Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema 

Kasi ya uelimishaji jamii kuhusu ugonjwa wa Siko Seli katika maeneo ya mijini na vijijini inatarajiwa kuongezeka maradufu kupitia Jarida la Shujaa ambalo linaandaliwa na watu wanaoishi na ugonjwa huo nchini Tanzania.

Jarida hilo la kipekee na la aina yake limezinduliwa leo Dar es Salaam na Jukwaa la watu wanaoishi na Siko Seli Tanzania chini ya Mkurugenzi wake Arafa Said, hafla iliyoshuhudiwa na wadau mbalimbali wa magonjwa yasiyoambukiza, waandishi wa habari na mashujaa hao.

Akizungumza, Arafa amesema bado kuna uelewa duni kuhusu ugonjwa wa Siko Seli kwenye jamii na kwamba jukwaa hilo liliona wazi kuna umuhimu wa kuanzisha jarida ili kuongeza nguvu zaidi katika uelimishaji.

“… maudhui yake makubwa ni kuongeza elimu, kutoa burudani, kuwezesha mashujaa kujua/kupata mwelekeo {yaani} kuweza kuelewa kuwa na Siko Seli si mwisho {wa maisha},” amesema.

Ameongeza “Tunaongea na mashujaa waliokubali ushujaa wao na kuendelea kufanya kazi nyingi za kijamii na kuwa na maono nje ya kuwa na siko seli,

“Tunafurahi sana na tunategemea liwe linatoka mara tatu kwa mwaka, kwa sasa tutajikita kwenye mitandao ya kijamii lakini pia tuna wito kwa wafadhili wakiweza kutusaidia tutatoa machapisho mengi,” amesema.

Fatuma Ubwa, shujaa anayeishi na Siko Seli kwa miaka 70 sasa ni miongoni mwa mashujaa ambao makala yake imechapwa ndani ya Jarida hilo, toleo la kwanza.

“Nashukuru linaweza kufika mbali kwa upeo wangu, watazidi kuelimika watu mjini hadi vijijini, tupiganie sana,” ametoa rai.

Mwanahabari kutoka jukwaa la TOANCD, Exuperius Kachenje amesema “Uzinduzi huu ni hatua mbele katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

“.., hasa upande wa elimu kwa sababu inajulikana magonjwa yasiyoambukiza hayapewi kipaumbele katika taarifa zake kuingia kwenye vyombo vya habari.

“Jarida hili litabeba vitu vingi, elimu kuhusu siko seli na mambo mbalimbali, ushirikishwaji wa wagonjwa wenyewe watatoa shuhuda zao.

“Elimu itasambaa na mapambano yatafika mbali, naamini siku moja watanzania wataelimika zaidi na tutafika mbali,” amesema.

Naye, Mbarouk Ambali ambaye ni mzazi wa Shujaa amesema “.., Jarida hili ni kitu kikubwa sana na nina imani sisi kama wazazi na walezi kama litafika tutalipata kwa wakati, litatusaidia.

Ameshauri pia kuwe na mpango wa kuhakikisha jarida hilo linafika Tanzania nzima kwani bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu kuhusu Siko Seli na taarifa nyingi potofu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Hospitali ya Taifa Muhimbili Elisha Osati ambaye pia ni mtafiti mbobezi katika ugonjwa wa Siko Seli, amesema jarida hilo litasaidia kuwasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali kuhusu ugonjwa huo kwa lugha rahisi itakayoeleweka kwa jamii.

“Itakuwa inazungumzia matibabu kwa wagonjwa na maoni mbalimbali kutoka kwa wagonjwa wa sikoseli kuhusu maisha yao.

Ameongeza “Lakini pia wagonjwa wengine, ni jambo zuri itatusaidia kupeleka taarifa, ujumbe kwa jamii na wataalamu mbalimbali.

“Tunawapongeza arafa na timu nzima ya chama cha wagonjwa wenye siko seli kwa kuja na mradi huu ambao umetoka kwao wenyewe.

“.., wao kama wagonjwa wana uzoefu zaidi kuhusu ugonjwa wao kuliko sisi wataalamu, inakuwa vizuri wakija kwa pamoja kitasaidia jamii, watatupa ule uhalisia.

“Sisi kama wataalamu tunaahidi kuendelea kushirikiana nao na kupeleka mbele ujumbe huu wa jarida, tunaomba wanahabari, wadau watusaidie kupeleka mbali taarifa hizi,” ametoa rai.

Takwimu za dunia zinaeleza kila mwaka kuna watoto wapatao 300,000 wanaozaliwa na ugonjwa huo huku Tanzania ikiwa ni nchi ya tano kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli.

Takwimu zinaeleza Tanzania kila mwaka wakizaliwa watoto 11,000 ikiwa ni sawa na mtoto mmoja katika kila watoto 1,000 na 20% ya raia wake wana vinasaba vya ugonjwa huo na wengi bado hawajijui hali zao.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement