Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Kipimo cha damu chenye uwezo wa kubaini viashiria vya aina 10 za saratani kwa haraka na mapema zaidi, katika hatua ya awali {MultCancer Early Detection}, kitaletwa nchini Tanzania.

Hatua hiyo inatazamiwa kwamba italeta matokeo chanya katika kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwa uibuaji wagonjwa mapema na kuwapatia matibabu mapema.

Wanasayansi wanasema saratani inavyoibuliwa na kutibiwa mapema huleta matokeo chanya ya tiba na mtu kupona kabisa, hivyo kuepushwa na mateso mengi yatokanayo na maradhi hayo na hata vifo.

Mvumbuzi wa kipimo hicho cha OncoSeek {MCED} Dkt. Mao Mao wa Seekln yenye ofisi zake USA na China amesema kinatumia teknolojia ya AI pamoja na mashine ya maabara kubaini saratani hizo aina 10.

“Kipimo kinaweza kufanywa na watoa huduma za afya katika ngazi ya chini kabisa, sampuli ikasafirishwa kwa njia ya kawaida kabisa ya usafirishaji kwa kufungashwa vizuri hadi katika maabara kwa uchunguzi wa kina,” amebainisha.

Amesema ndani ya kipindi kifupi mno majibu ya uhakika hupatikana huku akibainisha aina za saratani ambazo zinaweza kuchunguzwa kwa kipimo hicho kimoja ni ya kibofu, matiti, kizazi, utumbo mpana.

Ametaja aina nyingine za saratani ni ya mapafu, ini, vifuko vya mayai vya mama {ovary}, kongosho, tumbo na matezi.

“Ni mbinu ya ubunifu wa juu katika zama hizi, inawezesha kuibua kwa haraka watu wanaokabiliwa na saratani na gharama yake ni nafuu sana kwa mwananchi na upatikanaji wa kipimo hiki ni wa nafuu mno,” amesisitiza.

Dkt. Mao Mao akiwa ameambatana na Prof. Rob Tenbrick kutoka Shirika la Inspire2Live la Uholanzi wametua nchini na kueleza namna kipimo hicho kinavyofanya kazi mbele ya wataalamu wa magonjwa ya saratani Taasisi ya Saratani Ocean Road {ORCI}.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na mashujaa {watu waliogua na kupona na wale waliopo kwenye tiba dhidi ya saratani mbalimbali} ocean road, Dkt. Alphonsina Nanai wa Shirika la Afya Duniani {WHO Tanzania}, Dkt. Sara Maongezi kutoka mradi wa TCCP pamoja na waandishi wa habari.

Akizungumza, Prof. Tenbrick amesema ni kipimo kinachoweza kubebeka na wataalamu kwenda kufanya uchunguzi katika maeneo mbalimbali hata yale ambayo hayana mashine za kisasa.

Ameahidi kutoa ushirikiano katika eneo la mafunzo kwa wataalamu katika ngazi ya vituo vya afya namna ya kuchukua sampuli na hadi kuzisafirisha hadi maabara kwa uchunguzi, huduma hiyo punde itakapoanzishwa.

"Tutawafundisha pia madaktari wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza namna ya kutumia dawa ya gharama nafuu sana, Lidocaine katika kudhibiti maumivu kwa wagonjwa," amesisitiza.

Mkurugenzi na Muasisi wa Tanzania Cancer Society {TACASO}, Franklin Mtei ndiye ambaye ameleta wataalamu hao mabingwa nchini.

Dkt. Mtei anaiwakilisha Tanzania katika ushirikiano na Insipire2Live katika ushirikishwaji wa wagonjwa ili kuboresha huduma za kinga, uchunguzi na tiba.

Akizungumza, amesema kipimo hicho kimeshafanyiwa majaribio kwa nchi za Ulaya, Amerika na China.

“Kwa mara ya kwanza tunatarajia huduma hii itaanza kutumika Tanzania, pindi itakapoanzishwa itakuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kukitumia,” amesema.

Ameongeza “Kwa nchi za wenzetu {ambako kimeshatumika} kipimo hicho kimesaidia kuboresha afua zinazotumika katika kupambana na ugonjwa wa saratani.

“Kwa sababu wagonjwa wanaibuliwa mapema, wanatibiwa mapema wameweza kupunguza kwa kiwango kikubwa gharama za matibabu.

“Kwa mfano, kwa mwaka mgonjwa mmoja anaweza kugharimu Tsh. 50,000 tu na Bima zao za afya zinayamudu matibabu yao.

Tanzania ni miongoni mwa Mataifa yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani, ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) ya mwaka  2018, kila mwaka kuna wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka Tanzania.

Lakini takwimu za Wizara ya Afya Tanzania zinaonesha idadi hiyo ya wagonjwa haijawahi kufikiwa / kuibuliwa.

Takwimu zinaonesha bado kuna kundi kubwa la wagonjwa ambao hawafiki/hawajitokezi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliopo ORCI inaonesha saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni ya Tezidume 21%, Koo 11.8%, Utumbo mkubwa na mdogo 9%, Mdomo na Kinywa 7.3%.

Kwa wanawake saratani zinazowaathiri zaidi ni pamoja na ya Mlango ya Kizazi 43%, Matiti 14.2% na Koo 3.8%.

Ni takribani 80% ya wanaofika vituoni hufika huku ugonjwa ukiwa katika hatua za juu {3 na 4} ambazo ni ngumu kutibika na kupona.

IARC inaeleza takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo Tanzania. 

“Saratani ni ugonjwa mtambuka, juhudi za pamoja zinahitajika ili kupambana nayo,” amesema Meneja wa ubia, uwezeshaji na mawasiliano kwenye mradi mtambuka wa saratani {TCCP} ulio chini ya Hospital ya Aghakan Dk.Sarah Maongezi.

Ameongeza “Pale Agakhan tunapokea wagonjwa wengi, lakini wengi wamechelewa na huwa kwenye maumivu makali.

Dkt. Alphonsina Nanai kutoka WHO Tanzania anayeshughulikia Magonjwa Yasiyoambukiza {NCD's} ameipongeza Tanzania kwa kuwekeza katika huduma za tiba za kibingwa na kisasa zaidi dhidi ya saratani.

Pamoja na hilo, ameshauri ni muhimu nguvu zaidi pia ikaelekezwa katika tafiti pamoja na uelimishaji jamii  kuepuka visababishi vinavyochochea magonjwa hayo.

“Saratani imo ndani ya kundi la magonjwa, kuna magonjwa mengine pia ikiwamo ya akili na mtakumbuka mwaka jana Tanzania ilifanya kongamano kubwa la kwanza ambalo lilileta pamoja wataalamu na wananchi na kujadili kuhusu afya ya akili.

“Ni muhimu pia tukawa na kongamano la kitaifa kwa upande wa saratani, kujadili kwa kina na watafiti waje na mbinu za kusaidia Taifa dhidi ya saratani, huku pia huduma za uchunguzi wa awali zikiimarishwa pamoja na huduma za tiba za ubingwa wa juu na uelimishaji,” ameshauri.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement