Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Ripoti za Wizara ya Afya Tanzania zikieleza bado hakuna kisa chochote cha mgonjwa wa Ebola, Taifa hilo la Afrika Mashariki limezidi kujiimarisha mifumo yake ya ufuatiliaji wa magonjwa.

Hatua hiyo inalenga kuzidi kuzuia ugonjwa huo ambao umeripotiwa katika nchi ya Uganda lakini pia kujiimarisha endapo ikatokea umeingia basi udhibitiwe, usiweze kusambaa zaidi na kuathiri zaidi.

Imeelezwa, Mkoa wa Dar es Salaam ambao ni miongoni mwa mikoa iliyopo kwenye hatari na tishio zaidi la kupata maambukizi ya ugonjwa huo kutokana na muingiliano mkubwa wa watu, umejiimarisha kwa kuwapa mafunzo wataalamu zaidi ya 3,000 wa sekta ya afya.

Mratibu wa Kujikinga na Kudhibiti Magonjwa ya milipuko kutoka Wizara ya Afya Dkt. Joseph Hokororo amebainisha hayo leo wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika semina ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo, namna unavyoambukiza na jinsi ya kujikinga ili wapeleke elimu sahihi kwa jamii.

"Tanzania inachukua hatua hiyo madhubuti pamoja na nyinginezo ikiwamo ile ya kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege na kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na nchi jirani {Magufuli Bus Stand}, kwa sababu upo huko nchini Uganda," amesema.

Hokororo ameongeza "Hatuna mhisiwa wala mgonjwa wa Ebola kulingana na ripoti ya mwisho iliyotolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu.

"Hata hivyo, bado tunalazimika kuendelea kujiimarisha mifumo yetu ya ufuatiliaji na ndiyo maana kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambao kuna muingiliano mkubwa wa watu na tuna mabasi ambayo hufika hapa yakitokea Uganda moja kwa moja ndiyo maana watumishi hao wakapatiwa mafunzo hayo.

Hokororo ameongeza "Wizara imejipanga kuhakikisha ugonjwa huu hauingii kabisa nchini na tayari imeshazielekeza halmashauri zote kuhakikisha zimetenga vituo ambavyo vitatumika endapo ugonjwa huu utaingia nchini.

"Kwa Dar es Salaam vituo hivyo vimetengwa pale Temeke na Kipawa," amebainisha huku akifafanua zaidi " Ebola ni ugonjwa hatari na kwamba kirusi kilichozuka huko Uganda, aina ya Sudan {SUVD} ni tishio zaidi kwani bado hakujathibitika chanjo inayoweza kumkinga binadamu dhidi ya kirusi hicho.

Amesema virusi hivyo hubebwa na wanyama kama popo na sokwe na kwamba binadamu katika hatua ya awali huambukizwa na viumbe hao.

"Kwa mfano kwa kula nyama ya Sokwe, lakini binadamu akishapata maambukizi katika hatua hiyo huweza kusababisha maambukizi kwa binadamu mwingine kupitia majimaji ya aina zote yanayotoka kwake.

"Kama vile machozi, jasho, damu, sindano, mbegu za kiume, au kwa njia ya kunyonya maziwa ya mama nakadhalika... virusi vinaweza kuishi kwa masaa au siku kadhaa katika eneo ambalo mgonjwa alikaa au kugusa," amesema.

Amesema ni kutokana na uhitaji wa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huo namna gani wazingatie ili kuzuia maambukizi yasiingie nchini na kuleta athari zaidi, ndiyo maana Wizara iliona umuhimu wa kukutana na kundi la waandishi wa habari.

"Kundi la waandishi wa habari ni miongoni mwa makundi yalpo hatarini kupata maambukizi kutokana na kazi mnazofanya, ndiyo maana tuliona tuwape ABC za ugonjwa huu ili iwe rahisi kwenu pia kuweza kutoa elimu sahihi kwa jamii ya Watanzania," amesema.

Awali, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Afya, Catherine Sungura amewahimiza wanahabari nchini kuzingatia usahihi wa taarifa wanazoziandaa kwa ajili ya kwenda kuziripoti/kuziandika kwa jamii.

"Taarifa zinazohusiana na magonjwa ya mlipuko hakikisheni zinakuwa sahihi, epukeni kuandika au kuripoti ambazo si sahihi kwani zinaweza kuleta taharuki na hofu kwa jamii," ametoa rai.

Amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kuelimisha jamii mara kwa mara hivyo ni muhimu kuzingatia usahihi wa taarifa wanazowapatia kwani jamii inaviamini vyombo vya habari na kile ambacho huwasilisha.

Akizungumza, Aziza Masoud kutoka Tanzania Daima ameishukuru Wizara ya Afya kwa mafunzo hayo kwa niaba ya wenzake waliohudhuria huku akiahidi kwamba watatumia vema elimu waliyopatiwa, akiomba pia wataalamu kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari pale inapohitajika.

Wizara ya Afya inawapa mafunzo hayo waandishi wa habari wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ushirikiano na Shirika la Management Sciences for Health (MSH)

Mafunzo hayo yalianza jana, leo na kesho yanatarajiwa kuhitimika na watakuwa wamepewa mafunzo jumla ya waandishi wa habari 120 ndani ya Mkoa huo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement