Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Afya ya ubongo/akili kwa watu zaidi ya milioni 76.368 ingeathiriwa kwa siku moja tu, endapo mzigo wa kilogram 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na metamphetamine zingeingia mitaani. 

Idadi ya watu hao ambao wangeathirika ni wale waliokuwa wamelengwa kufikiwa na ‘mapapa vinara wa unga’ ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

‘Wavu’ imara, intelijensia ya vyombo vya Dola umewanasa wafanyabiashara saba wakiwa na shehena’ hiyo Wilaya ya Kigamboni, Ubungo na Kinondoni [Dar es Salaam] pia Wilaya ya Iringa [Iringa].

Dawa hizo zilifungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai, ili kurahisisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania, tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya,”.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya [DCEA] Aretas Lyimo amesema hayo leo Dar es Salaam, katika mkutano wake na vyombo vya habari.

Shehena hiyo ilihifadhiwa kwa usiri mkubwa katika nyumba walizokuwa wakiishi 'mapapa' hao bafuni, chooni, chumbani hadi chini ya kitanda. Ni mtandao uliokuwa ukiitesa mno Tanzania.

“Waliokamatwa ni miongoni mwa wana mtandao mkubwa wa kimataifa, wanafanya biashara hii na usafirisha nchi mbalimbali duniani, wawili kati yao wana asili ya Asia,” amebainisha.

Amesema mtandao huo hutumia njia ya bahari kusafirisha biashara hiyo haramu kwenda kwenye nchi nyingine ambako wamekita ‘mizizi’ yao ya biashara. 

“Ukiacha dawa ya heroin inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye mimea ya afyuni [opium popy] inayolimwa katika nchi za Asia na baadhi kutoka Amerika,

“Dawa aina ya metamphetamine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine,” amefafanua.

Kamishna Jenerali Lyimo ameongeza “Dawa hii huwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbalimbali.

Amesema dawa hiyo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbalimbali za kemikali bashirifu.

“Dawa hii ni hatari kwa afya ya mtumiaji, madhara yake ni makubwa na hayatibiki kirahisi kwani mtumiaji hupata madhara ya kudumu kwenye ubongo.

“Hivyo, hupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusababisha uraibu na kuathiri mfumo mzima wa fahamu.

Amesisitiza, ukamataji wa kiasi hicho cha dawa za kulevya umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi yake ndani na nje ya nchi.

Amesema katika oparesheni hiyo iliyofanyika kipindi cha Desemba 5 hadi 23, 2023 ‘papa’ mmoja alitoroka kwenda kujificha nje ya nchi.

Amesema ila kwa ushirikiano madhubuti walionao na nchi zingine, ‘papa’ huyo alikamatwa Afrika Kusini na ataletwa kujumuishwa na ‘mapapa’ wenzake katika kesi inayowakabili.

“Tutawaleta na kuendelea kuchukua hatua, tutawasaka popote walipo duniani, tutawakamata na kuhakikisha biashara hii haiwi rafiki kwao,” amesema na kusisitiza,

“DCEA inatoa onyo kwa wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini, kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali.

“Kwani Mamlaka imejidhatiti kukomesha biashara ya dawa za kulevya kwa kufanya oparesheni katika maeneo mbalimbali nchini,” amesisitiza.

Ameongeza “Mamlaka inaishukuru Serikali ya Tanzania na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

“Tukishirikiana kwa umoja wetu tutaweza kuokoa vizazi vyetu na Taifa letu dhidi ya tatizo la dawa za kulevya,” amesisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement