Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Mtoto mmoja ambaye alizaliwa na tatizo la jinsi tata [ambigious genitalia] amefanyiwa upasuaji mkubwa wa kutengenezwa njia ya kike ya uzazi [uke].

Wataalamu mabingwa wametumia ngozi iliyochukuliwa kutoka kwenye mwili wake kisha kutengeneza njia hiyo ya uzazi.

Hatua hiyo imefanyika baada ya vipimo vya kimaabara kuthibitisha mtoto huyo kibaiolojia ni mwanamke kwani ana via vya uzazi vya kike ndani ya mwili wake na si mwanaume kama ulivyo muonekano wa nje.

Ni upasuaji mkubwa wa aina yake uliofanyika kwa mara ya kwanza ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH] Januari, 2024 ambapo watoto 31 wametibiwa matatizo mbalimbali ikiwamo 6 wenye jinsi tata.

“Mmoja aliyefanyiwa upasuaji wa kipekee ni kutengenezewa njia ya kike kwa kutumia sehemu ya mwili wake, hatukuwahi kufanya upasuaji huu hapa [Muhimbili],”.

Yamebainishwa hayo na Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo [Uroloji] MNH Gabriel Mtaturu hii leo alipozungumza mbele ya waandishi wa habari hospitalini hapo.

Amesema pamoja na huyo yupo mtoto mwingine ambaye alizaliwa na njia mbili za haja ndogo jambo ambalo si la kawaida.

“Kwa hiyo tumeondoa njia moja na kubaki na moja, yupo vizuri [baada ya upasuaji] na anafurahia,” amesema na kubainisha watoto wote waliofanyiwa upasuaji na tayari wamerejea nyumbani.

Jinsi tata ni tatizo ambalo mtoto mmoja kati ya watoto 5,000 wanaozaliwa hai, huzaliwa nalo duniani.

Ikiwa utachukua watoto waliozaliwa na maumbile ambayo hayajakaa sawa sawa basi unapata mtoto mmoja katika kila watoto 300 ambaye amezaliwa na tatizo la jinsi tata, duniani.

Wataalamu mabingwa wa upasuaji wa watoto wanatafsiri jinsi tata ni hali ya ulemavu ambayo mtoto huzaliwa nayo.

“Unaweza kuona wa kiume kule ndani kuna via vya uzazi vya kike, kwa kutumia njia ya kifaa cha kamera, tukiingiza tumboni tunaona via vya uzazi, mayai.

Wapo pia watoto ambao huwa na muonekano wa kike lakini kwa ndani yao wana via vya uzazi vya kiume.

Kuna ambao huwa si rahisi kabisa kuwatambua kwa kuwaangalia muonekano wa via vyao vya uzazi kwa nje hivyo uhitaji uchunguzi zaidi kwa kutumia vipimo vya kimaabara vya kisasa ikiwamo kile cha DNA.

Daktari Mshauri Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Muhimbili Petronila Ngiloi amefafanua “Unaweza kuweka katika makundi matatu.

“Kuna mtoto anazaliwa ukiangalia maumbile ni mvulaana ila kiuhalisia ni msichana, kuna mwingine ukimuangalia hivi anaonekana ni msichana lakini kiuhalisia ni mvulana.

“Kuna kundi la tatu ambalo ndilo gumu zaidi anazaliwa na jinsi zote mbili, ukimuangalia maumbile ya nje unaweza kuhisi ni mvulana lakini ki-uhalisia ana jinsi zote mbili ni mvulana na msichana wakati ule ule.

Amesema kwa sababu hiyo kuna ulazima na umuhimu kwa jamii kufahamu mtoto/watoto wanapaswa kuchunguzwa vema maumbile yao ya uzazi tangu wakiwa katika umri mdogo.

“Kwa sababu mama anapojifungua tu, mkunga humtaarifu kwamba hongera mama umepata mtoto wa kiume au hongera mama umepata mtoto wa kike.

“Sasa baada ya hapo, wa-mama wengi hawana tabia ya kwenda kumkagua mtoto wake vizuri.

“Kama umepata mtoto wa jinsi ya kiume ile inakuwa ni rahisi, unamuangalia kwenye mfuko wake wa uzazi [korodani] kwa sababu upo nje.

“Unaangalia kama kuna korodani mbili, kama ipo moja ni tatizo,” amesema na kuongeza,

“Kama hamna tatizo pia ni tatizo kwa hiyo ujue kabisa mtoto wangu huyu itahitaji kwenda hospitali apate uchunguzi.

Amesisistiza “Kwanini tunashauri mtoto achunguzwe akiwa mdogo huyu aliyezaliwa na muonekano wa kiume halafu kumbe ni mwanaume.

“.., akakuzwa hivyo mpaka akawa mkubwa, shida inakuja wakati wa balehe, tunajua huyu ni mvulana na jamii inajua ni mvulana na jina ana la kiume.

