Bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyokamatwa katika oparesheni maalum ya TMDA
Na Veronica Mrema
Oparesheni maalum iliyofanyika Novemba 20 hadi 24, 2023
imeibua mikoa minne vinara wa uchepushaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya
Serikali ni Dar es Salaam, Lindi, Ruvuma na Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA] Adam
Fimbo amebainisha hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari alipotoa
ripoti kuhusu oparesheni hiyo.
Ilihusisha kukamata dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya
Serikali, dawa bandia, duni, zisizo na usajili na pamoja na dawa
za kulevya.
“Hii ndiyo mikoa vinara ambako dawa za Serikali
zilichepushwa na tunaendelea kufanya upelelezi kwa wale ambao tuliwakuta nazo,”
amesema.
Ameongeza “Kwa sababu tukikuta kwenye maduka ya dawa binafsi
ameletewa, kikubwa unarudi nyuma kuangalia mtandao mzima atusaidie kutuambia
aliyeleta ni nani?.
“… na huyo aliyeleta amezipata wapi? Mpaka tujue mnyororo
mzima, turudi kwenye chanzo nani amefanya hivyo.
“Kwa sababu dawa zikitoka MSD [Bohari ya Dawa] zinaenda
hospitali kwenye utaratibu wa Serikali, tukirudi nyuma tutajua wanaohusika kina
nani?.
“Wote hao tunawafuatilia, tuwapate wote,” amesisitiza. Oparesheni
hiyo ya TMDA ilihusisha pia Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya [DCEA], Baraza la Famasi na Jeshi la Polisi.
Fimbo amesema walikamata dawa zilizokuwa na maandishi maalum
‘For GOV-TZ-NOT FOR SALE’ na nyingine zikiwa na nembo ya MSD.
Amebainisha katika oparesheni hiyo jumla ya bidhaa zenye
thamani ya Tsh. Mil. 172 zilikamatwa na walibaini wachepushaji walikuwa
wakifuta nembo za Serikali ili zisigundulike.
“Maboksi mengi yamefutwa maandishi yalisomeka GOT hizi
wamezitoa kwenye mnyororo wa Serikali, zinauzwa maduka binafsi na nyingine
tumezikuta zina nembo ya MSD,” amesema.
Amesema katika oparesheni hiyo pia wamekamata dawa bandia za
mifugo, dawa na vifaa tiba duni, zilizoisha muda wa matumizi na visivyo na
usajili au kutambuliwa na TMDA, zimekutwa zikiuzwa mtaani.
Amesema pia wamekuta dawa za TB zikiuzwa nje ya mfumo wakati
haziruhusiwi kuuzwa, dawa za uzazi na zingine za kutibu fangasi na zile za oparesheni
zinazotumika kwa nusu kaputi nazo zimekamatwa.
“Tumekamata dawa duni [zenye ubora hafifu], bandeji ambazo
ukibandika hazishiki, gozi ambazo zinapukutika tu.
Amesema walikagua majengo 777 ya sehemu za biashara na
kubaini 200 [25.7%] kati yake yalikuwa hayana usajili/ hayatambuliki kabisa.
“125 [16.1] yalikutwa na bidhaa zilizokwisha muda wa
matumizi, 84 [10.8] hayakuwa na vibali vya biashara, 67 [8.6] hayakuwa na
mtaalam, 66 [8.5] hayakuwa na nyaraka za manunuzi.
“64 [8.2] ambayo ni DLDM yalikutwa na dawa zilizoruhusiwa
kuwepo katika DLDM, 36 [4.6] yalikutwa na dawa za Serikali, 20 [2.6] yalikutwa
na bidhaa duni.
“5 [0.6] yalikutwa yanatoa huduma za kitabibu na 3 [0.4]
yalikutwa na bidhaa bandia,” amebainisha.
Ameongeza “Kufuatia matokeo haya watuhumiwa wote waliokutwa
na kuhusika moja kwa moja na kusambaza au kuuza dawa, vifaa tiba au
vitendanishi vya Serikali na bandia wamefikishwa katika vyombo vya Sheria.
“Jumla ya majalada 13 yamefunguliwa dhidi yao na taratibu za
kuwafikisha mahakamani zinaendelea katika vituo vya Polisi, jumla ya faini Tsh.
Mil. 100.8 zimetozwa .
Amesema bidhaa zote bandia, zisizo na usajili na
zilizokwisha muda wa matumizi zimeondolewa sokoni kulinda afya ya jamii.
Msajili wa Baraza la Famasia Elizabeth Shekalaghe amesema
wamekamata wauzaji wa dawa katika famasi na maduka ya dawa za binadamu na
mifugo ambao hawana utaalamu.
“Kumekuwa na dhana potofu wananchi wengi wakidhani biashara
ya dawa ni nyepesi kufanya kwa lengo la kujipatia kipato,” amesema.
Ameongeza “Dawa hizi zilizokamatwa inawezekana katika maeneo
mengine ambayo hatujafika zipo, nitoe wito kwa wataalamu wote wa dawa tutumie
weledi kufanya kazi zetu.
“Kwa waliobainika, taarifa itaebdelea kufanyiwa kazi na
iwapo kuna mwana-taaluma wa famasi amejihusisha na uuzaji dawa za Serikali,
duni, bandia hatua za ki-Sheria zitachukuliwa ikiwamo kufutiwa leseni.
Amesema kuna tabia pia ya baadhi ya wamiliki wa maduka
kununua dawa mikononi na kuwataka waache mara moja.
“Natoa wito kwa wananchi kutupatia taarifa, kila mtu
anatakiwa kuhakikisha analinda afya ya mwingine,” amesema.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu wamekamata watoa dawa
3,000 ambao waliuza bila kuwa na sifa.
Kamishna wa Polisi, Daniel Nyambabe amesema tayari majalada
13 yamefunguliwa tayari kushughulikia kesi hizo za uuzaji dawa za Serikali,
bandia, duni na zenye asili ya kulevya kinyume cha Sheria.
“Yapo hatua za upelelezi chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka [DPP],” amebainisha.
Chapisha Maoni