Na Veronica Mrema
Ulemavu wa
kudumu atabaki nao maisha yake mwanamke mwenye busha nchini, hii ni kwa sababu hadi
sasa bado hakuna teknolojia inayotumika Tanzania kwa upasuaji wa kuliondoa.
Hii ni
tofauti na wanaume ambao ipo teknolojia ya kuwasaidia kufanya upasuaji na
kuondoa busha.
Kwa wanawake
ambao wamepata tatizo hili hali ni ngumu kwao kwani hali hiyo huwasababishia
changamoto ndani ya mahusiano na ndoa zao.
Lakini pia
imekuwa ngumu kwa wanawake wenye busha kujitokeza kutafuta tiba kwa kuhofia
unyanyapaa watakaofanyiwa ndani ya jamii zao.
“Ugonjwa wa
matende na mabusha unaenezwa na mbu aina zote na unaathiri watu wote ambao
wanaishi kwenye maeneo ambayo yana maambukizi,” anasema Dkt. Clara Mwansasu.
Ni Afisa
kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele [NTDCP]
ulio chini ya Wizara ya Afya Tanzania.
Matende na
mabusha si ugonjwa unaosababisha vifo moja kwa moja lakini madhara yake ni
makubwa kwani husababisha ulemavu wa kudumu.
Dkt. Clara
anaongeza “Unaposababisha ulemavu wa kudumu maana yake huyu mtu anaingia kwenye
umaskini.
“Kwa sababu
anakuwa hawezi tena kuzalisha mali kutokana na madhara anayoyapata. Ni ugonjwa
unaosababishwa na minyoo midogo midogo ambayo inaathiri mfumo wa maji damu.
Anafafanya zaidi, “Ukishaathiri unapelekea maji kutokurudi kwenye mfumo wake wa kawaida hivyo kujaa kwenye sehemu za miguu na sehemu za siri.
“Wanaume kwa
wanawake wote wapo kwenye uhatarishi sawia kwa sababu kwa wanawake akipata
maambukizi anaweza kupata tende likaathiri titi au sehemu za siri.
“Anaweza kupata
tende kwenye miguu au mkono, inategemea vile vimelea vimejikita zaidi sehemu
gani,” anasema na kuongeza,
“Kwa wanaume
kadhalika wanaweza kupata tende sehemu za miguu, mikono na wao pia wanaweza
kupata madhara kwenye sehemu za siri na kupelekea ngirimaji au busha.
Anasema mtu
anaweza kupata maambukizi ya ugonjwa huo katika umri mdogo ila madhara yake
yakajitokeza baada ya miaka 10 au 15.
“Pale unapoanza
kuzalisha uchumi athari zinajitokeza,” anasema.
Anasisitiza kutegemea
na kiungo kilichoathirika, mathalani mtu akiathiriwa mguu au mkono hakuna namna
yoyote ile ya kurekebisha uwe katika hali ya kawaida.
Mtu husika
hupewa elimu jinsi ya kutunza tende alilopata ili asipate maambukizi na hii ni
kwa wote wanaume na wanawake.
Anaongeza “Kwa
wanawake ni tofauti wakipata sehemu za siri huwa hakuna namna ya kurekebisha,
“.., tofauti
na wanaume wakipata busha huwa wanafanyiwa upasuaji kuondosha maji na anarudi
kuwa kawaida.
“‘Advantage’
[kwa] mwanaume akipata sehemu za siri anafanyiwa upasuaji kurekebisha/kutoa busha
kwenye mfuko wa korodani anarudi kawaida.
“Mwanamke akipata
madhara inakuwa inampelekea ulemavu wa kudumu,” anasema.
Anaongeza “..,
na wanawake wanapopata madhara haya mfano sehemu za siri mara nyingi huwa
wanapata changamoto kwenye tendo la ndoa.
“[Ndoa] huvunjika
na hupata unyanyapaa kwenye jamii, ni changamoto kwa kuwa hamna namna ya
kurekebisha, ataishi na ulemavu huo wa kudumu.
Je wanawake wangapi hujitokeza kutafuta tiba? Anafafanua ni wanawake wachache mno hufika vituo vya huduma za afya kutafuta tiba.
“Hatuna suluhisho lakini pia bado wanaogopa kujitokeza
kwa sababu ya unyanyapaa," anabainisha na kwamba huishi wakiwa na msongo wa mawazo.
Je, Wizara ya Afya inafanya nini
kuokoa jamii yake,? Dkt. Clara anabainisha,
“Inatekeleza mpango/program ya kupambana na magonjwa
yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwa mojawapo ni matende na mabusha.
“Lakini afua
tunayoitekeleza sasa ni umezeshaji wa dawa kinga kwenye jamii zilizoathirika.
Anasema ili tuitekeleze
program hiyo Wizara ilifanya tathmini nchi nzima na kujua halmashauri 119 kati
ya 184 zilizopo Tanzania Bara zilikuwa zimeathiriwa na matende na mabusha.
“Baada ya
kuainisha ukubwa wa tatizo kwa nchi nzima hizo halmashauri zote ziliingia
kwenye program ya kumezesha dawa mara moja kwa mwaka.
“Kwa mwongozo
wa WHO dawa zinapaswa kumezeshwa angalau mara moja kwa miaka mitano mpaka sita
na ukifikia walengwa wote ambao ni miaka mitano kwenye jamii,” anasema.
Anaongeza “Ukishafanya
hivyo unafanya tathimini kuangalia ukubwa wa tatizo.
“Mwaka huu
tumekuwa tukifanya na sasa hizo 199 zilizokuwa zimeathirika maambukizi
yameshuka.
“Tumebaki na
halmashauri saba ikiwamo Kinondoni, Lindi MC, Mtwara Mikindani, Mafia na
Pangani, tunaenelea na umezeshaji dawakinga, wasipate maambukizi.
“Tunafanya ‘mass
program’ [kampeni kubwa kwa jamii kubwa zaidi],” anabainisha.
Anaongeza “Wito
wangu kwa wakina mama na jamii kwa ujumla maeneo ambako bado yana maambukizi wanajitokeza,
tunaomba wajitokeze kwa wingi wapate dawa
“Ikizingatiwa
madhara uya ugonjwa huu hujitokeza baada ya muda, wahimize pia watoto wafike
dawa hizi ni salama hazina madhara yoyote.
“Wanaume pia washiriki kwa sababu pamoja tukiungana tunaweza kutokomeza magonjwa haya yaliyokuwa hayapewi kipaumbele,” ametoa rai.
Januari 30, 2024 Tanzania itaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Kupambana na Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele [NTD's].
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema 'Tuungane, Tuchukua Hatua kutokomeza Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele'..
Chapisha Maoni