“Lakini inapofika balehe anaanza kupata hedhi, maumbile ya kike pale ni shida anaota matiti, ngozi nyororo kwa sababu anakuwa na zile homoni za kike.

Ameongeza “Wengi ni wakati ule anakuja hospitali [ili] kusimamisha tu ile hedhi, tunapomchunguza tunamuambia wewe ni mwanamke si mwanaume.

“Lakini kwa sababu umri unakuwa umeenda anakuja na miaka 15, 17 wengine umri umeenda hadi miaka 30.

“Ukimuambia tukurekebishe uwe kwenye jinsi yako sahihi wengi wanakataa kwa sababu ya ile hali ya jamii inamuonaje?,” amesema.

Kutokana na hali hiyo wengi hufanya maamuzi magumu ya kubaki vile vile walivyo kulingana na namna ambavyo jamii inawatambua.

Kwa uamuzi huo hubakia na via vya uzazi ambavyo si vya uhalisia wake kibaiolojia hivyo huwa hawana uwezo wa kutengeneza/kuzalisha mtoto/watoto.

Sayansi inaeleza tatizo hili linaweza kutokea hata pale kunakuwa na muungano wa mbegu za kiume na kike.

“Vile vinasaba ambavyo vinatengeneza utu wetu kunaweza kutokea tatizo labda kitu kidogo [kwa mfano / labda] kimenyofoka pale kinaleta kule kuzaliwa na lile tatizo,” amebainisha Dkt. Ngiloi.

Ameongeza “Huwezi kumlaumu mzazi yeyote kati ya mwanaume au mwanamke tunaita ile ni kama bahati mbaya.

“Ukubwa wa tatizo hili kwenye jamii bahati mbaya hatujalifanyia sana utafiti, lakini ni shida ambayo tumekuwa tukiiona tangu [miaka ya nyuma].

“Tumekuwa tukifanya marekebisho lakini kwa vifaa vilivyokuwa duni sana, tunataka jamii ielewe umuhimu wa kuwaleta watoto wa namna hii kusudi tuwafanyie marekebisho.

Amefafanua “Kwa aina ya tatu wenye jinsi mchanganyiko, tatizo hilo si tu maumbile ya nje tunavyoona muonekano anakuwa wa kiume na ndani anakuwa na sehemu ya jinsi ya kike,.

“Bahati mbaya chochote tutakachofanya  hatakuwa na uwezo wa uzazi, ni yeye ataamua abaki na jinsi ya kike au kiume.

“Tunawaasa wazazi mtoto anapozaliwa mumkague vizuri maumbile yake ili kusudi kama kuna dosari waweze kufanyiwa uchunguzi,” amesisitiza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema watoto 31 waliofanyiwa upasuaji walikuwa kati ya umri wa miezi 18 na miaka 24.

Amesema Muhimbili ilishirikiana na wataalamu wenzao kutoka Ireland na Bahrain.

“Jinsi tata ni changamoto kwenye jamii kwa sababu mtoto anafikiria yeye ni mwanaume, wazazi wanafikiria ni mwanaume.

“Tumefanya marekebisho na watoto waliozaliwa na sehemu moja tu haja kubwa inatoka hapo, haja ndogo inatoka hapo.

Ameongeza “Dhumuni kubwa ni kwamba unarekebisha tatizo lililopo pia unapunguza yule mtoto kuishi bila ile aibu kubwa.

“Inamsaidia mtoto kama kuna viungo vyote viwili kike na kiume, tunatizama kwa ndani vipoje, vimekaa upande gani zaidi.

“Hili tunalieleza kwa sababu ni muhimu jamii ikaelewa kwa kina watoto wetu wakizaliwa ni muhimu kukagua vile viungo vipo sawa sawa/.

Amesisitiza “Kuna kitu unaona changamoto fika kituo cha afya au hospitali iliyo karibu na wewe badala ya kuwa na dhana zisizofaa.

Amesema Muhimbili inaendelea kujiimarisha na kufanya upasuaji wa kisasa zaidi ili kurejesha furaha kwa wananchi, kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika nje ya nchi na kuimarisha utalii tiba.

“Nia yetu kubwa tumeweza kumrejesha mtoto kwenye hali yake ya kawaida, arudi kucheza na wenzake, arudi shule kwa sababu ndiyo madaktari, wanasheria wetu wa miaka ijayo.

“Fedha nyingi zinaokolewa za kigeni ambazo sasa ni changamoto, zote zibaki humu ndani, kupitia Wizara yetu tunafanya utalii tiba.

“Una sehemu mbili, kwanza kuna wtanzania ambao wana uwezo kupanda ndege kwenda kufuata amatibabu, wakija hospitali zetu za Muhimbili, JKCI, MOI, BMH na kwengineko.

“Tuna wale [wagonjwa] wanaotoka nchi za jirani huu ni mchango wetu mkubwa ndani ya nchi,” amebainisha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement