Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Manyara

Ni siku 19 sasa tangu ilipotokea janga la maporomoko ya tope mawe na maji kutoka Mlima Hanang yaliyoathiti kwa kiwango kikubwa Mji Mdogo wa Katesh, Mkoani Manyara.

Ripoti ya Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ya kipindi cha Desemba 3, 2023 hadi Desemba 22, 2023 imeeleza hatua za msingi zilizozingatiwa kuilinda afya ya jamii.

Miongoni mwa athari zilizosababishwa na maporomoko hayo ni majeruhi, vifo, uharibifu wa makazi, mali mazingira na miundombinu ya huduma za kijamii kama maji, umeme na barabara.

Anasema Halmashauri ya Hanang ina Wakazi wapatao 367,39, kati ya Kata 33 zilizopo, kata nne ndizo zilizo athirika zaidi ambazo ni Gendabi, Jorodom, Ganana na Katesh na vijiji vilivyoathirika zaidi ni Gendabi, Sarijanda, Arugushay na Sebasi.

Anabainisha hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR- TAMISEMI, Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri.

"Katika kukabiliana na athari za mafuriko hayo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri iliweza kuratibu upatikana watalaam 298 wa kada mbalimbali ili kusaidia katika utoaji wa huduma za afya kulingana na mahitaji yaliyo jitokeza," anasema. 
Anaongeza "Timu za afya zilipelekwa Hanang kutoka Mikoa ya Jirani, Hospitali za Taifa, Kanda, Maalum za Rufaa za Mikoa, Vyuo na wataalam kutoka ngazi ya Taifa kuongeza nguvu ambapo zilianza kufika Hanang siku ya tukio. 

"Wataalam wa Afya 79 ikiwemo Madaktari Bingwa 16 [Upasuaji, Magonjwa ya ndani, Afya ya Akili, Mifupa, Watoto na dharura] waliongezwa, hivyo kufanya jumla ya wataalam 298.

"Wakiwemo wa Halmashauri mbalimbali mkoani Manyara kutoa huduma kwa waathirika wakisaidiwa na timu kutoka ngazi ya taifa iliyojumuisha wataalam katika maeneo mbalimbali kama vile ugavi, maji na usafi wa mazingira, afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na uratibu.

"Elimu ya afya kwa umma, lishe, ufuatiliaji wa magonjwa, chanjo na maabara.Hadi kufikia tarehe 22 Desemba 2023, jumla ya majeruhi 139 walilazwa na kutibiwa kati yao, 18 walifanyiwa upasuaji," anasema.

Anasisitiza jumla ya waathirika 2,696 wamepata huduma za afya za nje [ikiwemo afya ya akili na msaada wa kisaikolojia].

"Majeruhi waliobaki wodini ni 5 [Manyara RRH – 4 na Hospitali ya Tumaini -1 na hali zao zinaendelea vizuri]. Aidha, Mwathirika aliebaki kwenye kambi ni 1.

Anabainisha gatua nyingine zilizochukuliwa na Wizara ya Afya zinajumuisha dawa, vifaa kinga na tiba vyenye thamani ya zaidi ya Tsh. Mil.  627.

"Vimetolewa na Serikali na wadau mbalimbali ili kuwezesha utoaji wa huduma za afya kwa waathirika, zoezi la mapokezi ya vifaa hivi liliratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu [Kitengo cha Maafa].

Anabainisha Wizara iliratibu upatikanaji wa magari ya kubebea wagonjwa [Ambulance] saba na magari mengine ya kawaida 15 yalipelekwa kwa ajili ya kusaidia huduma za majeruhi na usafiri kwa timu za kutoa huduma za afya, ustawi wa jamii pamoja na lishe.

"Hatua za kuzuia na kukabiliana na magonjwa yanayoambatana na mafuriko zimechukuliwa," anasema na kuongeza,

"Ikiwamo, tathmini ya kila siku ya afya na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya, makambi na katika ngazi ya jamii kwa kushirikiana na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii [WAJA] wapatao 50.

