Mataifa yaliyopo Barani Afrika
yamehimizwa kuongeza uwekezaji katika mifumo yake ya sekta ya afya ili
kuimarisha zaidi ulinzi wa afya ya jamii kwa ujumla dhidi ya majanga na
magonjwa mbalimbali hususan ya milipuko.
Rai hiyo imetolewa na
Waziri wa Afya wa Rwanda Dkt. Yvan Butera alipokuwa akizungumza wakati wa kuhitimishwa
kwa mkutano wa pili wa kimataifa CPHIA, uliofanyika Mjini Kigali.
Mkutano huo uliosimamiwa
chini ya shirika la Africa CDC ambao ulijikita kuangazia uwekezaji wa mifumo ili
kuimarisha ulinzi wa afya ya jamii Barani Afrika.
“Ni muhimu kuenelea kuwapo
ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika na washirika wa kimataifa {wadau wa
maendeleo} ili kuendeleza ‘uzalishaji’ wa bidhaa za afya kwa ubora zaidi,
kuimarisha mifumo ya kukabiliana na dharura, kuimarisha afya kwa wote
ulimwenguni,” amesema Dkt. Butera.
“Serikali ya Rwanda kupitia Wizara ya Afya inafuraha kushirikiana na Africa CDC katika utekelezaji wa mpango wa ‘The New Public Health Order’ katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuimarisha taasisi za afya ya umma.
Amesema hayo yote
yanaakisi malengo makuu ya mkutano huo katika kuhakikisha mataifa yanaweka ahueni
na mifumo imara ya kudhibiti na kuzuia magonjwa ya milipuko na majanga kwa siku
zijazo.
Katika hatua hiyo mpya
inayolenga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji afya ngazi ya jamii, nguzo muhimu
za kufikia malengo zimetajwa ni pamoja na uongozi imara, usawa, uvumbuzi na
kujitegemea.
Wadau wameunga mkono
kwamba ni vema kuwepo kwa mbinu mpya itakayoyawezesha mataifa ya Afrika kuwa na
utayari wa kukabiliana na changamoto za ki-afya kwa siku zijazo.
"Mazungumzo na
matukio haya yanaonyesha kile ambacho sote tunafanya ili kufikia lengo, ni wazi
kwamba tumetoka mbali tangu tulipozindua mpango wa kwanza mwaka 2020.
“Lakini tuna kazi zaidi ya
kufanya kabla ya kila mmoja wa kaka na dada zetu kupata huduma bora za afya,” amesema
Kaimu Mkurgenzi wa Africa CDC, Dkt. Ahmed Ogwell Ouma.
Sambamba na hilo, Africa CDC iliweza kutambua michango ya baadhi ya wataalamu wa afya waliojiweka mstari wa mbele katika kuimarisha huduma kwenye mataifa yao.
Miongoni mwa walitambuliwa kwa tuzo maalum ni Dkt. Ameyo
Stella Adadevoh kutoka Nigeria ambaye alisaidia mapambano dhidi ya Ebola.
Mwengine aliyetunukiwa ni Prof. Rose Leke kutoka Chuo Kikuu cha masuala ya Sayansi – Cameroon. Africa CDC pia imemtambua Gorreti Marie Zalwango kutoka Uganda na Dkt. Mutia Kehwalla Aza.
Katika mkutano huo makubaliano mbalimbali pia yamesainiwa
ili kuhakikisha sekta ya afya inazidi kupewa kipaumbele Barani humo.
Mkutano huo wa siku 3 {13-15 Desemba, 2022} ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kigali ukiwa na washiriki zaidi ya 2,500 kutoka nchi 90 katika Bara la Afrika na kwingineko.
Umewajumuisha wakuu wa nchi na mawaziri wa afya, wanasayansi na watafiti wakuu, wawakilishi
kutoka. sekta binafsi, mashirika ya kiraia, mashirika ya kimataifa ya afya na
maendeleo.
Uliongozwa na wasemaji
wakuu mbalimbali, akiwamo Rt. Mhe. Édouard Ngirente, Waziri Mkuu, Jamhuri ya
Rwanda; Mhe. Dk. Yvan Butera, Waziri wa Afya wa Jimbo, Jamhuri ya Rwanda; Dk.
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu, Shirika la Afya Duniani {WHO}.
Wengine ni Chikwe Ihekweazu, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi, Shirika la Afya Duniani {WHO} kwa Ufuatiliaji na Ujasusi wa Dharura wa Afya; Bi Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji UNAIDS, Prof Awa Marie Coll Seck.
Wengine ni Waziri wa Nchi kwa Rais wa Jamhuri
ya Senegal na Dkt. Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi, Kituo cha Afrika cha
Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa {Africa CDC.}
Mkutano wa tatu wa CPHIA unatarajiwa kufanyika Lusaka, Zambia ambapo mwenyeji mkuu wake ni Wizara ya Afya nchini humo.
Picha kwa hisani ya akaunti rasmi za Africa CDC
Chapisha Maoni