Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Binadamu anapoendekeza uchafu kwa kujisaidia hovyo kinyesi au mkojo katika maeneo mbalimbali hasa kandokando ya maji yaliyotuama, mabwawa, madimbwi na ziwa ni chanzo cha kueneza kichocho.

Kwa sababu mtu mwenye maambukizi au ugonjwa wa Kichocho hutoa mayai ya minyoo ya Kichocho kupitia kinyesi au mkojo wake pale anapojisaidia.

Mayai hayo yanapofika kwenye vyanzo vya maji yaliyotuama (mfano ziwani) huingia kwenye konokono ili kuanguliwa.

Konokono hao hutoa vimelea vinavyosambaa ndani ya maji ambavyo hupenya kwenye ngozi ya binadamu pale anapofanya shughuli zake kwenye maji hayo.

"Kwa mfano kuogelea, kufua, kuosha vyombo, shughuli za kilimo na uvuvi," amesema Afisa Programu Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele [NTDCP] Isaac Njau.

Ameongeza "Mzunguko huu huendelea kujirudia endapo hatua madhubuti za kudhibiti maambukizi hazitachukuliwa

Amesema sayansi inabainisha kuna aina kuu mbili za kichocho ambavyo ni kichocho cha tumbo na kichocho cha kibofu.

"Kichocho cha kibofu cha mkojo kinaambukizwa na minyoo inayopatikana kwenye maji yaliyotuama kama vile mabwawa, madimbwi au ziwa na wanaingia kwenye mwili wa binadamu kupitia ngozi.

"Kichocho cha tumbo husababishwa na minyoo midogo aina ya “Schistosoma mansoni” inayoishi katika mishipa ya damu inayozunguka utumbo mpana.

"Kichocho cha kibofu cha mkojo husababishwa na minyoo midogo aina ya “Schistosoma haematobium”, inayoishi kwenye mishipa ya damu inayozunguka kuta za kibofu cha mkojo.

"Minyoo hii hupatikana kwa wingi kwenye maeneo mbalimbali hususan kandokando ya maji yaliyotuama, mabwawa, madimbwi na ziwa," amebainisha na kusisitiza

"Binadamu ndiye chanzo cha kwanza kabisa kusambaza ugonjwa huu, yeye ndiye mbebaji wa minyoo hii na anaeneza kwa njia ya kujisaidia katika vyanzo vya maji.

Amesema ili kuepuka ugonjwa huo ni muhimu kuimarisha usafi wa mazingira na kwamba wananchi ambao wanaugua ni muhimu kuwahi tiba.

“Binadamu huambukizwa ugonjwa huo kwa kugusa maji hayo,kuogelea au shughuli za umwagiliaji wa mazao pamoja na kufua,

"Ni muhimu pia kupata dawakinga ambayo hutolewa na Serikali ili kuikinga jamii yake kwa kupunguza maambukizi.

Kichocho ni miongoni mwa magonjwa yasiyo katika kundi la Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele [NTD's].

Dkt. Njau amesisitiza "Endapo mazingira yataboreshwa na kuwa masafi maambukizi pia yanapungua ndio maana huwa tunawahimiza wananchi wawe na vyoo bora na wavitumie, wazingatie usafi," ametoa rai.

Amesema ugonjwa wa Kichocho ni tofauti na magonjwa mengine kama maralia kutokana na dalili zake kuchukua muda mrefu hadi kuonekana.

"Dalili kubwa za ugonjwa huu ni kupata homa, maumivu ya tumbo na unapojisaidia haja kubwa inakuwa imechanganyikana na damu," amesema.

Amesema jamii inashauriwa mgonjwa kuwahishwa katika kituo cha kutolea huduma za afya ili afanyiwe uchunguzi wa kina na kupatiwa ushauri na tiba stahiki.

"Kichocho cha tumbo mgonjwa huwa na maumivu sehemu ya chini ya tumbo au chini ya kitovu na hivyo kupelekea kukojoa damu

Amebainisha dawakinga hutolewa kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kutokana na michezo yao mbalimbali ambayo hucheza [kwa mfano kupendelea kuogelea ziwani].

"Hivyo kupelekea kuwa na maambukizi kuliko watu wazima tunapowapa dawakinga tunakuwa tumeisaidia jamii kwa kiasi kikubwa," amefafanua.

Amesema madhara ya ugonjwa huo hutokea kwenye mfumo wa chakula ikiwamo kuharibu utumbo mkubwa na kusababisha saratani ya tumbo.

Amesema Kichocho huharibu ini, husababisha tatizo la tumbo kujaa maji pamoja na kuleta hali ya kutapika damu kwa mgonjwa.

"Kichocho huathiri mfumo wa mkojo na husababisha figo figo kujaa maji, husababisha uvimbe kwenye figo pia huweza kusababisha saratani ya kibofu cha mkojo kwa mgonjwa," amebainisha.

Januari 30, 2024 Tanzania kupitia Mpango huo ulio chini ya Wizara ya Afya itaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele [NTD's].

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yamepewa kauli mbiu isemayo 'Tuungane, Tuchukue Hatua Kutokomeza Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele].

Tanzania inaungana na mataifa mengine ikiwa ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa [UN] ambapo kupitia Malengo Endelevu ya Dunia [SDG'S] imekusudia kutokomeza magonjwa hayo ifikapo 2030.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement