Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Mwanza

Wodi maalum {NCU} ya kulaza watoto wachanga tu wanaohitaji uchunguzi zaidi wa hali zao za ki-afya baada ya kuzaliwa kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani, imeanzishwa rasmi Kituo cha Afya Buzuruga.

Kambi maalum ya 'Madaktari Bingwa wa Mama’ ndiyo waliyoanzisha wodi hiyo yenye uwezo wa kulaza watoto 16 kwa wakati mmoja.

Ndani ya wodi hiyo kila mtoto mmoja analazwa na mama yake tofauti na wodi walikokuwa wakilazwa awali ambako walichanganywa na wagonjwa wengine.

Wodi ya zamani pia walichanganywa pamoja na wajawazito wanaofikishwa kujifungua na wakati mwingine kwa sababu ya wingi wa wagonjwa walilazwa watatu hadi wanne kitanda kimoja.

Hatua ya kuanzishwa wodi mpya inatazamwa ni ukombozi kwani itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza maambukizi ya magonjwa kwa watoto wachanga pamoja na vifo vya mapema vya watoto wachanga.

Mwita Chacha ni Daktari wa Watoto, miongoni mwa wataalamu wa jopo la Madaktari Bingwa wa Mama' program maalum iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Program hiyo imeanzishwa na Dkt. Samia kupitia kampeni ya Jiongeze, Tuwavushe Salama yenye kwa lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, Tanzania.

Dkt. Chacha amezungumza na timu ya maafisa habari na mawasiliano kutoka Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya pamoja na waandishi wa habari.

Timu hiyo ipo mkoani hapa kuangazia manufaa yaliyopatikana kupitia kambi hii katika kuboresha afya ya mama na mtoto.

“Kwa kweli kituo hiki kinahudumia wagonjwa wengi hapa Mkoani Mwanza, kwa siku kinazalisha wajawazito 15 na hakikuwa na ‘unit’ za watoto kutoa huduma za watoto wachanga,” amesema.

Ameongeza “Tulifanya tathmini siku ya kwanza, tulikuta sehemu za kulaza watoto hazikutengwa na hakukuwa na watumishi wa kutoa huduma na kufanya ‘assessment’ {ufuatiliaji wa hali ya mtoto baada ya kuzaliwa}.

“Walikuwa hawafanyi baada ya mtoto kuzaliwa tu, wakiona hali ya mama ni imara na mtoto ananyonya vizuri wanamruhusu kurudi nyumbani.

“Lakini baada ya siku kadhaa baadhi ya watoto walirudishwa kituoni wakiwa ni wagonjwa. {Kwa sababu hiyo}  tumehimiza kituo kutoa kipaumbele kusaidia watoto kuwavusha salama.

Amesema uongozi wa Kituo, wilaya pamoja na mkoa walipokea wazo hilo na kulifanyia kazi hatimaye kupatikana kwa wodi hiyo.

“Watoto wachanga wote sasa wanaweza kupatiwa huduma hapa kabla ya kuruhusiwa hadi huduma ya ‘kangaroo’ kwa waliozaliwa kabla ya wakati wakiwa na uzito pungufu, inatolewa kwa usalama zaidi.

Dkt. Chacha amesisitiza “Tumeboresha pia ‘skills’ kwa ajili ya {kuhudumia}  watoto wachanga, hii ni sehemu nzuri sana hakuna tena malalamiko kutoka kwa wakina mama.

“Tulikuja na miongozo na tumeibandika kuwawezesha wale watoa huduma kuhakikisha wanatoa huduma bora.

“Utaona wodi imejaa hii inaonesha watu waliokuwa na uhitaji wa huduma ni wengi, ninatamani hii ‘mentorship’ ipelekwe na vituo vingine vya afya, ili wapate ujuzi na iwe endelevu kusaidia jamii,” amesema.

Lucy Emmanuel ni Afisa Muuguzi Msaidizi na Msimamizi wa wodi hii amesema wanamshukuru Mungu kupata wodi hiyo kwani sasa wataokoa uhai wa watoto wengi wanaozaliwa kituoni hapo.

“Tunamshukuru mno Rais Samia kwa kuwaleta madaktari hawa, sasa tupo hapa wanapata hudum kwa wakati ‘Mentorship’ imeleta matunda haya.

“Awali tulikuwa hatuwaangalii watoto wanapozaliwa sasa wanafanyiwa wakigundulika wanaletwa hapa na kufuatiliwa hali zao.

“Namshukuru Rais Samia kwa kutuletea hizi program zimetupa elimu na uwezo kusaidia watoto, tunaahidi kuiendeleza na kusimamia vema wodi hii, tumeona manufaa yake kuokoa mama na mtoto,” amesema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakina mama waliolazwa pamoja na watoto wao ndani ya wodi hiyo wamesema ni hatua ya kupongeza.

“Tunalala hapa kila mmoja na mtoto wake, mazingira ni masafi, watalaamu wanatuhudumia vizuri, wana lugha nzuri, neti na vitanda yaani ni kusafi mno, tumefarijika na tunamshukuru sana Rais Samia,” amesema Salome Mikael.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement