Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema

Unapokula chakula huenda moja kwa moja ndani ya tumbo huko humeng’enywa na mwili kupokea virutubisho muhimu kwa ajili ya kuijenga afya yako.

Ila kwa zaidi ya miaka 23 kila wiki kuna vijana wapatao 10 ambao waligeuzwa ‘punda’,  matumbo yao yalibebeshwa na kusafirisha mizigo ya dawa za kulevya aina ya cocaine.

Yaani badala ya matumbo yao kutenda kazi ya kipekee iliyokusudiwa na Mwenyezi Mungu [kwa ajili ya chakula], wao wametumikishwa miaka yote hiyo kusafirisha ‘unga’ wa cocaine.

Safari ngumu iliyogharimu uhai na maisha ya wengi wao, kwani dawa hizo zinapomezwa na kuingia ndani ya tumbo la binadamu uwezo wa kuhimili na kukaa humo ni wastani wa saa 8 tu.

Muda huo ulipozidi zilipasuka tumboni na wakafa na wapo ambao waliishia mikononi mwa vyombo vya Dola katika nchi walizokamatwa, wakafungwa jela.

Kuna baadhi ambao walifanikiwa kumaliza vifungo vyao nje ya nchi lakini hadi leo bado wamenasa huko huko, hawana fedha za kurejea nchini na wametelekezwa.

Ni mtandao mkubwa na mpana wa watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya cocaine ambao kinara wake ni Mtanzania na himaya yake ilikuwa hapa nchini kwa miaka yote.

Dunia imekuwa ikimsaka kila kona, wahenga walisema za mwizi ni 40 kinara huyo amenasa katika ‘mikono’ ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya [DCEA], Tanzania.

Oparesheni kali za DCEA zilizotanda kila kona ya nchi, zimefanikisha kumkamata akiwa huko Boko ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Mamlaka imefanikiwa kumkamata kinara wa mtandao wa wafanyabiashara wa cocaine pamoja na jumla ya gramu 692.336 za cocaine zinazohusisha watuhumiwa wanne,”.

Ni kauli yake Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo alipozungumza leo Dar es Salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari..

Ameongeza “Mfanyabiashara huyo alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu, alikamatwa na washirika wake watatu.

“Kati yao wawili walikamatwa Dar es Salaam na mmoja katika Kijiji cha Shamwengo, Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya.

“Huyu mfanyabiashara [kinara] tuliyemkamata mtandao wake ni mkubwa, ana watu wengi ambao anawatumia katika kusafirisha dawa za kulevya, ndani ya nchi na nje ya nchi.

“Ni kati ya wafanyabishara wakubwa ambao tulikuwa tunawatafuta,” amesisitiza.

JINSI ALIVYOWATUMIA VIJANA

‘Papa’ huyo amekuwa akisafirisha dawa hizo haramu na kuziingiza nchini au kupeleka nchi zingine kwa kutumia watu maarufu kwa jina la punda ambapo wengi wao ni vijana.

Kundi la ‘punda’ wa ‘papa’ huyo lilijumuisha wanaume kwa wanawake ambao hupewa dawa hizo kuzimeza tumboni au kuweka kwenye maungo yao mengine ya mwili. 

“Dawa ya kulevya aina ya cocaine huzalishwa kwa wingi katika Bara la Amerika kusini, husafirishwa kwa njia ya anga na wabebaji maarufu kwa jina la ‘punda’ kutoka nchi mbalimbali.

 “Huwatumia kusafirisha kwa njia ya kumeza, hivyo makosa yake yanaangukia katika uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka,” amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Ameongeza “Huzimeza kwa mfumo wa ‘pipi’ ambapo kwa mara moja mtu mmoja hubeba kuanzia gram 300 hadi 1200 na baadhi yao hadi gram 2000 kwa wakati mmoja.

“Yeye ‘papa’ akishanunua huko anakonunua anawapa wale watu ‘punda’ wanazimeza na kusafirisha hadi Tanzania na wakati mwingine wanazishusha kwenye nchi mbalimbali.

“Si kwamba zote zinafika Tanzania yeye ‘ana-organize’ ule mtandao wanashusha Tanzania, wengine wanashusha kwenye nchi zingine kulingana na kule nchi anakopeleka zile dawa.

“Mtu mmoja ana uwezo kumeza gram 300 hadi 1200, wachache hasa wanawake huwa wana uwezo kumeza hadi gram 2000,” amesema na kuongeza,

“Wanasafirisha kwa usafiri wa ndege, katika ufuatiliaji tumebaini kwa wiki moja watu 10 walisafirisha dawa kwenye matumbo ndani na nje ya nchi.

