Upatikanaji duni wa huduma rafiki za masuala ya afya ya
uzazi bado ni ‘mwiba’ kwa kundi la vijana, nchini Tanzania.
Kukosekana elimu, stadi na miongozo sahihi ya afya ya uzazi
na ujinsia kwa vijana kunatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa vijana kujiingiza
katika tabia hatarishi ikiwemo ngono zisizo salama.
Athari za vitendo hivyo ni pamoja na mimba zisizotarajiwa, magonjwa
ya ngono na matumizi holela ya dawa za
kuharibu mimba.
Kuna ongezeko la wasichana wanaopata ujauzito katika umri wa
miaka 15 hadi 19 ambapo kipindi cha mwaka 2010 idadi ilikuwa 23% lakini
imefikia 27% mwaka 2015/16.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti za TDHS zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Akizungumza, Kaimu
Mkurugenzi wa Mtandao unaojihusisha na masuala ya Ukimwi na Afya Ukanda wa Afrika
Mashariki {EANNASO} Onesmus Kalama amesema..,
“Upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kwa vijana bado
haujawa rafiki kwao, wengi wanaogopa kwenda kwa sababu ni sehemu mchanganyiko.
“Kijana anaangalia je nikikutana na shangazi yangu
itakuwaje?,” amesema na kuongeza
“Ndiyo maana unakuta wengi wanakimbilia famasi wanajinunulia
bila kufuata maelekezo kwa daktari ambayo ni athari kubwa.
Amesema kwa sababu dawa nyingi wanazojinunulia hupaswa
kutolewa kwa mwongozo wa daktari lakini wao huambizana wenyewe na marafiki
kwenda kununua.
“Hawajui dawa zile wanameza zitakuwa na athari gani hapo mbele,” amesisitiza.
Tanzania bado inatajwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya
juu vya ndoa za utotoni duniani, ripoti ya TDHS ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
2015/16 imesisitiza.
Kulingana na ripoti hiyo, miongoni mwa wasichana wenye umri
wa miaka 20 hadi 24 ambapo 5.2% waliolewa wakiwa na miaka 15 huku 30.5% wakiwa
na umri wa miaka 18.
Lilian Lema ambaye ni mtengeneza maudhui mtandaoni
yanayoangazia afya ya uzazi hususan kwa kundi la vijana amesema elimu kuhusu
afya ya uzazi ni muhimu kwa kundi la vijana.
“Kwani inasaidia vijana kujikinga na magonjwa ya ngono, mimba za utotoni, wanawake wazazi ni namna gani ya kujikinga kipindi cha uzazi mpaka wanapojifungua na hata masuala ya hedhi salama.
Ameongeza “Elimu inaendelea kutolewa na kufanya uchechemuzi
kwenye kuboresha Sera zetu kuweka fedha za kutosha kwenye eneo hili.
“Pia vijana kupata elimu na huduma rafiki ili kuweza
kujitambua na kufanya maamuzi sahihi, lakini bado kuna changamoto huduma
rafiki na zisizo na unyanyapaa.
“Bado vijana wanakumbana na unyanyapaa kiasi kwamba wanaacha
kufuata huduma rafiki kwenye vituo vya afya ambako Serikali inawekeza fedha
nyingi.
“Matokeo yake wanafuata hizo huduma sehemu ambazo si sahihi
au wanakwenda kupata huduma kwa watu wasio sahihi matokeo yake wanafanya vitu
ambavyo wengi wao vinaharibu maisha yao.
Amesema kuna mimba za utotoni.., zisizopangwa, kuna
wanaopoteza uhai kwa kutoa mimba kwa njia zisizo salama, au wanapata virusi vya
ukimwi na ukimwi pale wanapotumia njia zisizo salama.
Kalama ameshauri ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa huduma
rafiki za uzazi kwa vijana zinakuwapo ili wawe na uwezo wa kwenda katika vituo
vya kutolea huduma za afya na si kwengineko.
❤️🙏🏾
JibuFutaChapisha Maoni