Na Veronica Mrema - Dodoma
Huba alilokuwa nalo na mwenza wake, mahaba mazito
waliyokuwa wakipeana, hakuwahi kufikiri hata siku moja, atamuingiza kwenye
janga zito la matumizi ya dawa za kulevya.
Ni mwenyeji wa Morogoro, Fatuma James
amelazimika kusafiri umbali mrefu na kuhamishia makazi hapa Dodoma akifuata
tiba ya Methadone baada ya kuathiriwa na heroin.
“Wanaume..., hawala wangu ndiye alikuwa ananivutisha dawa
za kulevya [lakini] mara ya kwanza aliniambia bangi tu, vuta mke wangu,”
anasimulia.
Anasema jambo lililokuwa likishangaza ni pale alipokuwa
akivuta bangi zingine hakuwa anapata hisia zile alizokuwa akizipata baada ya
kuvuta bangi ya mpenzi wake huyo.
“Nilikuwa najiuliza hii bangi gani? Mbona nahisi alosto, akinivutisha
ile yake najisikia vizuri, nikivuta bangi yangu maumivu yanaongezeka, nilikuwa
najiuliza hii ni nini?,” anasema.
Anasema siku moja alimkuta mpenzi wake akisaga kitu kwenye
jiwe, “Nilimkuta anasaga, nilimuuliza hii ndiyo bangi gani?, alinijibu kwani
ulikuwa hujui hii ndiyo dawa ya kulevya.
‘PENZI
LA UPOFU’
Anasema alihamaki na kujikuta akimuuliza mpenzi wake huyo… “Eh!
Hivi wewe kaka ni mgonjwa wa akili?, kwanini unaniingiza kwenye hili? [naye] Akaniambia
si ulinipenda?.
“.., na kweli yule kaka nilimpenda, alichokuwa ananiambia
chochote, mimi nakubali ndiyo hapo aliingiza kwenye dawa za kulevya na mimi
nikaujua ‘unga’.
Anaongeza “Niliishiwa nguvu, nilianza kulia, nilimuambia
kwanini unaniingiza kwenye janga hilo.
“Nilikuwa sijui anayetumia dawa za kulevya yupoje, sijui
hata nikutane naye niambiwe mteja nilikuwa sijui.
“Hadi nilivyotumia ndiyo nilijua aha kumbe ndiyo
wanavyodhalilishwa hivi?,” anasema, tangu hapo maisha yake yalibadilika mno.
“Mwanangu roho ilikuwa inamuuma, alikuwa ananiambia shuleni
wenzake walikuwa wanamcheka kweli mama yake anatumia ‘ma-unga’, analia.
‘KOVU
LA MOYO’
Anaongeza “Nilishajutia mapenzi na nilisema sitakuja
kupenda, nitakaa tu na mwanaume, basi kwa sababu mimi ni mwanamke, lakini huko
kupenda hapana.
“Nimevuta unga bado mdogo sana, miaka 14, nyumbani
sishikiki, yule jamaa kila akinitafuta. Shule niliishia darasa la nne, hata
kusoma sijui, ndiyo uhuni au matatizo sijui.
“Nikaanza kutoka ‘road’ namtoroka… kwa sababu yeye
akichelewa tu, naenda ‘road’ … natafuta fedha na mimi naenda kwa ‘mzungu’,
nilishapajua.
Je
kwenda ‘road’ maana yake nini? Fatuma anabainisha “Sisi
wanawake ni kujiuza tu dada yangu, unaenda unajiuza.
“Ndiyo unapata hiyo hela, mwingine kuiba hawezi umeshazoea
kujiuza, ndiyo hivyo unaenda kujiuza unapata hela.
“Unakuta li-baba lingine hujui lina Ukimwi, hujui lina
nini.., likikuambia mimi nina 20,000 hii hapa, halafu na una ‘alosto’ ili
ukidhi mahitaji yako utakubali tu.
Anaongeza “‘Alosto’ imeshaisha ndiyo unajuta, dah! Hivi
mimi… yule m-baba kweli nimelala naye bila kondom?!.
“Yaani baadae ndiyo unaanza kujutia, ‘alosto’ hapo
imeshaisha, tena ikianza wewe mwenyewe utaenda tu ‘road’.
MAJUTO
NI MENGI
Fatuma anazikumbuka siku zake za kwanza kabla hajatumbukia
kwenye janga hilo, anasema kabla ya mahusiano na mpenzi wake huyo alikuwa msusi
mzuri mno.
