Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Vikoba [ama Saccos] na majukwaa mengine mbalimbali kwa mfano ya michezo ambayo hukusanya idadi kubwa ya wanawake, yametazamwa kwa ‘jicho la tatu’, kuongeza elimu uchangiaji damu kwa hiyari.

Wanawake wanalengwa hapa kwani ni miongoni mwa makundi ya wahitaji wakubwa wa damu hususan kipindi cha ujauzito hasa wakati wa kujifungua.

Takwimu za Mpango wa Taifa wa Damu Salama [NBTS] zinaonesha uhitaji wao ni takriban 23% baada ya kundi la wagonjwa wa saratani, siko seli na mengineyo yenye 43% na watoto chini ya miaka mitano 25%.

Lakini bado wengi wamesalia nyuma, hawajitokezi kuchangia damu kwa hiyari, kulingana na NBTS kuna takribani 14% ya wanawake nchi nzima ambao hujitolea damu kwa hiyari.

‘Vuka Mwaka na Mjamzito Mmoja’ kauli mbiu ya kampeni maalum ya shukran ya kumaliza mwaka 2023 na Jumuiya ya Wachangia Damu wa Hiyari Mkoa wa Dar es Salaam [ASBLA].

Akizungumza na MATUKIO NA MAISHA BLOG Mwenyekiti wa ASBLA Dominic Mkane amesema kampeni hiyo walilenga kuleta hamasa kwa wasio na desturi ya kuchangia damu, wajitokeze kuchangia kwa hiyari.

“Hususan wakina mama wenyewe, tukiamini kabisa sehemu kubwa ya watu wanaokuwa wazito ni kina mama lakini tunajua damu ni bidhaa adimu si ya kununua hasa kwa mwanadamu mwenyewe.

“Kwa sababu damu ya binadamu haipatikani isipokuwa kwa binadamu mwenyewe. Tuliona tusogeze hii huduma na vijana zaidi.

Amesema ili waweze kuhamasika japo kwa vijana napo kuna tatizo ama uwoga au elimu hawapati ya kutosha juu ya uchangiaji damu.

“Dar es Salama sasa tunahitaji kwenda vizuri japo idadi ya uniti tunayoitaka kwa mwaka hatujawahi kuipata, kutokananna wengi ama hawajapata elimu au wamepata lakini wanakuwa waoga kwenda.,

“Namba kubwa ni wanaume, wanawake wanakuwa wachavche ama elimu hawajaipata au waliopata au uwoga, ndiyo maana tulitenga siku tuone tunakwendaje,

“Tulivyotumia kauli mbiu tuliamini wao wangejitokeza sana, ila sisi tupo ‘kuwa-support’ tulidhani wao [wanawake] watakuwa wengi.

Ameongeza “Tumeona tutumie vikundi vya kina mama sakosi, michezo kufikisha elimu huko huo ni mkakati wetu wa kwanza, vikoba nakadhalika.

“Wanakuwa na muda wao kuna siku wanavunja vikoba, siku hiyo tutakwenda kufikisha elimu, wakishaipata tukiwaambia kuna ‘event’ hii tunaomba mfike… watakuja.

Mkazi wa Ukonga na mwana-ASBLA Herman Bukuku amesema ni mara ya 11 sasa amekuwa akichangia damu kwa hiyari kuokoa uhai wa wahitaji.

“Juzi nikapata taarifa kutoka kwa kiongozi wangu kwamba kuna kuchangia damu kina mama wajawazito ili mwaka huu waweze kuvuka salama.

“Wale wahitaji hasa wa damu na mimi nikawiwa, kabla ya hapo mara ya mwisho nilichangia Muhimbili nako ilikuwa kujitolea kwa watu wenye shida ya damu, ilikuwa Septemba, mwaka huu,” amesema.

Amesema alikuwa na mpango wa kurudi kuchangia tena kwani ni jambo jema na ni muda wake wa kumshukuru Mungu kumaliza mwaka salama.

“.., na unaposhukuru ndiyo mwanzo wa kuomba tena, ninaomba mwenyezi mungu anipe afya ili niendelee kuhudumia wengine kwa sadaka hii ambayo hata sijawahi kuihangaikia.

Amesema wengi wanaogopa kujitokeza kuchangia kwa hiyari wakihofia kupimwa magonjwa mbalimbali.

“Kutokana na maisha ya sasa ni ya shida kidogo, watu wanajiingiza kwenye matatizo mengi, sasa ni waioga kwamba akija kuchangia atapimwa yale magonjwa ya hatari.

Ameongeza “Atapimwa yale magonjwa ya hatari kwamba akigundulika ule wasiwasi utamchukua, kwa sababu wengi tunakufa kwa wasiwasi si kwa ajili ya ugonjwa.

“Kwa hiyo walio wengi mimi ninavyoona na kwa sababu  ukiwaambia anakuambia umeenda kuchangia, umepimwa kwa hiyo wengi wanaogopa kupimwa si kuchangia.

“[Lakini] hii ni sadaka ambayo haina mawaa, mimi ni mcha Mungu naomba watu waendelee kuchangia bila kujua nani inaenda kuokoa.

“Kwa sababu sadaka nzuri ni ile mkono wa kushoto usijue wa kushoto umebeba nini, mimi sadaka yangu sijui inaenda kumuokoa nani lakini naomba Mwenyezi Mungu aipokee.

Mkazi wa Ilala na mwana-ASBLA Abedi Mdavila ameongeza “Mimi ni baba wa familia nikaona ni jukumu langu kuja kuchangia.

“Mara ya mwisho ilikuwa Septemba 18, 2023 nilipiga hesabu zangu nikaona ni muda wangu wa kuja tena kuchangia damu.,

“Naweza kuwaambia watu waliopo majumbani, mtaani wawe na utaratibu wa kuchangia damu. Kuna watu wana shida kuna ajali, kuna kuvamiwa na vibaka… watu wengi wanahitaji damu.

Mkazi wa Mbezi Neema John katika maoni yake amesema wanawake wengi wanaogopa kujitolea damu wakihofia kufariki mapema.

“Ni imani iliyopo, wanasemezana kuna kufa mapema ukichangia damu, mimi nimewahi kuchangia mara moja tu, kuna ndugu yangu alipata ajali ilibidi kumchangia.

Mkazi wa Temeke na mwana-ASBLA Khalfan Akida amesema imani hiyo haina mashiko na haina ukweli halisi kwani yeye amechangia damu kwa miaka 22 sasa na hajapata tatizo lolote lile.

“Ni mchangiaji wa muda mrefu nimetambuliwa nimepewa kadi ya kielektroniki naishukuru Wizara ya Afya kwa kunitambua,” amesema.

Ameongeza “Msisitizo wangu kwa kiasi kikubwa wanaochangia ni muendelezo wa wale wale, wanaokuja wengine wanakuwa ni wachache hasa vijana.

“.., wamekuwa waoga ukiwaambia kuhusu uchangiaji damu tatizo lao nini, sijui. Lakini sisi wengine tumeshapitiliza umri sasa.

“Tunaenda 'above age', kwa hiyo tunaomba sana vijana wasione tatizo kwenye kuchangia damu.

“Ni miaka 22 sasa tangu nianze kuchangia damu na hakuna tatizo lologe, nipo safi, ‘confortable’ na hakuna madhara ambayo yamenikuta kwa kuchangia damu.

Ameongeza “Damu inahitajika sana, madhara ya watu wanaopata ajali, wajawazito wenye matatizo yanayomaliza damu nimewasaidia mno.

Mkane amesisitiza uchangiaji damu ni wa muhimu kwa wote kwani damu ya mwanadamu haipatikani popote.

“Ingekuwa inapatikana kwenye machinjio ungekuta watu wameshaweka odaa. Hii ngombe yangu, ila inabidi tuchangie.

“Sisi tunajiona wazima leo lakini baada ya dakika kadhaa tunaweza kuwa wahitaji, si kwamba mpaka uumwe malaria au ugonjwa mwingine wowote.

“.., hapana unaweza kujikwaa na damu ikavuja ukawa mhitaji wa damu, inafaa kila Mtanzania kuwa ‘member’ wa kuchangia,

“Tupo watu wapatao Mil. 60 [kulingana na Sensa ya Watu na Makazi Tanzania /NBS, hivyo] tukichangia damu itakuwa nyingi na hili tatizo tutakuwa tumelitatua,” amesema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement