Na Veronica Mrema
Kaya zaidi ya 98% zilizopitiwa na mradi wa bomba la mafuta
ghafi [East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP] tayari wamefikiwa na kulipwa
fedha kwa mujibu wa Sheria ili kupisha mradi huo, Tanzania.
Ujenzi wa bomba hilo unachukua kiasi cha Km 1,443 kutoka Kabaale
Uganda hadi Chongoleani Tanga, ambapo mafuta hayo yatapakiwa kwenye meli tayari
kusafirishwa nchi mbalimbali.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano EACOP kwa upande wa Tanzania Catherine Mbatia amesema bomba hilo
litapita katika mikoa minane Tanzania.
Amesema tayari wamegawa nyumba 339 kwa waathirika ambao walichukuliwa
makazi yao kwa kupitiwa na mradi huo.
Ameongeza “Mwezi Uliopita tumegawa nyumba ya mwisho ya mnufaika,
tulikuwa na wa aina mbili kuna waliochukua ardhi tupu na kuna waliochukuliwa
makazi yao [nyumba] walikuwa 339.
“… na mwezi ulioisha tumempa mwathirika wa nyumba 339 Tanga
na wale waliochukuliwa ardhi zao namaanisha mashamba na waliopewa ‘composition’
kwa njia ya fedha karibu wote wameshalipwa.
“Wale waliopatikana na wale ambao hawajapatikana fedha zao
zipo, tuna anuwani na majina yao, tumeshatangaza kupitia vyombo mbalimbali vya
habari kwa kutumia redio za jamii na Taifa.
Amesisitiza “Tumefanikiwa kupata wengi, tumebaki na wachache
na hao fedha zao zimehifadhiwa, wakati wowote hata kama mradi utaisha wakija na
vielelezo sahihi watalipwa.
“Mradi unaendelea tumeshuhudia mwanzoni mwa Desemba hii
tumepokea mabomba, yanayokwenda kuwekwa Km. 100.
“Tunafahamu kwa Tanzania mradi huu una Km. 1443 ni mwanzo
mzuri tumeanza kupokea mabomba yatakayowekwa Km. 100.
Amesema hii inaonesha kwamba ule mradi ambao Watanzania wamekuwa
wakiusikia siku zote sasa unakwenda kutekelezeka.
“Walikuwa na hamu ya kuuona unatekelezeka kwa kupokea
mabomba hayo inaonesha sasa kazi imeanza na mradi wetu upon a Watanzania
tutaendelea kunufaika zaidi na zaidi,” amesisitiza.
Kitovu cha mradi huo ni katika Ziwa Albert huko Uganda
ambapo 80% litapita upande wa Tanzania kwa kiwango cha Km. 1,443 na Uganda
ikiwa na Km. 296.
Kampuni ya Total Energy inamiliki 62% ya hisa katika mradi
huo, Uganda kupitia UNOC ina 15%, Tanzania kupitia TPDC 15% na Kampuni ya China
CNOOC ina 8%.
Catherine ameongeza “Kwa kupita tu mradi huu Watanzania
wengi wamenufaika, ni pamoja na wakandarasi wetu wakubwa kwa wadogo wamepata tenda
nyingi mbalimbali,” amesema na kuongeza,
“Si tu wakandarasi bali hadi Watanzania wadogo wadogo kwa
sababu ajira zetu zinaanzia tangu kwenye ngazi ya kijiji, hivyo tunaajiri
katika vijiji vyote ambapo bomba hili limekatiza,” amesema.
Chapisha Maoni