Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Ni furaha kubwa pale familia inapopewa ripoti ya kuruhusiwa kwa mgonjwa wao kutoka wodini na kuweza kurejea naye nyumbani, baada ya kuhitimisha matibabu hospitalini.

Hata hivyo, wapo baadhi ya wagonjwa ambao kulingana na aina ya ugonjwa unaowakabili hutakiwa kurejea hospitalini mara kwa mara kwa kipindi fulani ili waendelee kupatiwa huduma za ziada.

Kwa mfano, kama mtu alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake katika ajali fulani, huyo hutakiwa kurejea hospitalini kwa ajili ya kusafishwa na kufungwa upya kidonda.

Hatua hiyo ya muhimu mno hulenga kumuepusha asipate maambukizi mengine katika kidonda ambayo yanaweza kumsababishia matatizo mengi na hata kupoteza kiungo chake {kilichoathiriwa}, mwilini.

“Ni wakati kama huo, mtu anapokuwa akihitaji kusafishwa kidonda sisi kupitia taasisi yetu tunaweza kufika nyumbani kwake na kumpatia huduma,” anasema Ofisa Muuguzi mwenye uzoefu wa miaka mingi nchini, May Mushatsi.

Katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG hivi karibuni, May anasema pamoja na wataalamu wenzake, kupitia kampuni inayotoa huduma za kiuguzi majumbani {Nilax Home Health Services and Rehabilitation}, huwafikia wagonjwa kokote walipo.

May ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji anasema huduma hiyo ya uuguzi majumbani hutolewa kwa mgonjwa kwa kuzingatia miiko na maadili yote ya taaluma hiyo kama inavyotakiwa.

“Tumepatiwa usajili na mamlaka zote zinazohusika ikiwamo Wizara ya Afya, ni huduma rafiki na nzuri, tunaifanya kwa kushirikiana kwa ukaribu na wataalamu {madaktari} ambako wagonjwa wetu walipita na kupatiwa huduma kwanza.

Anatolea mfano mwengine pia kwamba ,magonjwa mengi yasiyoambukiza mara nyingi unaweza kukuta yamemsababishia ulemavu wa aina fulani mtu husika.

“Kwa mfano aliyepata kiharusi anahitaji mazoezi ya muda mrefu {physchiotherapy} ili huyo mtu arudi katika hali yake inawezekana siyo asilimia zote kama alivyokuwa anaweza kufanya shughuli zake za kila siku.

“Lakini {baada ya kupatiwa huduma} anaweza kurudisha uwezo wake kwa asilimia kadhaa, huyu mtu anafanyiwa mazoezi ya viungo katika mwili wake.

“Tunafanya hivyo pale alipo ama nyumbani, mazingira ya kutunza wagonjwa, tunamfuata na kumfanyisha mazoezi.

“Ili aweze kurudisha hali yake auy kwa kiasi fulani aweze kujitegemea, ikiwa ni sambamba na dawa zake na ndiyo maana tunashirikiana kwa ukaribu na madaktari wa wagonjwa husika,” anasema.

Anaongeza “Jamii ina elewa mtu anahitaji huduma ya namna hii lakini wapate wapi huduma kama hizi hapo ndipo kwenye changamoto,

“Unakuta wakati fulani hospitali zetu zinaelemewa, tunashirikiana nao ili kuongeza 'quality of life' kwa mtu husika, jamii inatoa ushirikiano mzuri kwetu katika kusaidia wagonjwa hawa.

Anabainisha {kwa kuwa wengi bado hawajui wanapoweza kupata huduma ya uuguzi nyumbani}, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu walipoanza rasmi Kisheria, 85% ya wagonjwa waliowahudumia ni wenye magonjwa yasiyoambukiza.

“ … hasa kisukari na shinikizo la damu, huhitaji huduma zetu, kuhakikisha wanaendelea kusalia salama licha ya matatizo yanayowakabili,” anasema.

Janga la mlipuko wa UVIKO – 19 limeacha athari nyingi {chanya na hasi} duniani hususan katika mifumo ya sekta ya afya, uchumi, jamii kwa ujumla na hata tamaduni.

Nchi nyingi zikishuhudia mabadiliko na maboresho ya mifumo yake mbalimbali ili iendane na hali ya wakati wa sasa.

May anaongeza “Nafahamu huduma hizi hutolewa pia na wataalamu walio chini ya Serikali na sisi wa sekta binafsi sasa tumeingia huku ili kuunganisha nguvu za pamoja na kutoa huduma kwa jamii yetu.

“Katika kipindi hiki ambapo tulishuhudia mlipuko wa UVIKO – 19 ni huduma ya wakati mwafaka kwa sababu utakumbuka kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima ilikuwa ni mbinu ya kuepuka ugonjwa huu.

“Kwa hiyo tukiweza kuwafikia wagonjwa nyumbani na kuwahudumia inakuwa ni huduma nzuri pia,” anasema.

Anaongeza “Kwa sababu unakuta pengine mgonjwa amewekewa mpira wa usaidizi labda wa kutoa haja ndogo au wa kupatiwa chakula, sisi tunakwenda nyumbani na kumpa huduma ya uuguzi pale inapohitajika.

“Kwa Dar es Salaam ambako ndipo tupo sasa na nimekuwa nikifanya kazi kwa muda mrefu wagonjwa kama hawa wapo kwa kiwango kikubwa,” anasema.

May anasema wanazingatia vigezo vyote muhimu katika kuwapata watoa huduma watakaokwenda majumbani kama ambavyo taasisi nyingine huzingatia.

“Huwa tunatangaza na watoa huduma wanaomba nafasi kufanya nasi kazi, kabla ya kuwaruhusu kwenda majumbani huwa tunawapa semina maalum.

“Tunawafuatilia hatua kwa hatua, ikiwamo kujaza ripoti maalum ambayo huiwasilisha kwetu na pia mgonjwa aliyehudumiwa hujaza ripoti na kuituma kwetu.

Anasisitiza “Hatua hii inalenga kulinda maadili ya kazi na kuboresha huduma zetu ambazo tunawapatia wagonjwa ambao tunawafikia majumbani.

“Tunaingia nao makubaliano maalum, lakini pia pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa huwa tunawapa elimu kwa ndugu wa mgonjwa jinsi wanavyoweza kumsaidia jamaa yao pia wakiwa nyumbani,” anabainisha.

Anasisitiza “Zinatusaidia kuboresha huduma zetu na kujua kama mtoa huduma anafuata maadili kwa mgonjwa wetu, jamii ijue kuna huduma hizi, wanapohitaji tunapatikana Sayansi Kijitonyama kwa sasa.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement