Na Veronica Mrema - Dodoma
Si kila aliye karibu nawe ana mapenzi ya dhati na anapenda
maendeleo yako, wapo wanaoficha ukweli usoni mwaokwamba moyoni wanakuwazia
mabaya na wanataka kukuangusha.
Fatuma James mmoja wa waraibu wanaotibiwa kwa methadone,
Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe – Dodoma, amesema katika mahojiano
maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG.
Akiangua kilio, amesimulia alivyoanza kujihusisha kimapenzi
akiwa na miaka 14 na mwanaume mmoja ambaye ndiye aliyemuingiza katika janga la
matumizi ya ‘unga’ na kuishia darasa la nne.
Amesema mpenzi wake alimuingiza huko pasipo ridhaa yake na
kusisitiza wazazi na walezi kufuatilia kwa ukaribu nyendo za watoto wao.
Amesema mwanaume aliyekuwa naye alianza kumshawishi kuvuta
bangi aliyokuwa akiivuta yeye, hakumuambia imechanganywa na ‘unga’ aina ya
heroin.
“Nawaambia majanga haya si mazuri, dawa za kulevya si nzuri
waepuke kukaa kwenye vijiwe, marafiki waepuke waangalie wenye muelekeo, si wote
wazuri,” ameshauri vijana.
Ameongeza “Wapo wengine hawapendi maendeleo yako, sasa
wanaopotea sana ni wenye hela. Ipo mara nyingi kwa sababu fulani ameathirika naye
aje huku,” amesema na kubainisha,
Baadhi ya watu walioathiriwa na ‘unga’ hutamani kuona
wenzao ambao hawajaathirika nao wanaingia kwenye janga hilo.
“[Husema] yule
nitamkomesha sisi msemo wetu adui yako usimuombee njaa muombee aingie kwenye
unga.
“Mimi sijafanikiwa [kuingiza maadui kwenye janga hili] ila
wapo wanaoingiza watu huku kwa sababu hiyo.
“Wazazi wawazingatie watoto wao, wawashikilie sana, hili
janga baya sana, si umezaa kwa uchungu mzingatie mwanao fuatilia nyendo zake
asiingie pabaya, sasa hivi watoto wanafuatiliwa sana.
Hivi karibuni Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya [DCEA] ilitangaza kwa Umma namna ilivyoweza kubaini mtambo wa
kutengeneza biskuti za bangi.
DCEA ilibaini na kumata pia bidhaa zilizozalishwa na
kuchanganywa na bangi ikiwamo tomato sauce na juisi.
Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo alihimiza wazazi na
walezi pia kuwa karibu na kufuatilia watoto wao kwani mtandao huo sasa unalenga
watoto, kuwaingiza kwenye janga hilo.
Fatuma amesimulia mengi kuhusu maisha yake na namna
anavyopambana kuacha matumizi ya dawa za kulevya, makala hayo tutakuletea hapa
hapa MATUKIO NA MAISHA BLOG jumanne.
Chapisha Maoni