Kamishna Lyimo amesisitiza “Ana mtandao mkubwa wa wabebaji ‘punda’ kutoka nchi mbalimbali.

“Huwatumia kwa njia ya kumeza kusafirisha, hivyo makosa yake yanaangukia kwenye uhalifu unaovuka mipaka. 

ASILI YA COCAINE

Cocaine ni dawa ya kulevya inayozalishwa kutoka kwenye mmea wa Coca unaojulikana kitaalamu kama ‘Erythroxylum Coca/Coca Plant’. 

Mmea huo hulimwa zaidi katika nchi za Bolivia, Peru na Colombia zilizopo huko Amerika Kusini.

Cocaine ipo katika kundi la viochangamshi kama zilizo dawa za kulevya aina ya Amphetamine, Metamphetamine na Mirungi.

ATHARI KIAFYA

Sayansi imethibitisha ni dawa hatari kwa afya ya mtumiaji kwani huathiri  huathiri uendeshaji wa mfumo wa fahamu, husababisha kukosa usingizi, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi na vifo vya ghafla.

Cocaine huweza kusababisha matatizo ya akili, husababisha hasira, ukatili, vurugu kukosa utulivu na hata mtumiaji kutaka kujiua.

 “Dawa hizi husababisha uraibu wa haraka hivyo kuwa vigumu kwa mtumiaji kuweza kuacha.

“Husafishwa kutoka nchi za mbali na ndiyo maana katika njia hiyo kuzisafirisha ni mbali ndiyo maana haisafirishwi kwa wingi,” amesema Kamishna Jenarali Lyimo.

Amesema ‘mapapa’ wa Cocaine hukwepa kusafirisha kwa njia ya bahari na kutumia ‘punda’ hao kwa sababu ya hatari iliyopo kiafya.

“Inasafirishwa kwa tumbo, kuja Afrika Mashariki ni mbali inaweza kuchukua mwezi au miezi miwili, na huko kuna ulinzi na usalama.

“Wanajikuta hawawezi kusafirisha kwa njia za boti, wanachofanya wanasafirisha kwa njia ya tumbo.

Amesema zamani walitumika njia ya vifurushi kabla teknokojia kukua kuwekwa scanner ndipo waliamua kutumia zaidi ‘punda’.

“Ikiwamo JNIA walipoweka ‘scanner’ ile mizigo ikipita unaweza kuona kilichopo ndani, sasa wanatumia tumbo baada ya teknolojia kukua.

“Wanaiona [njia ya tumbo] ni salama kwa sababu si kila abiria atapita kwenye ‘scanner’ labda u-muhisi ndiyo umpitishe kwenye 'scanner' 

WANAWAKE ‘TARGET’

Ni kundi ambalo wanaweza kubeba mzigo hadi wa gramu 2000 kwa mara moja, kutokana na asili ya maumbile ya wengi wao.

“‘Nature’ ya tumbo zao, kabla [ya kubebeshwa] wanapewa mafunzo hata mwezi mzima kula chakula kigumu, ugali ili tumbo litanuke.

“Wakijua ana uwezo wa kubeba kilo nyingi wanawapeleka,” amebainisha Kamishna Lyimo.

‘PUNDA’ WENGI WAMEFIA NJIANI

Ni safari ya majuto unaweza kusema kifo kipo mkononi kwani wengi wa ‘punda’ hao ambao hubeba dawa hizo tumboni, hupasuka na wao kufa. 

Ameongeza “‘Punda’ wake wengi wamekamatwa India, China na wamefungwa kutokana na kubeba dawa za kulevya kwa kutumia tumbo, wengine wamekamatwa.

“Afrika Mashariki, [‘papa’ huyu] ametafutwa miaka mingi, miaka yote hiyo alikuwa akitafutwa na hakuweza kukamatwa.

“‘Punda’ wake mmoja amekamatwa Msumbiji na baada ya kumaliza kifungo chake alitaka kumtumia nauli arudi Tanzania na tumemkamata yule hajarudi.

Kamishna Lyimo ameongeza “Yaani ni binadamu mwenzako unamtumia, unamfanya kama ‘punda’ mbeba mizigo kwa ajili ya biashara yako, watoto wa maskini ndiyo wanaaotumika, ndiyo wanaokufa. 

“Dawa zinapasukia tumboni mwao wanafariki, wengine wanafungwa nje ya nchi na wanatelekezwa huko hawarudi. 

“Hawa ni watu hatari ambao sisi watanzania wote tunatakiwa tuungane, kuhakikisha tunawabaini na kuchukua hatua.

“Kuhakikisha tunachukua hatua na kumaliza mitandao yote ya wasafirishaji wa dawa za kulevya nchini,” amesisitiza Kamishna Lyimo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement