Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema  

Kila binadamu ameumbwa na hali ya misukumo/mihemko {ya ndani} kwa ajili ya kufanya jambo fulani, lakini misukumo ile wengine huweza kuidhibiti ili isiweze kuleta madhara.

Chukulia mfano… kuna wakati mwingine unaongea na mtu fulani kisha akakuudhi basi unaweza kujikuta unapata ule msukumo wa ndani labda umtukane au upigane naye.

Hali hiyo inaweza kutokea ilihali hukuwa umekusudia kabisa kumpiga au kumtukana, ni katika mazingira ya namna hiyo ambayo unaweza kujikuta umeua na hata kuchukua uamuzi wa kujiua.

Lakini wataalamu wa masuala ya afya ya akili wanasema mtu anao uwezo wa kudhibiti msukumo wa ndani {wa hasira na visasi} hatimaye kuepuka kuua au kujiua.

Ndani ya mwaka huu wa 2022 karibu kila siku jamii ya Watanzania imekuwa ikishuhudia au kusikia visa vya watu kuua au kujiua.

Vitendo hivyo vimekuwa vikiibua mjadala kila kona kiasi cha Wizara yenye dhamana ya masuala ya afya kuitisha mjadala/mdahalo wa kwanza Kitaifa kuhusu afya ya akili.

Kipo kisa kilichoripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni ‘Aliyekatazwa mahusiano ajiua’ ambacho ni miongoni mwa visa vilivyoshangaza wengi.

Aidha, kipo kisa kingine cha kijana mwenye umri wa miaka 22 mkoani Geita ikielezwa kwamba amejiua kwa kunywa sumu baada ya kudaiwa hajalipa deni la Tsh. 45,000 ya soda.

“Matukio kama haya yanayojitokeza ya watu kujiua {kujidhuru} kutokana na kuwa kwenye mazingira yanawachochea.

“.. wakajikuta kuwa Wana msukumo wa kuamua jambo pasipo kujua matokeo yake,” anasema Daktari wa Binadamu kutoka Idara ya Afya ya Akili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Raymond Mtani.

Dkt. Raymond anaongeza “Kwa maana mtu amepoteza ‘control of impath’ {msukumo wa hasira/visasi… ndani ya mwili wake}.

“Kuna wale wengine wanaweza kudhibiti ile hali na kuna wengine ambao wanajikuta wanashindwa kuidhibiti.

“Hivyo, {akiudhiwa} kama ni mpango wa kupiga atajikuta anapiga kama ni mpango wa kutukana, atatukana kwa sababu anakosa huo udhibiti.

“Ni kwamba kunakuwa na huo msukumo… ukiwa na hasira kunakuwa na msukumo fulani,” anasisitiza Dkt. Raymond.

HUCHOCHEWA NA PRESHA ZA NJE’

Dkt. Raymond anafafanua “Kuna mwengine inaweza ikawa ameudhiwa, ameambiwa jambo ambalo hajalitenda.

“Anapata huo msukumo wa hasira {kutokana na kusingiziwa jambo hilo huku akijua wazi hajalitenda}… zinampa ‘presha’ ya kufanya kitu.

“Inawezekana anapopata ‘presha’ ya kufanya kitu {kutukana au kupigana} huwa hafikirii madhara au matokeo ya huo msukumo anaoupata {kimazingira/kusingiziwa} itakuwaje.

Anaongeza “Kwa hiyo inaweza ikatokea mtu amefanya jambo na au hajafanya kitu lakini kuna ‘presha’ kutoka nje kwamba {wewe ndiye umefanya}.

“Kwa hiyo mtu anapandwa na hasira, anashindwa kuudhibiti ule msukumo, anaweza akaamua kuchukua kitu ili ajichome au anywe sumu.

JINSI YA KUEPUKA

Dkt. Raymond anasema kuna umuhimu mkubwa jamii kuweza kusaidia watu ambao hukumbana na hali zinazoweza kuchochea wawe na msukumo wa hasira ili kuepusha madhara.

“… matukio mengi yanatokea, mtu alikuwa kwenye mazungumzo wamepishana kidogo mtu anapata msukumo, hasira anachukua jiwe au chupa.

“Kuna umuhimu mkubwa kama jamii kuweza kuwa na udhibiti {wa misukumo ya hasira / visasi},” anashauri.

Anasisitiza “Tuwe na uwezo wa kusimamia {kudhibiti hasira/visasi}, mara nyingi nasema ni muhimu mtu kufundishwa tangu akiwa mdogo… anapopandwa na hasira.

“.., asiruhusu kuchukua hatua yoyote, aondoke eneo ambalo linachochea kuwa na hasira.

“Lingine ni uwezo wa kuvuta pumzi au wakati mwingine ni nafasi ile ya kutokutoa nafasi ya kutoa tafsiri ya kile kitu ambacho umefanyiwa.

Anafafanua “Mara nyingi tunatoa tafsiri ya yale ambayo wenzetu wametuambia labda amekutukana mtu unapatwa na hasira kubwa.

“Lakini ingetokea mtu labda ana changamoto {ya akili} hana utimamu {akakutukana} huchukii uzito.

“Lakini labda ndugu yako amekutukana, unaanza kutafsiri {akilini mwako} kwamba kwanini amenitukana.

“Tukishindwa kudhiti {msukumo wa hasira/visasi} inaweza kuleta madhara {ikiwamo kuua / kujiua,” anasema. 

Dkt. Raymond ambaye pia ni mjumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari za Afya ya Akili Tanzania {AMNHJ} anasema ni muhimu pia vyombo vya habari kuendelea kuwapa nafasi wataalamu wa masuala ya afya ya akili ili kwa pamoja waisaidie jamii.

“Vyombo vya habari ni muhimu kupata nafasi ya kutoa elimu kwa jamii namna gani ya kuepuka misukumo au mihemko ili kuepusha vifo vinavyoweza kuzuilika,” anasisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement