Na Veronica Mrema
Chumba cha siri cha Chief wa Kabila la
Wahehe, Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga maarufu Mtwa Mkwawa inahitaji ujasiri
na kujiamini kiwango cha hali ya juu kuingia.
Historia ya kipekee yenye mvuto wa aina
yake inapatikana ndani ya Tanzania pekee, katika mapango yaliyoumbwa na
kujiunda kwa mtindo wa kuvutia na wa aina yake.
Katika eneo hilo kuna mabaki ya vitu
kadhaa alivyowahi kutumia Mtwa Mkwawa ikiwamo vyungu, friji ya asili, jiwe
alilosugulia miguu yake, mafiga alipokuwa akipikiwa chakula chake.
Kuna kijito cha maji ya baraka ambayo aliwahi kuyanywa na kupona ugonjwa uliomsumbua muda mrefu akitibiwa bila mafanikio kwa dawa mbalimbali na tabibu wake.
Mapango hayo yapo pembezoni kidogo mwa Maporomoko
ya Kimani eneo la Mpanga Kipengere, Mkoani Njombe, ndiko kilipo
chumba hicho. Lipo pia bwawa lake la kuogelea kwenye maporomoko.
Kituo cha radio Highland Fm kwa kampeni yake ya ‘Kikwetukwetu’, imefanikiwa kwa ushirikiano na
wadau wake ambao wengi ni wasikilizaji wake, kufanya utalii wa ndani ndani ya
eneo hilo lililobeba historia ya Mtwa Mkwawa enzi za uhai wake.
Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la
Mbeya Triphonia Kisiga amesema eneo hilo lina mvuto wa kipekee usiopatikana
kwengineko duniani.
“Highland Fm wametushangaza, tumefurahia kwa kiwango ambacho waswahili wanasema kiwango cha lami, tumeona vitu vingi,” amesema.
Ameongeza “Tumefurahia zaidi tulipoenda
kwenye maji, chumbani cha siri cha Chief Mkwawa alipokuwa anafanya mambo yake.
“Tulivyoingia mule kwa kweli tumefurahia
sana, kilichonifurahisha zaidi namna ya kuingia kwenye chumba cha siri, wale
tulioingia mmeona.
“Kama haupo ‘strong’ huwezi kuingia
kwenye kile chumba cha siri, Kile chumba cha siri kwa kweli tumefurahia sana, ningetamani
na wenzetu wangefika kile chumba.
Amesema wamefurahia kuona mimea
mbalimbali ukiwamo wenye uwezo wa kurudisha mahusiano ya wanandoa
yaliyotetereka.
“Kuna watu wameogelea hadi katika Bwawa la Mapenzi, kila mtu
amefurahia sana, tumeona mandhari nzuri ukiwa kule Mbeya huwezi kuona mandhari
nzuri kama hii.
Amehimiza Highland Fm kuendelea kuandaa
ziara nyingine za utalii wa ndani na utamaduni ili kuzidi kuitangaza historia nzuri
ya Tanzania ambayo haipatikani kwengineko duniani.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Afisa
Utamaduni wa Mkoa huo, Victoria Shao ameongeza “Kama mkoa tumeshangazwa, hongereni
{Highland Fm} mmeweza kutufurahisha wote tuliofika hapa.
“Niwaombe tuendelee na utalii huu, kwa
sababu unakusanya watu wengi tuendelee kuenzi masuala ya utamaduni, wakati
tunapewa historia mtaweza kuona masuala ya utalii na utamaduni ni mambo
yanayoenda sambamba.
“Kuna utamaduni unaoshikika na ule
usioshikika, wa kushikika ni kama ngoma, vyakula, mimea lakini kuna masuala ya
imani haya ni utamaduni usioshikika, tumeambiwa kuna maji ya baraka ukinenea
chochote unafanikiwa.
“Tumeona vyungu, kitanda, mafiga yale
kwamba historia bado inatunzwa, niwaombe isiwe mwisho tuhakikishe tunaendelea na 'tour' hizi na kuandaa matamasha.
Amesisitiza “Tuone namna gani
tunaendelea kutoa elimu kwa jamii, tumeona kuna mmomonyoko wa maadili, tutumie
hizi ‘tour na matamasha kuhimiza watu kurudi kwenye tamaduni, mila na destuiri
zetu.
“Hata kama tunaiga tusiige yenye
madhara, tumeoneshwa kwenye vyakula vipo hadi vya mama mjamzito, tuwe mabalozi
tuendelee kutoa elimu na kuhimiza mila na desturi zetu.
Pamoja na hayo, amesema Mkuu wa Mkoa huo,
anapenda masuala ya utalii na anahimiza wadau kuendelea kuhimiza masuala ya
utalii.
Amesema mkoa huo pia utaendelea kuhimiza
utunzaji wa mazingira ili kuzidi kutunza na kulinda vyanzo vya maji kwa
upandaji miti katika vyanzo vyake na maeneo mengine mbalimbali.
Mkurugenzi wa Highland Fm Eveline Mwakyambiki amewashukuru
wadau wote walioungana na kituo hicho na kuahidi kuyatekeleza maelekezo
yaliyotolewa na viongozi hao.
Hakika kuingia kwenye Chumba cha Siri cha Mtwa Mkwawa yahitaji ujasiri.
JibuFutaChapisha Maoni