“Dada yangu ndiye aliukuwa ananifundisha tulikuwa wote
saluni, nilikuwa na chumba, godoro na kila kitu ndani.
“Ila nilipoanza kuvuta tu kila kitu niliuza ndani, hadi
nguo za mwanangu niliiba na kuziuza, hadi mama yangu nilishamuibia sana.
“Nina mtoto mmoja na kijana mwengine naye [ni muathirika wa
dawa za kulevya] nakunywa naye dawa hapa [Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili –
Mirembe].
Anasema mwanamke anayetumia dawa za kulevya anadharaulika
sana ndani ya jamii, jambo ambalo huwaumiza ‘moyo’ waraibu wengi.
“Wanasema lile si liteja tu, yaani ukipita mtaani, tu hadi
mwenyewe unaona aibu. Sasa utafanyaje, umeshatumia dawa, wakisema linapitia
huku linatokea huku.
“Utafanyaje?, kwa sababu umeshaingia kwenye lile janga, kwa
sababu wenyewe hawajui wewe ndiye unayejua yale maumivu, nimeshaenda sana jela,
nimeshakaa sana.
Je
amepelekwa jela mara ngapi? Anabainisha “Mara tatu nimeenda kwa kesi
za wizi, mara unaenda kulala na li-mwanaume unaliibia linakupeleka jela.
“Mama yangu, nilimuibia vitu vya ndani akanipeleka jela,
alijua mwanangu ataacha unga lakini ni vile vile.
Anaongeza “Nia ile sikuwa nayo … kuacha dawa za kulevya, ila
nilivyokuja kweny methadone naishukuru sana, ni mwaka wa pili sasa.
Anasema kwa kuwa Morogoro [kipindi hicho] hakukuwa na
kliniki ya tiba ya methadone ndiyo maana aliamua kuhamia Dodoma kufuata tiba
hiyo.
“Nakaa hapa hapa nimepanga chumba changu, nimefungua
biashara yangu, nauza chai, uji, [lakini] kabla ya yote haya nilitamani niwe
mtu mkubwa tu.
“Niwe na hela na heshima kubwa kwa jamii, kwenye ususi
inategemea na mtindo niliweza kupata Tsh. 10,000 hadi 30,000, inategemea na mtu
anavyokuja” anasema.
FUATILIENI
NYENDO
Fatuma ni miongoni mwa wanawake 12 ambao wamejitokeza
kupata tiba ya methadone kati ya waraibu 500 waliosajidiwa Mirembe.
“Sasa[wana-jamii] wanatukubali zamani walituita mteja sasa
wanasema hatuna ‘neno’ [ni watu wema] tunatumia dawa,” anasema na kueleza jinsi
alivyopata mtaji wake wa kuanzisha biashara.
“Nilimsiuka mtu yeboyebo alinilipa 15, 000 nikaanza kuuza chai, uji nikimaliza nakuja kwenye dawa. Hapa kliniki pia ni mnufaika wa mafunzo ya kilimo cha mbogamboga na nyanya.
Fatuma anashauri jamii hususan wazazi na walezi kuwa karibu
na watoto na kuhakikisha wanafuatilia nyendo zao hatua kwa hatua kwani sasa ni
kundi linalonyemelewa na ‘mapapa wa unga’.
Anawashauri pia vijana wale ambao hawajawahi kujihusisha na
biashara na matumizi ya dawa hizo wasithubutu kabisa kwani ni janga lenye
mateso mengi.
“Nawaambia majanga haya si mazuri, dawa za kulevya si nzuri
waepuke kukaa kwenye vijiwe, marafiki waepuke waangalie wenye muelekeo, si wote
wazuri
Anaongeza “Wapo wengine hawapendi maendeleo yako, sasa
wanaopotea sana ni wenye hela. Ipo mara nyingi kwa sababu fulani ameathirika
naye aje huku.
“Unaona tu yule nitamkomesha sisi msemo wetu adui yako
usimuombee njaa muombee aingie kwenye unga. Mimi sijafanikiwa ila wapo
wanaoingiza watu huku kwa sababu hiyo.
“Wazazi wawazingatie watoto wao, wawashikilie sana, hili janga
bay asana, si umezaa ua uchungu mzingatie mwanao fuatilia nyendo zake asiingie
pabaya. Sasa hivi watoto wanafuatiliwa sana.
Chapisha Maoni