Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Mgonjwa wa kwanza wa saratani anatarajiwa kutibiwa kwa kutumia mashine maalum wa kisasa wa uchunguzi na tiba dhidi ya ugonjwa huo [Pet CT Scan], mwezi huu katika Taasisi ya Saratani Ocean Road [ORCI]

ORCI tayari imesimika mashine hiyo yenye uwezo wa juu zaidi katika matibabu dhidi ya saratani na ambayo hutumiwa zaidi huko katika mataifa yaliyoendelea.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu leo amefanya ziara ORCI na kukagua mashine hiyo na kuagiza ianze kutumika kutibu Watanzania ili kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kufuata huduma hiyo."Mmeniambia Desemba 26 mtafanya majaribio ya mashine hii, sasa nataka nikija tena hapa Februari Mosi, 2024 nione imeanza kufanya kazi, Watanzania wapate huduma hapa nchini," ameagiza.

Saratani ni magonjwa yaliyo katika kundi la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaathiri idadi kubwa ya Watanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani kila mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa saratani wapatao 42,000.Takwimu za ORCI saratani zenye idadi kubwa zaidi ya wagonjwa kwa wanaume ni saratani ya tezidume 21%, saratani ya koo 11.8%, saratani ya utumbo mkubwa na mdogo 9% na saratani ya mdomo na kinywa 7.3%.

Kwa upande wa wanawake ni saratani ya mlango/shingo ya kizazi 43%, saratani ya matiti 14.2% na saratani ya koo 3.8%

.Waziri Ummy amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali afya za Watanzania kwa kuipa fedha sekta uya afya kwa ajili ya matibabu ikiwamo saratani pamoja na vifaa tiba."Kwa sasa wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa udhamini wa Serikali ni wagonjwa 42 wakiwemo wa Saratani," amesema.

Amebainisha kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba, 2023 wamepelekwa wagonjwa 15. 

“Tunataka kupunguza Rufaa za nje ya nchi ili kusogeza huduma kwa Watanzania lakini pia kuokoa fedha za Serikali," amesema.

Waziri Ummy amesisitiza Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za Saratani nchini na kuiagiza ORCI kwenda kuwajengea uwezo wataalamu waliopo Hospitali za Rufaa za Kanda na zile za Mikoa. "Hususan huduma za mkoba kwa kuwa Taasisi hiyo ni kituo cha umahiri wa Masuala ya Saratani nchini Tanzania," amesema. 

Ameitaka pia, Taasisi hiyo kuharakisha harakati za kufungua vituo katika Mkoa wa Mbeya na Dodoma ili watu wanaotaka kupata huduma za mionzi wazipate kwa haraka.Pamoja na hayo, ameipongeza kwa kazi nzuri ya kuhudumia Watanzania dhidi ya magonjwa ya saratani na kuihakikishia Serikali itatimiza wajibu wake ili wataalamu wafanye kazi katika mazingira rafiki.

Ametoa wito kwa Watanzania kuwa na tabia ya kupima Afya zao mara kwa mara ili kujua hali zao za kiafya mapema na kuanza kupata huduma mapema ikiwa watakutwa na ugonjwa huo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement