Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Kila mwezi kuna takribani wasichana 10 hadi 15 ambao wanafikishwa na wazazi/walezi wao katika Taasisi ya Saratani Ocean Road [ORCI] kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya HPV.

Chanjo hiyo imethibitika kuwa na uwezo wa kusaidia mwili wa msichana kujenga kinga dhidi ya kirusi cha HPV ambacho husababisha saratani ya mlango wa kizazi/shingo ya kizazi.

Sayansi inaeleza kirusi hicho kwa kawaida hubebwa katika mwili wa mwanaume na mwanamke hupata maambukizi wakati wa kujamiiana.

Kirusi hicho huweza kuishi kwa takribani miaka 10 na zaidi ndipo kianze kuonesha dalili tangu mwanamke alipopata maambukizi.

Wasichana wanapoanza kushiriki ngono mapema hujiweka kwenye hatari zaidi kupata maambukizi hayo na kuanza kupata athari zake mapema.

Kulingana na Wizara ya Afya Tanzania, saratani ya shingo/mlango wa kizazi inaongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa Tanzania, ndiyo maana iliamua kuchukua hatua kuanzisha chanjo hiyo ili kuwakinga raia wake.

Januari kila mwaka dunia huadhimisha mwezi wa uelimishaji jamii kuhusu saratani hiyo inayoathiri mamilioni ya wanawake na kusababisha vifo vingi duniani.

“Ni kweli chanjo hiyo inatolewa kwa jamii, lakini kwanini Serikali inatangaza chanjo hiyo ni bure huku wazazi tukienda hospitali, tunatozwa Tsh. 90,000,”.

Ni swali la mmoja wa wazazi ambaye aliijuza MATUKIO NA MAISHA BLOG na kutaja hospitali ambayo alimpeleka mwanawe ni ORCI.

Mzazi huyo alilalamika kushangazwa na gharama hiyo ambayo alilazimika kuilipia kwa dozi moja na kwamba bado anatakiwa kurejea tena kukamilisha dozi ya pili ambapo atalipia tena kiasi cha Tsh. 90,000

Je! kwanini chanjo hii inalipiwa kiasi hicho cha fedha huku Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo [IVD] hutangaza kutoa bila malipo chanjo hiyo?.

MATUKIO NA MAISHA BLOG imechukua hatua, kufuatilia suala hilo ili kujua ukweli wa mambo upoje.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa ORCI Dkt. Julius Mwaiselage amethibitisha uongozi wa taasisi hiyo kuweka kiasi hicho cha fedha kwa kila dozi moja ya HPV.

“Ni ukweli chanjo hii ni bure kupitia program maalum ya Taifa ambapo hutolewa kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 9 hadi 14,” amesema na kuongeza,

“Lakini hakuna program hiyo kwa wasichana wenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea, aliyezidi umri huo ambao umewekwa kwa program ya Taifa.

“Unajua, wazazi wengi walizuia watoto wao wasipate chanjo ya HPV walipokuwa shule, inawezekana kwa sababu bado hawakujua umuhimu wake.

“Lakini sasa wamejua umuhimu wake wanakuja ili wapatiwe chanjo hii, lakini wamevuka umri wa program ya Taifa,” anasema.

Dkt. Mwaiselage anasisitiza “Hasa wale wasichana ambao walikuwa katika shule za ‘private’ [binafsi] wazazi wengi hawakuruhusu watoto wao wapatiwe chanjo hii.

“Sisi [ORCI] tuliona kundi hili tusiliache, tukaamua kuanzisha chanjo hii kwa ajili ya kuwafikia wale ambao hawakuweza kupata chanjo ndani ya program ya Taifa.

Anasema tayari wengi wapo shule za upili [sekondari] na vyuo nawazazi/walezi wengi hupeleka watoto wao ORCI kwa ajili ya chanjo ya HPV kipindi cha likizo.

Kulingana na Dkt. Mwaiselage ORCI inatoa chanjo hiyo kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 21.

Anasisitiza “Sisi hatutoi chanjo hii kwa wenye umri wa program ya Taifa, hao tunawasaidia kwa kuwaelekeza vituo vya kwenda kwa mfano Hospitali ya Mnazi Mmoja.

“Hivyo, huenda huko na kupata chanjo bila malipo kwa sababu wapo katika umri wa miaka 9 hadi 14.

“Sisi tumeweka kiasi hicho cha Tsh. 90,000 ili angalau waweze kuchangia gharama, chanjo hii tunainunua, haipo katika mpango wa GAVI.

“Tena ORCI kiasi hicho tulichoweka ni kidogo, huko kwengineko jamii inalazimika kulipia chanjo hii kwa kiasi cha Dola 100 kwa kila dozi,” anabainisha.

Pamoja na ufafanuzi huo, MATUKIO NA MAISHA BLOG imefuatilia zaidi hadi Mpango wa Taifa wa Chanjo [IVD].

“Program ya Taifa ya chanjo ya HPV bado inaendelea kwa sasa, walio na umri wa miaka 9 hadi 14 wanapata bila malipo yoyote,” anasisitiza Afisa wa IVD Lotaris Gadau katika mahojiano haya maalum.

Anaongeza “Pamoja na chanjo ya HPV, chanjo zingine zote ambazo zipo chini ya program za IVD nazo ni bure isipokuwa chanjo ya Hepatitis B.

“Inawezekana pia, huenda kuna wasichana ambao hawakupata chanjo, labda siku ambayo maafisa walipitia wao hawakuwepo,” anasema.

Anasema IVD imezifikia shule zote katika program zake za awali na kwamba ifikapo April 16 hadi 19, 2024 Wizara ya Afya inatarajia kufanya tena kampeni kubwa ya Kitaifa kufikia wasichana wengi zaidi.

“Chanjo inayotolewa sasa ni ya dozi mbili, ila ambayo tutazindua ni dozi moja, imethibitika ina uwezo wa kukinga dhidi ya kirusi cha HPV,” anabainisha.

Anaongeza “Ni muhimu mno na nakushukuru kwa taarifa hii kwani wanahabari ni kundi muhimu mno kwa ajili ya kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii kuhusu chanjo.

“Ni wazi jamii sasa imeanza kuelewa chanjo hii ni ya muhimu kwa ajili ya kuwakinga wasichana wadogo dhidi ya maambukizi ya kirusi cha HPV.

Anasisitiza “Mimi niwahimize tu wazazi/walezi pale ambapo tutatangaza rasmi kampeni ya Kitaifa waruhusu watoto wao wapate.

“Kwa sababu baada ya kampeni hii, huenda hatutakuwa na kampeni nyingine ya Kitaifa kwani tutakuwa tayari tumefikia kundi kubwa la wasichana ambalo tulikusudia kulifikia.

“Baada ya hapo chanjo itaanza kutolewa kwa wasichana wadogo walio na umri wa miaka 9 peke yake, katika program zetu, hivyo wasije wakajikuta wanaangukia kundi jingine ambalo halipo ndani ya mpango.

Kuhusu kiasi hicho cha fedha kinachotozwa na ORCI, Gadau anasema bado IVD haina taarifa rasmi juu ya jambo hilo.

“Lakini, kwa kuwa umeniambia nitafuatilia kwa kina pia ili nijue zaidi,” anasisitiza Dkt..

Dkt. Mwaiselage anaongeza “Jamii inapaswa kuhimiza wasichana wadogo kupata chanjo hiyo kwani saratani ya shingo/mlango wa kizazi inatesa wanawake wengi hivi sasa Tanzania na duniani.

“Ni kweli, inashika namba moja kwa idadi kubwa ya wagonjwa inabidi tupambane nayo, hapa ORCI 30% hadi 40% ya wagonjwa ni wa saratani hii,” anasema na kuongeza,

“Lakini ni saratani tunayoweza kuizuia/kuikinga kwa chanjo ya HPV, kwa kuwa dozi zipo mbili kwa sasa ni muhimu wakazingatia kumaliza dozi ili wapate kinga kamili.

“ORCI hatutaki kuacha msichana yeyote nyuma asipate fursa ya kupata chanjo hii, ndiyo maana tumeweka program maalum kwa ajili ya walio nje ya program ya Taifa.

“Ni lengo la dunia pia [Malengo Endelevu ya Dunia/SDG’s] ambayo yanaitaka kila nchi kuhakikisha ifikapo 2030 inatokomeza ugonjwa wa saratani ya shingo/mlango wa kizazi,” anasema.

Anaongeza “Ni muhimu pia kufanya uchunguzi wa awali ili kujua iwapo mwanamke ameanza kuonesha dalili za awali za ugonjwa [ili apatiwe matibabu mapema].

Kulingana na takwimu za ORCI zaidi ya 80% ya wagonjwa hufika ugonjwa upo hatua za juu mno [3 na 4] ambazo huwa ngumu kutibika na kupona.

Lakini ikiwa mgonjwa huwahi kugundulika mapema, hupatiwa tiba stahiki hivyo kupona kabisa na kuendelea na maisha kama kawaida.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement