambazo kwa
kawaida ni ngumu kutibika na kupona}.
“Zaidi ya 64% ya wenye kisukari hufika hospitalini wakiwa tayari
wameanza kupata madhara ya ugonjwa kwa mfano kwenye macho, figo nakadhalika.
Dkt. Kiologwe amesema kutokana na hali hiyo ndiyo maana
inashauriwa watu kuchunguza afya zao mara kwa mara waweze kugundulika mapema na
kupatiwa matibabu ya mapema ili kuepushwa na madhara yanayoweza kusababishwa na
magonjwa hayo.
“Vituo vya afya vihakikishe vinapima kiwango cha sukari kwenye
damu, shinikizo la damu na kiwango cha mafuta kwenye damu kila mtu anayefika
kituoni kupata huduma.
Amesema wanashauri pia watoto wenye umri chini ya miaka mitano
tunashauri wapime macho angalau kila mwaka.
“Ni muhimu pia kina mama kuweka utaratibu wa kuchunguza afya za
matiti na kizazi angalau mara moja kwa mwaka,” ametoa rai.
Chapisha Maoni