"Kuhakikisha kunapatikana huduma za maji safi na salama kwenye vituo vya Kutolea huduma za afya, makambini, maeneo ya kuuzia chakula na maeneo ya jamii," anasema.

Anasema Wizara ya Afya ilishirikiana na Wizara ya Maji katika kuhakikisha maji yanapatikana kwa Wastani wa Lita 240,000 mpaka Lita 300,000 kwa siku.

"Zoezi hili lilienda sambamba na upimaji na kutibu maji; ufuatiliaji wa tetesi na wagonjwa yanayotokana na maambukizi ndani ya maji [Water borne diseases] katika jamii.

"Hadi kufikia Desemba 22, 2023 zaidi ya vidonge 495,375 vya kutakasa maji vimesambazwa kwenye kaya 8,128, mafunzo maalum yamefanyika kwa watoa huduma ngazi ya jamii [WAJA] 50.

"Jumla ya vyandarua 250,000 vimepelekwa Mkoani Manyara ili kuzuia magonjwa ikiwemo malaria kutokana na uwepo wa maeneo mengi ya mazalia ya mbu.," anasema.

Anabainisha usambazaji  ndoo 224 wa matenki 34 umefanyika katika ngazi ya jamii na makambi na uwekaji wa maji kila siku katika matenki hayo unaendelea ili kukabiliana na upungufu wa maji katika jamii. 

Anasema kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na Wadau pamoja na wawakilishi kutoka katika Jamii husika wanafanya uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo.

"Pia waathirika 2,496 toka kwenye makambi na kwenye jamii wameweza kupatiwa huduma mbali mbali ikiwemo huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia ili kuwasaidia waathirika hawa kuondokana na msongo wa mawazo.

"Ili kukabiliana na athari za kijamii kutokana na janga la mafuriko elimu ya kukabiliana na majanga Pamoja na magonjwa ya mlipuko imetolewa kwenye jamii kupitia matangazo ya barabarani na vipindi vya Radio 19 na Televisheni, usambazaji wa vipeperushi 2,550. 

"Pia kwa kushirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii elimu ya ujenzi wa vyoo bora na usafi wa mazingira imetolewa kwa kaya 321 zenye wakazi 6,940," anabainisha.

Sambamba na hilo, anahimiza jamii kupuuza upotoshaji unaofanywa na baadhi ya vyombo vya habari huko mitandaoni kuhusu misaada huko Hanang.

“Mambo yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu upotevu wa misaada ya Hanang si ya kweli; na kwamba wananchi waliopokewa katika kambi walifikia 689 kutoka kaya 139 na kwa hiari yao wenyewe waliomba warejee kwa ndugu zao au makwao kwa sababu wengine hawakupoteza nyumba bali ziliharibika au ziliingia tope,” anasema.

Anasisitiza Rais Samia Suluhu Hassan alisema baada ya tathmini Serikali itawajengea nyumba watu wote waliopoteza nyumba zao katika maafa haya. 

“Kila mwananchi aliye kwenye kambi anapewa uhuru wa kuamua na akiondoka anapewa misaada stahiki ambaoo katika awamu ya kwanza kila aliyeondoka alipewa chakula cha kutosha siku 30.

"Vifaa na vitu binafsi na vya ndani lakini tumekwenda awamu ya pili ambapo kila walioacha maelezo yao wanapelekewa misaada kwenye kata wanapoishi na wanapewa vitu vinavyotosha kwa muda wa miezi sita,” anasema.

Anasisitiza "Waathirika hao wanapewa vyakula vya kutosha miezi sita na kwa sukari ni inayotosha kwa matumizi ya miezi 19, kuna unga wa uji wenye virutubisho kwa ajili ya watoto, majiko, sabuni, magodoro, na vitu vingine vingi vya ndani isipokuwa samani. 

"Hata wale ambao hawakuhamia kambini nao wamesaidiwa chakula na vitu muhimu na kwamba misaada ya chakula na vitu imefikia shilingi bilioni mbili. 

Anasema pia fedha zilizokusanywa hadi kufikia Desemba 20, 2023, ni Tsh. Bil. 5.2 akieleza fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti moja ya maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement